Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watoto wenye Down syndrome wana uwezo wakipewa nafasi - Ceodou Mandingo 'Babuu wa Kitaa'

Ceodou Mandingo 'Babuu wa Kitaa' (aliyevaa kofia), Mtetezi wa watu wenye Down Syndrome.
Ceodou Mandingo (Babuu wa Kitaa)
Ceodou Mandingo 'Babuu wa Kitaa' (aliyevaa kofia), Mtetezi wa watu wenye Down Syndrome.

Watoto wenye Down syndrome wana uwezo wakipewa nafasi - Ceodou Mandingo 'Babuu wa Kitaa'

Afya

Hii leo katika kuadhimisha siku ya kimataifa ya kuhamasisha kuhusu ugonjwa unaothiri uwezo wa mtu kujifunza au Down syndrome tutamsikia Ceodou Mandingo almaarufu Babuu wa Kitaa wa nchini Tanzania ambaye ni mzazi mwenye mtoto aliye na changamoto hiyo na ameikubali hali ya mwanaye na anajitahidi kuelimisha umma kuhusu ugonjwa huo. Kumbuka kuwa mwezi Desemba mwaka 2011, Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kupitia azimio namba (A/RES/66/149) lilitangaza Machi 21 kuwa Siku ya Kimataifa ya Down Syndrome. Maadhimisho ya kwanza yalianza mwaka uliofuata.  

Ili kuongeza ufahamu wa umma kuhusu ugonjwa wa Down Syndrome, Baraza Kuu linaalika Nchi Wanachama wote, mashirika husika ya mfumo wa Umoja wa Mataifa na mashirika mengine ya kimataifa, pamoja na mashirika ya kiraia, ikiwa ni pamoja na mashirika yasiyo ya kiserikali na sekta binafsi, kuadhimisha Siku hiyo kwa namna inayofaa.

Ugonjwa wa Down syndrome hutokea wakati mtu ana nakala ya ziada ya ya kromosomu 21. Bado haijafahamika kwa nini ugonjwa huu hutokea, lakini Down syndrome daima imekuwa sehemu ya binadamu. Inapatikana katika maeneo yote duniani kote na kwa kawaida husababisha athari tofauti kwenye mitindo ya kujifunza, sifa za kimwili na afya.

Upatikanaji wa kutosha wa huduma za afya, programu za kuchukua hatua mapema, na elimu-jumuishi, pamoja na utafiti unaofaa, ni muhimu kwa ukuaji na maendeleo ya mtu binafsi.

Harakati za 'Babuu wa Kitaa'

Tazama video hii kusikia harakati za 'Babuu wa Kitaa' nchini Tanzania ambaye anahamasisha wazazi wenye watoto wanaougua Down Syndrome wasiwafiche bali wawatoe nje na wahakikishe wanapata huduma zinazostahili.

Inakadiriwa matukio ya ugonjwa wa Down syndrome ni kati ya mtoto 1 kati ya watoto 1,000 hadi mtoto 1 kati ya watoto 1,100 wanaozaliwa hai duniani kote. Kila mwaka, takriban watoto 3,000 hadi 5,000 huzaliwa na ugonjwa huu wa changamoto za kromosomu.

Ubora wa maisha ya watu walio na ugonjwa wa Down syndrome unaweza kuboreshwa kwa kukidhi mahitaji yao ya afya, ikiwa ni pamoja na kuchunguzwa mara kwa mara na wataalamu wa afya ili kufuatilia hali ya akili na kimwili na kutoa huduma kwa wakati unaofaa iwe mazoezi ya viungo (physiotherapy), mazoezi  kuweza kumudua shughuli mbalimbali, mazoezi ya kuzungumza, ushauri au elimu maalum. Watu walio na ugonjwa wa Down syndrome wanaweza kupata maisha bora zaidi kupitia utunzaji na usaidizi wa wazazi, mwongozo wa matibabu na mifumo ya usaidizi ya kijamii kama vile elimu-jumuishi katika viwango vyote. Hii inarahisisha ushiriki wao katika jamii kuu na utimilifu wa uwezo wao binafsi.

Komesha dhana potofu

Fikra au dhana potofu ni wazo ambalo watu wanalo kuhusu mtu au kitu kilivyo. Fikra potofu zinaweza kuwa chanya, hasi, au zisizoegemea upande wowote, lakini mara nyingi si sahihi.

Dhana potofu mara nyingi hutegemea maelezo machache au uzoefu wa kibinafsi. Dhana potofu zinaweza kuimarishwa na jinsi kitu kinavyowakilishwa katika vyombo vya habari au kwa mitazamo ya kitamaduni. Mara baada ya kuundwa, dhana potofu inaweza kuwa vigumu kubadili.

Kwa watu walio na ugonjwa wa Down syndrome, dhana potofu zinaweza kuzuia kutendewa kama watu wengine. Hata wanapokuwa na umri mkubwa jamii inaweza kuwatendea kama vile ni watoto, hawathaminiwi, na wanatengwa. Wakati fulani wanatendewa vibaya sana au hata kunyanyaswa.