Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wananchi DRC eleweni na ikubalini dhamira ya UN ya kulinda raia - TANZBATT-11

Kamanda wa TANZBATT-10, Luteni Kanali John Peter Kalabaka akimkabidhi bendera ya Tanzania Luteni Kanali  Vedasto Ernest Kikoti ikiwa ni ishara ya kukabidhiana majukumu ya ulinzi wa amani huko Beni Mavivi jimboni Kivu Kaskazini nchini Jamhuri ya Kidemokra…
TANZBATT-10
Kamanda wa TANZBATT-10, Luteni Kanali John Peter Kalabaka akimkabidhi bendera ya Tanzania Luteni Kanali Vedasto Ernest Kikoti ikiwa ni ishara ya kukabidhiana majukumu ya ulinzi wa amani huko Beni Mavivi jimboni Kivu Kaskazini nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC.

Wananchi DRC eleweni na ikubalini dhamira ya UN ya kulinda raia - TANZBATT-11

Amani na Usalama

Hii leo huko jimboni Kivu Kaskazini mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, kikosi cha 10 cha Tanzania (TANZBATT-10)  kilichoko kwenye brigedi ya mapigano (FIB) ya ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani nchini humo, MONUSCO imekabidhi majukumu kwa kikosi cha 11, TANZBATT-11, katika hafla iliyofanyika eneo la Beni-Mavivi. Msimulizi wetu ni Kapteni Abubakari Muna, Afisa Habari wa TANZBATT-10.

Mkuu wa TANZBATT-10 Luteni Kanali John Peter Kalabaka amekabidhi bendera ya Tanzania kwa Kamanda wa TANZBATT-11 Luteni Kanali Vedasto Ernest Kikoti ikiwa ni ishara ya kuanza majukumu ya ulinzi wa amani, katika tukio ambalo mgeni rasmi alikuwa Kaimu Kamanda wa FIB-MONUSCO Kanali Alex Tamson Malenda.

Akizungumza kwenye hafla hiyo Luteni Kanali Kalabaka amesema kwenye upande wa operesheni wameweza kukabili na kupunguza mashambulizi yanayofanywa na vikundi vilivyojihami kwenye eneo la ulinzi la TANZBATT-10 halikadhalika kuepusha mauaji ya raia wasio na hatia na pia kuepusha vitendo vya ubakaji.

“Kijamii tumeweza kushirikiana na jamii ya hapa Beni-Mavivi na pia kuwapatia misaada mbali mbali ya kijamii,” amesema Mkuu huyo wa TANZBATT-10.

Luteni Kanali Vedasto Ernest Kikoti ambaye amepokea jukumu la ulinzi akaeleza bayana kuwa watatekeleza majukumu yao vyema kwa kuzingatia taratibu za Umoja wa Mataifa na kwamba watakuwa tayari kuendelea kushirikiana na raia. 

“Tunaomba wananchi wakubali na waelewe dhamira hiyo, waukubali Umoja wa Mataifa ili kuupa nafasi uweze kutekeleza wajibu wake wa kulinda wananchi wa DRC,” ameeleza Luteni Kanali Kikoti.

Makofi Bukuka Gervain ambaye ni Chifu wa eneo hilo akashukuru TANZBATT-10 kwa ushirikiano walioonesha wakati wote wa kipind ichao cha ulinzi wa amani Beni-Mavivi na kueleza kuwa Kamanda wa Kikosi hicho alikuwa yuko karibu sana na wanajamii akitolea mfano wakati wa michezo ikiwemo mpira wa miguu.

“Ushirikiano wao na sisi umewezesha raia kufungua nyoyo zao na kuondokana na fikra zao za kupiga mawe MONUSCO barabarani. Sasa barabara zilibaki wazi na MONUSCO wakafanya kazi yao vema,” amesema Chifu Makofi

Meja Fatuma Haruna Makula, wa TANZBATT-11 ameahidi kuendeleza uhusiano mzuri kati ya wanajeshi wanawake kutoka Tanzania na wanawake wa Beni-Mavivi akisema, “wanawake maafisa na askari tuliokuja hapa wote tumepita mafunzo mbali mbali kuhusu suala zima la ulinzi wa amani. Tutahakikisha wanashiriki vema shughuli za ulinzi wa mani kwa mujibu wa taratibu za Umoja wa Mataifa chini ya MONUSCO.”

 

Imeandaliwa na Luteni Abubakari Muna, Afisa Habari, TANZBATT-10