Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

CSW68: Ujumuishi wanawake kifedha Rwanda umefikia asilimia 92

Waziri wa Rwanda wa Jinsia na Uendelezaji wa Familia  Valentine Uwamariya akihutubia kikao cha mawaziri katika moja ya vikao vya mkutano wa 68 wa Kamisheni ya Hali ya Wanawake duniani, CSW68 kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani
Video ya UN
Waziri wa Rwanda wa Jinsia na Uendelezaji wa Familia Valentine Uwamariya akihutubia kikao cha mawaziri katika moja ya vikao vya mkutano wa 68 wa Kamisheni ya Hali ya Wanawake duniani, CSW68 kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani

CSW68: Ujumuishi wanawake kifedha Rwanda umefikia asilimia 92

Wanawake

Mkutano wa 68 wa Kamisheni ya kwenye kumbi mbalimbali za makao makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani, Mawaziri kutoka nchi wanachama wan chi 193 wa umoja huo wamepata fursa ya kuelezea kile ambacho nchi zao zinafanya ili kutekeleza maudhui kipaumbele ya mkutano huo ambayo ni  “Chagiza mafanikio ya usawa wa jinsia na uwezeshaji wanawake wote na wasichana kwa kuondoa umaskini na kuimarisha taasisi na ufadhili kwa kuzingatia jinsia.”

 

RWANDA:  Ujumuishaji kifedha wanawake umefikia asilimia 92

Valentine Uwamariya, Waziri wa Jinsia na Uendelezaji wa Familia nchini Rwanda amesema taifa hilo linajivunia programu mahsusi za ujumuishaji wanawake kifedha ikiwemo uwekaji akiba, vikundi vya ushirika na mafunzo ya ujasiriamali, mambo ambayo yamewezesha ujumuishaji wanawake kifedha kufikia asilimia 92 takribani saw ana kiwango cha wanaume.

“Ongezeko la mwelekeo wa wanawake kujitegemea kifedha ni dhahiri kutokana na ongezeko la idadi yao wanaojihusisha na kukopa fedha benki na taasisi za utoaji za kifedha,” amesema Bi. Uwamariya.

Ameongeza kuwa kujitegema kifedha kunaimarishwa zaidi kupitia sheria za kuhakikisha wanawake wanamiliki ardhi na mali. Halikadhalika elimu ni kwa wote ni kipaumbele ambapo uandikishaji wasichana kwenye masomo ya Sayansi, Teknolojia, Uhandisi na Hisabati, STEM ni asilimia 46.2 ilhali Vyuo vya Ufundi Stadi na Elimu au TVET ni asilimia 43.2.

 “Juhudi za sasa ni kutokomeza mila na desturi potofu hasa mfumo dume na kuimarisha ushiriki wa wanawake kwenye sekta za kiuchumi, kijamii na utawala. Tunaoanisha pia stadi za kiufundi za wanawake na fursa za ajira,” amesema Waziri huyo kutoka Rwanda.

UGANDA: Benki zimeanzisha Programu maalum kwa wanawake

Amongi Betty Ongom, Waziri wa Uganda anayehusika na Jinsia, Kazi na Maendeleo ya Jamii alitaja hatua kadhaa zilizochukuliwa ili kusongesha Usawa wa Kijinsia na Uwezeshaji Wanawake au GEWE.
“Kwa kuingia ubia na Benki na Taasisi za Fedha ili zianzishe huduma za kifedha mahsusi kwa wanawake: Benki na taasisi hizo zimeanzisha Programu Maalum kwa Wanawake Wafanyabiashara zenye lengo la kurahisisha wanawake kupata fedha na huduma za kifedha zinazokidhi mahitaji yao.”

Ametaja benki hizo kuwa ni pamoja na BRAC Uganda Bank Limited, Stanbic Bank/Stanbic for Her na Centenary Bank na mradi wao wa Super Woman.

Halikidhalika Uganda imejengea uwezo wa stadi wanawake wajasiriamali ili waongeze thamani kwenye bidhaa zao hasa mazao ya kilimo.

ZIMBABWE: Tumeanzisha hadi Benki za Vijana na Wanawake

Kutoka Zimbabwe, Waziri wa Masuala ya Wanawake, Jamii, MAendeleo ya Biashara ndogo na za Kati, Monica Mutsvangwa  ametanabaisha kuwa Zimbabwe imeendelea kujumuisha suala la jinsia inapokuwa inaunda, inaendeleza, inatekeleza, inafuatilia na kutathmini sera, mikakati na mipango yote kuhusu masuala ya kiuchumi, kifedha na utokomezaji umaskini.

Mathalani utekelezaji wa mpanog wa kwanza na wa sasa wa Mkakati wa Kitaifa wa Ujumuishi wa Kifedha, kwa kiasi kikubwa umeimarisha ujumuishi wa wanawake na fursa za kupata fedha, kama inavyodhihirishwa na huduma ambazo zimeanzishwa kwa ajili ya wanawake, vijana na makundi mengine yaliyo hatarin,” amesema Waziri huyo.

Ametaja  huduma hizo kuwa ni pamoja na kuanzishwa kwa dawati la wanawake na vitengo karibu katika Benki zote, kuanzishwa kwa Benki ya Wanawake Zimbabwe ya kutoa mikopo, Benki ya Uwezeshaji Vijana na Mfuko wa Maendeleo ya Wanawake. Ingawa hivyo amesema licha ya mafanikio wanatambua kuwa bado safari ni ndefu kuelekea kuimarisha taasisi, utoaji wa fedha unaozingatia jinsia na kutokomeza umaskini miongoni mwa wanawake na wasichana.

Waziri wa Kenya wa Jinsia, Utamaduni, Sanaa na Urithi Aisha Jumwa Katana akihutubia kikao cha mawaziri katika moja ya vikao vya mkutano wa 68 wa Kamisheni ya Hali ya Wanawake duniani, CSW68 kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani
Video ya UN
Waziri wa Kenya wa Jinsia, Utamaduni, Sanaa na Urithi Aisha Jumwa Katana akihutubia kikao cha mawaziri katika moja ya vikao vya mkutano wa 68 wa Kamisheni ya Hali ya Wanawake duniani, CSW68 kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani

KENYA: Wanawake wanatumia majukwaa ya kidijitali kusajili makundi na kukopa fedha

Taifa hili la Afrika Mashariki liliwakilishwa na Waziri wake wa Jinsia, Utamaduni, Sanaa na Urithi Aisha Jumwa Katana ambaye amesema serikali ina sera na mikakati ya kiuchumi na kijamii inayohamasisha kusaka fedha na kufanikisha ujumuishaji wanawake kwenye sekta ya fedha.

Miongoni mwao ni Sera ya Taifa kuhusu Jinsia na Maendeleo ya mwaka 2019 na rasimu ya será ya Taifa kuhus umalezo na uwezeshaji wanawake kiuchumi, ambazo amesema msingi wao ni Katiba ambayo inasongesha usawa wa ijnsia na uwezeshaji wanawake na wakati huo huo kuhakikisha kuna usawa na hakuna ubaguzi.

Ametolea mfano wa hatua za kusongesha usawa wa jinsia na uwezeshaji wanawake kuwa ni Mfuko wa Wanawake wa Ujasiriamali , WEF, ambao amesema umeshatoa jumla ya dola milioni 6.72 kwa makundi 18,955 na kupata kukusanya dola 313,967.16 kama akiba.

“Kenya pia imetumia vizuri mbinu za kidijitali kuziba pengo la kidijitali kwenye jinsia kwa kuchagiza mfumo bora jumuishi wa kifedha. Mipango mahsusi juu ya matumizi ya dijitali imewekwa na kuwezesha wanawake wanaotaka kukopa fedha kusajili vikundi vyao, kupata mikopo na kukusanya akiba kupitia majukwaa ya kidijitali. Wanawake, vijana na watu wenye ulemavu wametengewa asilimia 30 ya zabuni za serikali,”  amesema Bi. Juma.

AFRIKA KUSINI: COVID-19 ilitumbukiza wanawake kwenye umaskini, tumechukua hatua

Kutoka Afrika Kusini, Lindiwe Zulu Waziri wa Maendeleo ya Jamii alieleza kuwa janga la COVID-19 lilifichua ukosefu wa usawa, umaskini utokanao na ukosefu wa ajira na njaa kwenye kaya, ambavyo vilichochea ongezeko la mzigo wa kazi zisizo na ujira na majukumu ya kazi za nyumbani kwa wanawake na wasichana na hatari wanazokumbana  nazo kutokana na ukatili wa kijinsia.

Akaelezea ni nini ambacho serikali ya taifa hilo lililofanya uchaguzi wa kwanza wa kidemokrasia mwaka 1994 imefanya akisema, “ilichukua hatua haraka kwa kupanua wigo wa hifadhi ya jamii, malipo maalum kwa wanawake wanaopatiwa msaada wa malezi ya watoto ili wakabiliane na kukosekana kipato kutokana na COVID-19, ongezeko la umaskini na ukosefu wa uhakika wa chakula. Serikali pia ilipitisha kanuni ya malipo maalum ya kuleta unafuu kwa watu wasio na ajira, hatua ambayo bado inatekelezwa.”

Lindiwe Zulu Waziri wa Maendeleo ya Jamii Afrika Kusini akizungumza katika Mkutano wa 68 wa Kamisheni ya kwenye kumbi mbalimbali za makao makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani.
UN News
Lindiwe Zulu Waziri wa Maendeleo ya Jamii Afrika Kusini akizungumza katika Mkutano wa 68 wa Kamisheni ya kwenye kumbi mbalimbali za makao makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani.