Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Vita ya Gaza yaweza kuchochea machafuko zaidi ya kikanda: UN

Wanaume wakitembea katika eneo lilosambaratishwa vibaya katikati ya Gaza. (Maktaba)
UN News/Ziad Taleb
Wanaume wakitembea katika eneo lilosambaratishwa vibaya katikati ya Gaza. (Maktaba)

Vita ya Gaza yaweza kuchochea machafuko zaidi ya kikanda: UN

Amani na Usalama

Mazungumzo ya kusitisha mapigano Gaza yanaendelea nchini Misri kwa siku ya pili leo huku Kamishina Mkuu wa Haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa akionya kwamba vita ya Gaza iko katika hatari ya kubadili mweleko na kupanua wigo zaidi utakaoathiri kila nchi Mashariki ya Kati na kwingineko.

Mazungumzo ya kusitisha mapigano Gaza yanaendelea nchini Misri kwa siku ya pili leo huku Kamishina Mkuu wa Haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa akionya kwamba vita ya Gaza iko katika hatari ya kubadili mweleko na kupanua wigo zaidi utakaoathiri kila nchi Mashariki ya Kati na kwingineko. Flora Nducha amefuatilia taarifa hiyo na anatujuza zaidi

Kamishina Mkuu Volker Türk ameliambia Baraza la Haki za Kibinadamu la Umoja wa Mataifa mjini Geneva Uswisi kuwa "Nina wasiwasi mkubwa kwamba katika janga hili la vita cheche yoyote zaidi inaweza kusababisha moto mkubwa zaidi," 

Hofu ya vita kusambaa

Katika taarifa ya hivi karibuni kuhusu migogoro ya kimataifa kwa Nchi 47 Wanachama wa Baraza hilo, Kamishna Mkuu alisisitiza kwamba jumuiya ya kimataifa inapaswa kufanya "kila linalowezekana ili kuepuka kuenea zaidi kwa vita ya Gaza.”

Maoni yake yanakuja huku kukiwa na wito wa "kusitishwa mara moja kwa mapigano kwa angalau wiki sita zijazo ili kuwezesha kuachiliwa huru kwa mateka wa Israeli.’

Wito huo umetoka kwa Makamu wa Rais wa Merika Kamala Harris, wakati wa mazungumzo ya kimataifa ya kusitisha mapigano nchini Misri Jumapili, ambayo yanayoripotiwa kuhusisha Marekani wajumbe wa Qatar na Hamas lakini hadi sasa hakuna wawakilishi wa Israel.

Hatari nchini Lebanon

Bwana Türk amesema “Hatari za kuyumbisha usalama wa kikanda tayari zilionekana kusini mwa Lebanon, akisisitiza kwamba wapiganaji wa wanamgambo wanaoiunga mkono Palestina sasa wanahusika katika hali ya kusikitisha sana ya uhasama na majibizano ya risasi na Israeli, katika msitali wa Bluu wa uangalizi wa Umoja wa Mataifa unaotenganisha nchi zote mbili.

Takriban watu 200 wameuawa nchini Lebanon tangu vita ilipozuka Gaza¸ Kamishna Mkuu amesema miongoni mwa waathirika wakubwa ni, watoto, wahudumu wa afya na waandishi wa habari.

Mkuu huyo wa haki za binadamu ameongeza kuwa “takriban watu 90,000 nchini Lebanon wamekimbia makazi yao kutokana na ghasia hizo, huku kukiwa na uharibifu mkubwa wa vituo vya afya, shule na miundombinu muhimu. Jamii za Israeli pia zimeshuhudia watu 80,000 wakiondolewa kutoka maeneo ya mpakani kwa sababu ya kuongezeka kwa vurugu.”

Ongezeko la vifo

Mashirika ya kibinadamu yameendelea kuripoti kuhusu hali mbayá na ongezeko la vifo vya raia ambapo lile la kuhudumia watoto UNICEF mwishoni mwa wiki likisema hadi sasa watoto 15 wamepoteza Maisha katika hospitali ya Kamal Adwan mjini Gaza kutokana na utapiamlo na ukosefu wa maji mwilini.

UNICEF imeonya kwamba watoto wengi zaidi watapoteza Maisha katika siku zijazo endapo msaada wa haraka unaohitajika hautofikishwa kunusuru Maisha yao.

Nalo shirika la Umoja wa Mataifa linalohusika na masuala ya wanawake UN Women linakadiria kuwa wanawake 9,000 wameshauawa tangu vita ilipozuka Gaza miezi mitano iliyopita. 

Mamlaka ya afya ya Gaza inasema jumla ya watu waliopoteza Maisha tangu kuanza kwa vita Gaza ni zaidi ya 30,400 na inatarajiwa kuendelea kuongezeka.