Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Vurugu za sasa DRC ni ishara ya onyo - Mshauri Maalumu wa UN kuhusu kuzuia mauaji ya kimbari 

Nyiranzaba na watoto wake tisa wanapata hifadhi kwenye hema baada ya kukimbia kijiji chake katika eneo la Rutshuru, jimbo la Kivu Kaskazini, DR Congo.
© UNICEF/Arlette Bashizi
Nyiranzaba na watoto wake tisa wanapata hifadhi kwenye hema baada ya kukimbia kijiji chake katika eneo la Rutshuru, jimbo la Kivu Kaskazini, DR Congo.

Vurugu za sasa DRC ni ishara ya onyo - Mshauri Maalumu wa UN kuhusu kuzuia mauaji ya kimbari 

Ukuaji wa Kiuchumi

Kufuatia ziara yake rasmi katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kuanzia tarehe 10-13 Novemba 2022, Mshauri Maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu kuzuia mauaji ya kimbari, Alice Wairimu Nderitu amesikitishwa sana na kuongezeka kwa ghasia katika Ukanda wa Maziwa Makuu ambako Mauaji ya Kimbari yam waka 1994 dhidi ya Watutsi nchini Rwanda yalitokea. 

Kupitia taarifa iliyosambazwa Jioni ya Jumatano hii ya tarehe 30 Novemba 2022, kwa saa za New York, Marekani ambako taarifa hii imetolewa, Bi. Nderitu amenukuliwa akisema, "vurugu za sasa ni ishara ya onyo la udhaifu wa jamii na uthibitisho wa uwepo wa kudumu wa hali ambayo iliruhusu chuki kubwa na vurugu kuzuka hadi mauaji ya kimbari hapo awali." 

Ziara yake imefuatia ujumbe wa ngazi ya kiufundi wa Ofisi yake ambao ulibaini kuwa viashiria na vichochezi vilivyomo katika Mfumo wa Umoja wa Mataifa wa Uchambuzi wa Uhalifu wa Kikatili vilikuwepo DRC vikiwemo; usambazaji wa matamshi ya chuki na kutokuwepo kwa mifumo huru ya kushughulikia suala hilo; siasa ya ubaguzi; kuongezeka kwa wanamgambo wa ndani na vikundi vingine vyenye silaha kote nchini; mashambulizi yaliyoenea na ya kuratibiwa, ikiwa ni pamoja na ukatili wa kijinsia, dhidi ya hasa Banyamulenge kwa misingi ya makabila yao na utii kwa nchi jirani; na mivutano ya vikundi. 

Mshauri Maalum pia ana wasiwasi mkubwa kuhusu vurugu za kijamii zinazoendelea Magharibi mwa DRC kati ya jamii za kabila la Suku, Mbala, Yansi, Songe, Luba, Kongo, Yaka na Teke. Watu kadhaa wamejeruhiwa na kuuawa, nyumba nyingi kuporwa na kuchomwa moto na Jeshi la Serikali, FARDC limeshambuliwa. 

Mashariki mwa DRC, ghasia za sasa zinatokana na janga la wakimbizi uliosababisha watu wengi waliohusika katika mauaji ya kimbari ya mwaka 1994 dhidi ya Watutsi nchini Rwanda kukimbilia Mashariki mwa DRC, na kuunda vikundi vyenye silaha kama vile Democratic Forces for the Liberation of Rwanda/Forces démocratiques de libération du Rwanda (FDLR) ambayo bado inafanya kazi Mashariki mwa DRC, Amesema Bi. Nderitu.  

“Katika kukabiliana na uwepo wa kundi hili lenye silaha, vikundi vipya vilivyo na silaha vilianzishwa na kushindwa kuwaleta wapiganaji wenye silaha wasio wa serikali kujiandikisha ndio matokeo tunayoona sasa.” Mshauri huyo ameongeza.   

Aidha amebainisha kuwa kutafuta suluhu kwa mzozo unaoendelea Mashariki mwa DRC kutahitaji kushughulikia sababu za msingi za ghasia na kujifunza kutoka kwa siku za nyuma. "Unyanyasaji unaotokea kwa sasa Mashariki mwa DRC, ikiwa ni pamoja na kuwalenga raia kwa misingi ya makabila yao au kudhaniwa kuwa wana uhusiano na pande zinazopigana lazima kukomeshwa. Ahadi yetu ya pamoja ya kutosahau ukatili uliopita ni wajibu wa kuzuia kutokea tena.” Amesisitiza.  

Akirejelea taarifa yake ya Juni 17, 2022 aliyoitoa kwa pamoja na Kamishna Mkuu wa Haki za Kibinadamu wakati huo Michele Bachelet, Mshauri Maalum Wairimu Nderitu ameonesha wasiwasi wake kuhusu athari kwa raia kutokana na ongezeko la hivi karibuni la uhasama kati ya kundi la M23 na Wanajeshi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo / Forces armées de la république démocratique du Congo (FARDC). 

Taarifa hiyo pia imeelezea wasiwasi wake kuhusu kuongezeka kwa maneno ya chuki na uchochezi wa ubaguzi, uhasama na ghasia nchini kote - na haswa dhidi ya Wanyarwanda wanaozungumza Kinyarwanda. Taarifa zimeonesha kwamba maneno ya chuki yameenezwa na viongozi wa vyama vya siasa, viongozi wa jamii, watendaji wa mashirika ya kiraia, na wananchi wa DRC waishio nje ya nchi.  

Mshauri huyo Maalum amesisitiza tena kwamba ingawa jukumu la msingi la kuzuia uhalifu wa kikatili ni la DRC kama Taifa, pande zote zinazohusika na mzozo huo mkali lazima zifanye kazi kwa haraka ili kupata suluhu  ya kisiasa ambayo italeta amani ya kina na endelevu kwa DRC kwa kushughulikia sababu ya msingi ya migawanyiko na vurugu, na wasiwasi halali wa wahusika wote. 

Mshauri huyo Maalum pia ameunga mkono wito wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres wa tarehe 30 Oktoba 2022 wa kukomesha mara moja uhasama ili kuhakikisha ulinzi wa raia na kuheshimiwa kwa sheria za kimataifa za kibinadamu. Aidha, amepongeza juhudi zinazoendelea kufanywa na Umoja wa Afrika na Jumuiya za Afrika Mashariki katika kurejesha hali ya kuaminiana na kuweka mazingira ya mazungumzo na mashauriano ya kisiasa kushughulikia mzozo wa usalama.