Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Umewadia wakati wa kuirejesha amani asema Guterres vita ikiingia mwaka wa 3 Ukraine

Katibu Mkuu wa UN António Guterres akihutubia Baraza la Usalama kujadili masuala ya amani na usalama Ukraine
UN Photo/Loey Felipe
Katibu Mkuu wa UN António Guterres akihutubia Baraza la Usalama kujadili masuala ya amani na usalama Ukraine

Umewadia wakati wa kuirejesha amani asema Guterres vita ikiingia mwaka wa 3 Ukraine

Amani na Usalama

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa leo amehutubia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na kusisitiza haja ya msingi ya kuheshimu mamlaka, uhuru, umoja na uadilifu wa eneo la Ukraine, wakati uvamizi kamili wa Urusi katika nchi hiyo unaadhimisha mwaka wake wa pili.

António Guterres amesema "Miaka miwili ya vita kamili na muongo mmoja tangu Urusi ilipojaribu kunyakua Jamhuri inayojiendesha ya Ukraine ya Crimea na mji wa Sevastopol, vita ya Ukraine inasalia kuwa kidonda kibichi katikati mwa Ulaya”.

Amesisitiza kuwa "Ni wakati muafaka wa amani, amani ya haki, kulingana na katiba ya Umoja wa Mataifa, sheria za kimataifa na maazimio ya Baraza Kuu." 

Akiwahutubia wajumbe wa Baraza la Usalama, pamoja na Mawaziri na mabalozi kadhaa waliohudhuria, Katibu Mkuu amewakumbusha kuhusu kanuni ya Umoja wa Mataifa ya haki ya kujitawala kwa wanachama wake wote.

Amesema kwa mujibu wa katiba ya Umoja wa Mataifa, migogoro ya kimataifa itasuluhishwa kwa njia za amani, na kwamba Mataifa yote yataepuka vitisho au matumizi ya nguvu dhidi ya uadilifu wa eneo au uhuru wa kisiasa wa nchi nyingine yoyote.

Baraza la Usalama likijadini amani na usalama kuhusu Ukraine
UN Photo/Loey Felipe
Baraza la Usalama likijadini amani na usalama kuhusu Ukraine

Katika vita yoyote, kila mtu anateseka

Bwana Guterres ameelezea mateso kwa raia wa pande zote mbili za vita.

Nchini Ukraine, raia wasiopungua 10,500 wamekufa na wengine zaidi wamejeruhiwa, shule, hospitali na miundombinu muhimu ya kiraia imeharibiwa, na maji na umeme katika miji na vijiji vimekatiwa wakati wa majira ya baridi kali.

Takriban watu milioni nne wamefurushwa kutoka kwa makazi yao, na familia nyingi, haswa kwenye mstari wa mbele, zinategemea msaada kuweza kuishi.

"Wananchi wengi wa Ukraine wanapitia majinamizi ya kupoteza watoto wao. Watoto wote ambao wametawanywa lazima waunganishwe na familia zao," amesema Bwana. Guterres.

Ameongeza kuwa "Vita pia inaumiza watu wa Urusi. Maelfu ya Warusi vijana wanakufa kwenye mstari wa mbele. Raia waliokumbwa na makombora katika miji ya Urusi pia wanateseka".

Hali ya maisha ya watu katika eneo la migogoro Mashariki mwa Ukraine. Picha hii ilipigwa kabla ya vita ya uvamizi wa sasa wa Urusi.
© UNHCR/Anastasia Vlasova
Hali ya maisha ya watu katika eneo la migogoro Mashariki mwa Ukraine. Picha hii ilipigwa kabla ya vita ya uvamizi wa sasa wa Urusi.

Hatari ya kuongezeka machafuko ni dhahiri

Katibu Mkuu pia ameonyesha wasiwasi mkubwa juu ya hatari iliyo wazi ya mzozo kuongezeka na kupanuka.

Amesema "Duniani kote, vita inazidisha migawanyiko ya kijiografia. Kuchagiza ukosefu wa utulivu wa kikanda. Na kupunguza nafasi iliyopo ya kushughulikia masuala mengine ya dharura ya kimataifa,”.

Akihitimisha hotuba yake, Guterres amesema tangu Urusi ilipovamia kikamilifu Ukraine, "tumekuwa na miaka miwili ya mapigano, miaka miwili ya mateso, miaka miwili ya kuzua mivutano ya kimataifa na kuzorotesha uhusiano wa kimataifa."

"Inatosha," amesisitiza, akibainisha kuwa kudharau katiba ya Umoja wa Mataifa imekuwa tatizo, na kuheshimu ni suluhisho.

Ameendelea kusema kuwa "Hiyo ina maanisha kuheshimu mamlaka, uhuru, umoja na uadilifu wa eneo la Ukraine, ndani ya mipaka yake inayotambulika kimataifa. Ni wakati wa kuzingatia upya katiba ya umoja wa Mataifa na kurejesha heshima kwa sheria za kimataifa. Hiyo ndiyo njia ya amani na usalama nchini Ukraine na duniani kote."