Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Itachukua miongo kadhaa na kiwango kikubwa cha fedha kurejesha uchumi wa Gaza

Msimu wa baridi na Mvua nyingi imefanya makazi huko Gaza kutokuwa na watu.
© UNRWA
Msimu wa baridi na Mvua nyingi imefanya makazi huko Gaza kutokuwa na watu.

Itachukua miongo kadhaa na kiwango kikubwa cha fedha kurejesha uchumi wa Gaza

Ukuaji wa Kiuchumi

Vita huko Gaza, Mashariki ya Kati imesababisha kiwango kikubwa cha kutwama kwa uchumi ambao  utahitaji mabilioni ya dola na mionog kadhaa kuurejesha katika hali iliyokuwa kabla ya kuanza kwa vita hiyo Oktoba 7 mwaka jana wa 2023.

Tathmini hiyo ya uchumi Gaza imo kwenye ripoti iliyotolewa leo na chombo cha Umoja wa Mataifa kinachohusika na biashara na maendeleo, au UNCTAD.

Ripoti hiyo yenye tathmini ya awali kuhusu madhara ya vita kwenye uchumi na jamii, inachunguza kupotea kwa Pato la Ndani la Taifa au GDP, muda wa kurejea kwa hali ya zamani na athari zake kwenye umaskini na matumizi ya kila kaya.

Inakadiriwa kuwa GPD ya Gaza imepungua kwa dola milioni 655 mwaka jana saw ana asilimia 24.

"Iwapo itaweza kujikwamua na kurejea kwenye hali yake ya kiuchumi, basi mapigano ya kijeshi lazima yakome sasa, na ujenzi mpya uanze kwa kina hivi sasa bila kuchelewa. Jamii ya kimataifa inahitaij kuchukua hatua sasa kabla hali haijawa mbaya,” imependekeza ripoti hiyo.

Kasi ya kuporomoka kwa uchumi ni kubwa

Gaza imekuwa imezingirwa tangu mwaka 2007, baada ya wanamgambo wa kipalestina, Hamas waingie madarakani, na imekuwa na kiwango cha wastani cha ukuaji cha asilimia 0.4 hadi mwaka 2022.

UNCTAD inakadiria kuwa uchumi huo tayari umesinyaa kwa asilimia 4.5 katika robo ya kwanza yam waka 2023.

 “Hata hivyo, operesheni za kijeshi zimesababisha kuongeza kasi ya kuporomoka kwa uchumi na GDP nayo imepungua. Na kwa mwaka mzima Pato la kila mwaka la mwananchi limepungua kwa asilimia 26.1,” imesema ripoti hiyo.

Ripoti imebaini kuwa iwapo mapigano yangalikoma sasa, na ujenzi mpya uanze mara moja, na kiwango cha ukuaji uchumi cha kuanzia 2007 hadi 2022 kiendelee, itachukua hadi mwaka 2092 kurejesha kiwango cha pato la ndani la Gaza la mwaka 2022, huku Pato la ndani la kila mtu na mazingira ya kiuchumi na kijamii yakiporomoka.

Mazingira magumu ya kiuchumi na kijamii

Mazingira tayari yalikuwa magumu kwenye Ukanda wa Gaza, moja ya maeneo yenye watu wengin kupindukia duniani, eneo lenye zaidi ya wapalestina milioni mbili wakiishi kwenye eneo la ukubwa wa kilometa 365 za mraba saw ana maili 141 za mraba.

Idadi kubwa ya watu hao, sawa na asilimia 80, wanategemea misaada ya kimataifa: theluthi mbili ni hohehahe, na kiwango cha ukosefu wa ajira ni asilimia 45 kabla ya kuanza kwa vita.

"Kufungua fursa za kiuchumi na ustawi Gaza ni pamoja na kurejesha huduma kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Gaza ambao sasa haufanyi kazi," - UNCTAD 

Watu wengi hawana huduma za msingi kama vile maji safi, umeme na mifumo sahiji ya majitaka. Halikadhalika, maeneo mengi yaliyokuwa yameharibiwa na Israel kabla ya vita ya sasa, bado hayajarekebishwa.

Kurejesha mazingira ya kiuchumi na kijamii kabla ya vita ya sasa kutahitaij miongo kadhaa na usaidizi wa kigeni, imesema UNCTAD, ikitanabaisha kuwa operesheni za kijeshi zinazoendelea sasa zimefurusha asilimia 85 ya wakazi wa Gaza. Shughuli za kiuchumi zimesimama, umaskini na ukosefu wa ajira umeongezeka.

Leo hii, takribani asilimia 80 ya nguvukazi haiko kwenye ajira, ilhali majengo 37,379 buildings —sawa na asilimia 18 ya jumla ya majengo yote Gaza, yameharibiwa au yamesambaratishwa kabisa.

“Ukanda wa Gaza, nusu ya wanaoishi humu ni watoto na sasa eneo hilo halikaliki, watu hawana chanzo cha kujipatia kipato, maji, huduma za kujisafi, afya na elimu,” imesema UNCTAD.

Kitongoji cha Tal Al-Sultan ni eneo lililofurika watu wengi zaidi kwenye Ukanda wa Gaza wakati huu ambapo mapigano yanaendelea.
UN News/Ziad Taleb
Kitongoji cha Tal Al-Sultan ni eneo lililofurika watu wengi zaidi kwenye Ukanda wa Gaza wakati huu ambapo mapigano yanaendelea.

Shughuli za kiuchumi zirejeshwe ikiwemo Uwanja wa ndege wa kimataifa Gaza

Kamati hiyo  ya Umoja wa Mataifa kuhusu Biashara na Maendeleo imeonya kuwa awamu mpya ya ujenzi mpya wa uchumi Gaza haiwezi kumaanisha kurejea katika hali ilivyokuwa kabla ya vita na  bali pia mzunguko wa uharibifu na ujenzi usio endelevu lazima usiendelee.

Ikidadavua hali ya uchumi wa Gaza na mikakati ya kukwamua eneo hilo, ripoti inasema kuwa “vikwazo vya uchumi Gaza, vimejikita katika miaka 56 ya kukaliwa na miaka 17 ya vizuizi, hivyo inaonesha ulazima wa kuelewa kwa kina na mikakati ya uhalisia ya kufungua uwezo wake wa kustawi kupitia mikakati kama vile kurejesha uwanja wa kimataifa wa Gaza, (ambao leo hii haufanyi kazi) kujenga bandari na kuwezesha serikali ya PAlestina kuendeleza machimbo ya nishati ya gesi pwani ya bahari ya Mediteranea ili mapato yasaidie ujenzi mpya wa miundombinu.”

Ripoti inasisitiza umuhimu wa kusaidia haraka juhudi za serikali ya Palestina za kuzuia uchumi kutwama zaidi, huku ikitambua kuwa misaada ya kigeni imepungua kutoka jumla yad ola bilioni 2 au asilimia 27 ya pato la ndani la taifa mwaka 2008 hadi dola milioni 550 mwaka 2022 sawa na chini ya asilimia 3 ya pato la ndani la Palestina.

Hlikadhalika UNCTAD inasisitiza kwamba suluhu ya janga Gaza inahitaji kumaliza operesheni za kijeshi na kuondoa vizuizi na hatua hizo ndio msingi wa kuelekea kufanikisha jawabu la mataifa mawili: Israel na Palestina yakiwa pamoja.