Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Miradi ya FAO na WFP yaboresha maisha ya wananchi Syria

Mashamba darasa ya kilimo na ufugaji nchini Syria yanayoendeshwa na shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo, FAO, yanaimarisha shughuli za ufugaji miongoni mwa wanawake nchini Syria.
©FAO/Andrea Thiodour
Mashamba darasa ya kilimo na ufugaji nchini Syria yanayoendeshwa na shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo, FAO, yanaimarisha shughuli za ufugaji miongoni mwa wanawake nchini Syria.

Miradi ya FAO na WFP yaboresha maisha ya wananchi Syria

Ukuaji wa Kiuchumi

Mashirika ya Umoja wa Mataifa lile la Chakula na Kilimo FAO na la Mpango wa chakula duniani WFP yanasaidia kuinua maisha ya wananchi katika nchi ya Syria kwa kuwapatia miradi mbali mbali ikiwemo ya ufugaji wa kondoo.

Mashariki mwa Syria katika mji wa Deir Ezzor ulioko umbali wa km 450 kutoka mji mkuu wa nchi hiyo Damascus, mashirika ya UN lile la FAO na WFP yanafanya kila juhudi kuwajengea uwezo na kubadili maisha ya wananchi kupitia miradi mbalimbali.

Katika Kijiji cha Al Masrab FAO ilianzisha mafunzo ya mashamba ya wakulima, na wanakijiji wakapewa mafunzo mbalimbali ikiwemo ya ufugaji wa kondoo kwa faida. Bi. Wafaa Al Sydyan anasema mara baada ya kuhitimu mafunzo hayo WFP ikampa mtaji wa zizi la kondoo.

Bi. Al Saydan anasema, "chanzo changu kikuu cha mapato kinatokana na ufugaji kondoo, na kipato changu kiliongezeka baada ya kupata uzoefu kutoka kwenye mafunzo mbalimbali ambayo yaliniwezesha mimi na familia yangu kumudu gharama za maisha. Nauza maziwa katika kituo cha ushindikaji cha hapa kijijini kwetu Al Masrab.”

Video ya WFP inamuonesha Bi. Baraa Nadal mnufaika wa WFP akiwa na wanawake wenzake wanne katika kituo cha usindikaji maziwa, wakichemsha maziwa na kisha kuchakata mazao yatokanayo na maziwa katika mashine maalum ili kujipatia mazao mbalimbali na anasema si haba biashara inaenda vyema. 

Yeye anasema, “tunauza baadhi ya mazao hapa kijijini kwetu na baadhi tunauza katika soko la Shmatieh. Tunamshukuru Mungu, mapato yetu yamekuwa bora kwa sababu ya kitengo cha usindikaji tulichowezeshwa na WFP.”

Miradi hii ya WFP na FAO imepata ufadhili kutoka kwa wadau mbalimbali ikiwemo Muungano wa Ulaya, (EU), Wizara ya Mambo ya Nje ya Norway na Idara ya Maendeleo ya serikali ya Italia.