Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mashirika ya UN yaomba kufunguliwe njia nyingine ya kufikisha misaada Gaza

Malori yaliyosheheni msaada wa kibinadamu yakijiandaa kuingia Gaza kupitia kivuko cha Rafah
© UNICEF/Eyad El Baba
Malori yaliyosheheni msaada wa kibinadamu yakijiandaa kuingia Gaza kupitia kivuko cha Rafah

Mashirika ya UN yaomba kufunguliwe njia nyingine ya kufikisha misaada Gaza

Msaada wa Kibinadamu

Zikiwa ni zaidi ya siku 100 tangu kuibuka upya kwa mzozo huko Mashariki ya Kati, mashirika ya Umoja wa Mataifa hii leo yametoa taarifa inayoelezea kuongezeka kwa hatari ya baa la njaa na milipuko ya magonjwa ya kuambukiza huku yakisisitiza muarobaini pekee kwa sasa ni kuruhusu njia mpya za kuingiza misaada ya kwenda kutatua changamoto zinazowakabili wananchi walioko Gaza. 

Hii leo kutoka Geneva Uswisi na New York Marekani Mashariki manne ya UN ambayo  ni lile la Mpango wa chakula duniani WFP, Afya ulimwenguni WHO, linalohusika na masuala ya watoto UNICEF na  la kuhudumia wakimbizi wa kipalestina UNRWA wametoa taarifa ya pamoja inayoeleza zahma zinazowakumba wakazi wa Gaza na nini kifanyike kuwasaidia. 

WFP, ambao tangu tarehe 7 wamekuwa wakitoa Msaada wa chakula na kuweza kuwafikia zaidi ya wananchi 900,000 mpaka sasa, wanaeleza kuwa wananchi wengi wanakabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula ambapo watu wazima wanapitisha hata siku nzima bila kula chochote ili angalau watoto waweze kuweka chochote tumboni. 

“Wananchi wa Gaza wapo hatarini kufa njaa wakati maili chache tu toka walipu kuna msururu wa malori yaliyojaa chakula” amesema Mkurugenzi Mkuu wa WFP Cindy McCaini ambaye pia ametoa suluhu akisema “Kila saa inayopotea tunaweka maisha mengi hatarini. Tunaweza kuzuia njaa lakini ikiwa tu tunaweza kutoa vifaa vya kutosha na pia kufikisha misaada hiyo kwa njia zilizo salama ili kula mwenye uhitaji popote alipo afikiwe.”

UNICEF, Mkurugenzi Mkuu wake anasema Bi. Catherine Russell anasema watoto huko Gaza mbali na kiwewe cha milipuko na kutakiwa kuhama huku kisha kule na kujeruhiwa na kuuawa wengi wanakabiliwa na utapiamlo mkali na wengine wana uzito mdogo ikilinganishwa na urefu wao. 

“Watoto walio katika hatari kubwa ya kufa kutokana na utapiamlo na magonjwa wanahitaji sana matibabu, maji safi na huduma za usafi wa mazingira, lakini hali haituruhusu kuwafikia watoto na familia zao, baadhi ya misaada inayohitaji sana kuwasaidia imezuiliwa kuingia Gaza. Maisha ya watoto na familia zao yananing'inia kwenye mizani.”

Mkurugenzi wa WHO Dkt.Tedros Adhanom Ghebreyesus anasema mbali na kutoa misaada ya vifaa tiba na kusaidia sekta ya afya iliyohemewa na wingi wa wagonjwa lakini wamelazimika kufungua majiko mawili katika hospital maana watu wanaumwa na wana njaa. 

“Watu huko Gaza wanateseka kutokana na ukosefu wa chakula, maji, dawa na ukosefu wa  huduma za afya za kutosha. Njaa itafanya hali mbaya ambayo ipo tayari kuwa janga kwa sababu wagonjwa wana uwezekano mkubwa wa kufa na njaa na watu wenye njaa wana hatari zaidi ya magonjwa. Tunahitaji ufikishaji misaada usiozuiliwa, salama wa kutoa misaada na usitishaji mapigano kwa sababu za kibinadamu ili kuzuia vifo na mateso zaidi.”

Mkuu wa UNRWA Phillip Lazzarini amehitimisha taarifa hiyo ya pamoja kwa kusema misaada inayoingia Gaza ni tone la maji katika baharí ya misaada inayohitajika , ombi ni kuwa Israel iruhusu bandari ya Ashdod ambayo ipo umbali wa Km 40 tu kutoka Gaza kaskazini itumike kupitisha misaada ili waweze kuwafikia wananchi wengi wenye uhitaji.