Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Baada ya miaka 10 Mali, MINUSMA ‘yafunga rasmi pazia’

Walina amani wa Umoja wa Mataifa kutoka Chad hapa wakiwa wamewasili Gao kutamatisha uwemo wa MINUSMA huko Kidal kaskazini mwa Mali
MINUSMA
Walina amani wa Umoja wa Mataifa kutoka Chad hapa wakiwa wamewasili Gao kutamatisha uwemo wa MINUSMA huko Kidal kaskazini mwa Mali

Baada ya miaka 10 Mali, MINUSMA ‘yafunga rasmi pazia’

Amani na Usalama

Hii leo Desemba 31 mwaka 2023, ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kuweka utulivu nchini Mali, MINUSMA umekamilisha operesheni ya kuondoka nchini humo kwa mujibu wa azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa namba 2690 la mwaka huu wa 2023.

MINUSMA ilianza jukumu lake nchini Mali, Julai 1, mwaka 2013 kufuatia azimio la Baraza la Usalamaa namba 2100 la tarehe 25 Aprili mwaka 2013.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema kupitia taarifa iliyotolewa Jumamosi jijini New York, Marekani kwamba anatambua dhima muhimu ya MINUSMA kwenye kulinda raia, kusaidia mchakato wa amani na kuhakikisha uzingatiwaji wa sitisho la mapigano kwa mujibu wa Mkataba wa Amani na Maridhiano wa mwaka 2015.

Halikadhalika ujumbe huo ulisaidia pia kwenye kipindi cha mpito, kurejesha mamlaka ya serikali na kuona amani inakuwa na manufaa kwa wananchi.

“Ameelezea shukrani zake za dhati kwa wafanyakazi wa MINUSMA akiwemo Mkuu wa ujumbe na Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu El-Ghassim Wane ambaye ameonesha uongozi wa kipekee katika mazingira yenye changamoto,” imesema taarifa hiyo.

Kuondoka kulighubikwa na changamoto lukuki

Ujumbe wa MINUSMA ulikuwa ukishambuliwa mara kwa mara. Pichani kikosi kutoka Guinea kikiwa kimeweka lindo eneo la vilimani mjini Kidal.
UN /Sylvain Liechti
Ujumbe wa MINUSMA ulikuwa ukishambuliwa mara kwa mara. Pichani kikosi kutoka Guinea kikiwa kimeweka lindo eneo la vilimani mjini Kidal.

Kwa namna ya kipekee ameshukuru ari, azma na huduma kutoka kwa nchi zilizochangia askari na polisi kwenye mazingira magumu nchini Mali, ikiwemo wakati wa kupunguza askari na kuondoka kwa ujumbe huo.

Operesheni za kuondoka nchini humo zilikuwa zinakumbwa na changamoto lukuki ikiwemo misafara ya walinda amani kushambuliwa njiani na kusababisha vifo na majeruhi.

Ametuma rambirambi kwa watendaji 311 wa MINUSMA waliopoteza maisha yao katika kipindi chote cha MINUSMA, na zaidi ya 700 waliojeruhiwa wakiwa kwenye harakati za ujenzi wa amani kwa miaka yote 10 ya ujumbe huo.

“Katibu Mkuu na Umoja wa Mataifa kwa ujumla uko na majonzi na mshikamano na familia zao, marafiki na wafanyakazi wa waliopoteza maisha, wakati huu tunasalia tumehamasishwa na kujitoa kwao na kutokuwa na ubinafsi katika kusaka amani,” imesema taarifa hiyo ikimnukuu Katibu Mkuu.

Usafirishaji wa mali zilizosalia

Kuanzia Januari 1, 2024 ndipo kitaanza kipindi cha kufunga masalia ya majukumu ambapo timu ya watu wachache itakayokuwa inaripoti Idara ya  Umoja wa Mataifa ya Usaidizi wa Operesheni, sambamba na nchi zinazochangia askari na polisi watakuweko Gao na Bamako.

Jukumu lao ni kusimamia usafirishaji wa mali za nchi zinazochangia askari na polisi na kuondokana pia na mali za Umoja wa Mataifa.

“Katibu Mkuu anatarajia ushirikiano wa hali ya juu kutoka serikali ya mpito mali ili kuhakikisha mchakaot huu unakamilika haraka iwezekanavyo.”

Japo MINUSMA imefunga virago, mfumo mzima wa Umoja wa Mataifa yakiwemo mashirika yake 21 na Ofisi ya UN nchini Mali, na ile ya Umoja wa Mataifa Afrika Magharibi, wataendelea na kuweko Mali kusaidia taifa hilo kufanikisha Ajenda 2030 ya malengo ya maendeleo endelevu, SDGs na Programu ya ushirikiano kati ya UN na Mali ya 2020-2024.