Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mashambulizi ya ndege za Urusi zisizo na rubani dhidi ya Ukraine yakemewa vikali

Mji wa Dnipro mashariki mwa Ukraine umekumbwa na mashambulizi mapya ya makombora.
© Proliska
Mji wa Dnipro mashariki mwa Ukraine umekumbwa na mashambulizi mapya ya makombora.

Mashambulizi ya ndege za Urusi zisizo na rubani dhidi ya Ukraine yakemewa vikali

Amani na Usalama

Maafisa kadhaa wa ngazi za juu wa Umoja wa Mataifa, akiwemo Katibu Mkuu Antonio Guterres, Ijumaa kwa saa za Marekani wamelaani vikali shambulio kubwa la makombora lililotekelezwa usiku na ndege zisizo na rubani katika miji kadhaa ya Ukraine, ikiwa ni pamoja na kushambulia miundombinu ya kiraia.

Shambulio hilo limeripotiwa kusababisha vifo vya takriban raia 24 na wengine zaidi ya 134 kujeruhiwa, amesema Stéphane Dujarric, Msemaji wa Katibu Mkuu. 

Kwa mujibu wa ripoti za vyombo vya habari, mamlaka ya Ukraine imesema kuwa karibu makombora 110 yalirushwa dhidi ya Ukraine siku ya Ijumaa na kulenga mji mkuu wa Kyiv, pamoja na vituo vya wakazi vya Kharkiv, Lviv, Zapporizhia na Odessa.

Ukiukaji wa sheria za kibinadamu

"Mashambulizi dhidi ya raia na miundombinu ya kiraia yanakiuka sheria za kimataifa za kibinadamu, hayakubaliki na lazima yakome mara moja," Bwana Dujarric amesema, na kuongeza kuwa Katibu Mkuu ametoa "rambirambi zake za kina kwa familia za waathirika wote" na kuwatakia ahueni ya haraka. waliojeruhiwa.

Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa, Volker Türk, amesema "ameshtushwa" na mfululizo huu mpya wa mashambulizi makubwa ya makombora na ndege zisizo na rubani zilizoratibiwa na Urusi kote Ukraine usiku wa Desemba 28 hadi 29.

Amebainisha kwamba shambulio hilo limepiga "miundombinu mbalimbali ya raia, ikiwa ni pamoja na majengo ya ghorofa, wodi ya wazazi, shule, shule za chekechea, bustani, kituo cha treni na kituo cha manunuzi, pamoja na miundombinu ya nishati." Umeme ulikatwa katika maeneo kadhaa kufuatia uharibifu wa njia za kusambaza umeme, alisema.

"Sheria ya kimataifa ya kibinadamu inakataza kwa uwazi mashambulizi yanayolenga kimakusudi miundombinu ya kiraia, pamoja na mashambulizi ya kiholela, katika hali zote. Kwa mara nyingine tena natoa wito kwa Shirikisho la Urusi kusitisha mara moja mashambulizi yake dhidi ya Ukraine na kuheshimu kikamilifu sheria zote za sheria za kimataifa zinazohusiana na uhasama,” mkuu huyo wa haki za binadamu alisema.

Njia ya uharibifu na kifo

Mratibu wa Misaada ya Kibinadamu wa Ukraine Denise Brown awali amelaani wimbi la mashambulizi katika miji ya Ukraine.

"Ninalaani, kwa maneno makali iwezekanavyo, wimbi la kutisha la mashambulizi yaliyoanzishwa na Urusi dhidi ya maeneo yenye wakazi wa Ukraine katika saa zilizopita, ambayo yameacha njia ya uharibifu, vifo na mateso ya binadamu," amesema katika taarifa yake kwa vyombo vya habari.

"Kwa watu wa Ukraine, huu ni mfano mwingine usiokubalika wa ukweli wa kutisha wanaokabiliana nao na ambao umefanya mwaka 2023 kuwa mwaka mwingine wa mateso makubwa," ameshutumu. "Shirikisho la Urusi linaendelea kupuuza majukumu yake chini ya sheria ya kimataifa ya kibinadamu. Mashambulio ya kiholela au mashambulizi yanayoelekezwa kimakusudi dhidi ya raia au vitu vya kiraia yamepigwa marufuku kabisa."

Mkutano wa Baraza la Usalama

Baraza la Usalama limekutana leo Novemba 29 kwa dharura ili kutathmini hali ya Ukraine.

Wajumbe kumi na watano wa Baraza hilo wamesikiliza maelezo kutoka kwa Khaled Khiari, Msaidizi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika Idara za Masuala ya Kisiasa na Ujenzi wa Amani na Operesheni za Amani.

"Waukraine kwa mara nyingine wanalazimika kutumia mapumziko kutafuta makazi, kusafisha vifusi na kuwazika wafu katika hali ya hewa ya baridi," Hiyari amelieleza baraza.

Khaled Khiari, Msaidizi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika Idara za Masuala ya Kisiasa na Ujenzi wa Amani na Operesheni za Amani akihutubia Baraza la Usalama.
UN Photo/Eskinder Debebe

Amesisitiza kuwa shambulizi dhidi ya Ukraine usiku wa kuamkia leo lilikuwa la hivi karibuni zaidi katika msururu wa mashambulizi yanayoongezeka ya Urusi. Kulingana na takwimu za hivi karibuni, takriban raia 30 wameuawa na takribani 160 wamejeruhiwa. Miundombinu ya kiraia, pamoja na shule na hospitali, imeharibiwa.

"Mashambulizi haya yalikuwa mojawapo ya mashambulizi makubwa zaidi ya anga tangu uvamizi kamili wa Urusi Februari 2022, ulioanzishwa kinyume na Mkataba wa Umoja wa Mataifa na sheria za kimataifa," Hiyari amesisitiza.