Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

WFP yasikitishwa na wizi wa chakula katika ghala Gezira, Sudan

Ghala za WFP katika bandari ya Sudan zinahifadhi bidhaa za chakula kwa ajili ya usambazaji wa dharura.
© WFP/Mohamed Elamin
Ghala za WFP katika bandari ya Sudan zinahifadhi bidhaa za chakula kwa ajili ya usambazaji wa dharura.

WFP yasikitishwa na wizi wa chakula katika ghala Gezira, Sudan

Msaada wa Kibinadamu

Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) limelaani vikali uporaji wa chakula cha kuokoa maisha kutoka katika majengo yake kwenye Jimbo la Gezira nchini Sudan mwishoni mwa wiki iliyopita baada ya baadhi ya wanajeshi waasi wanaounda kikosi cha RSF kuvunja ghala na ofisi, baada ya kulitwaa eneo la Wad Medani. 


 

Taarifa ya WFP iliyotolewa leo Novemba 28 huko Port Suda - Sudan na Nairobi – Kenya imeeleza kuwa ghala hilo lilikuwa na akiba ya kutosha kulisha karibu watu milioni 1.5 wasio na uhakika wa chakula kwa mwezi mmoja katika Jimbo la Gezira, ambapo shambulio jipya limelazimisha zaidi ya watu 300,000 kukimbia tena kuokoa maisha yao. 

"Watu wa Sudan ambao tayari wamekata tamaa na kukimbia mapigano sasa msaada wao muhimu wanaohitaji umeibwa. Hili halivumiliki na lazima likomeshwe,” amesema Michael Dunford, Mkurugenzi wa WFP wa Kanda ya Afrika Mashariki. "Katika maeneo yaliyo chini ya udhibiti wao, Vikosi vya RSF lazima vihakikishe ulinzi wa usaidizi wa kibinadamu, wafanyakazi na majengo". 

Ghala la WFP lilikuwa na zaidi ya tani 2,500 za chakula cha kuokoa maisha, ikiwa ni pamoja na kunde, mtama, mafuta ya mboga na virutubisho vya lishe. Vyakula hivyo maalumu vya lishe vilikusudiwa kuzuia na kusaidia matibabu ya utapiamlo kwa zaidi ya watoto 20,000 na wanawake wajawazito na wanaonyonyesha kupitia vituo vya afya vinavyoungwa mkono na WFP. 

WFP ililazimika kusitisha usambazaji wa chakula kwa muda katika jimbo la Gezira wikendi iliyopita. Kwa mara nyingine tena inapanga upya kufanya shughuli zake za kibinadamu na imeanza usambazaji katika majimbo zaidi ya Mashariki, ambapo watu wanaokimbia Gezira sasa wanatafuta hifadhi. 

“Operesheni za WFP ni suluhu kwa karibu watu milioni moja waliokata tamaa katika jimbo la Gezira na uporaji wa majengo unadhoofisha shughuli zetu wakati ambapo karibu watu milioni 18 wanakabiliwa na njaa kali.” Anasema Michael Dunford. 

WFP imesaidia zaidi ya watu milioni 5.6 katika majimbo kumi na saba kati ya kumi na nane kote Sudan kwa usaidizi wa chakula na lishe tangu mzozo huo ulipozuka katikati ya mwezi Aprili 2023. Shirika hilo lilionya mapema mwezi huu juu ya janga la njaa linalokaribia ikiwa watu hawataweza kupokea misaada.