Habari kwa ufupi: Gaza, Sudan, Mifumo ya chakula
Habari kwa ufupi: Gaza, Sudan, Mifumo ya chakula
Leo Umoja wa Mataifa umeonya kwamba Gaza ni mahali hatari zaidi kuishi kwa watoto. Akizungumza na waandishi wa habari mjini Geneva Uswis msemaji wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF, James Elder amesema “Siku baada ya siku ukatili wa hali ya juu unadhihirika. Katika saa 48 zilizopita hospitali kubwa Zaidi iliyobaki inafanyakazi imeshambuliwa mara mbili. Hospitali hiyo ya Al Nasser iliyopo Khan Yunis sio tu kwamba inahifadhi idadi kubwa ya Watoto ambao tayari wamejeruhiwa vibaya katika mashambulizi majumbani kwao lakini pia inahifadhi mamia ya wanawake na Watoto wanaosaka usalama.”
Nalo shirika la Umoja wa Mataifa la msaada kwa wakimbizi wa Kipalestina UNRWA limesema zaidi ya asilimia 60 ya mioundombinu Gaza imesambaratishwa kabisa na zaidi ya asilimia 90 ya watu wametawanywa .
Wimbi kubwa la watu wakimbia mizozo Sudan
Nchini Sudan shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR leo limesema linatiwa wasiwasi kubwa na kiwango cha janga la watu wanaoendelea kulazimika kutawanywa ndani ya Sudan na katika nchi Jirani. Shirika hilo limesema mamia kwa maelfu ya watu wamefurushwa makwao katika mapigano mapya kwenye jimbo la katikati mwa Sudan la Al Jazirah lililoko Kusini Mashariki mwa mji mkuu, Khartoum.
Mifumo ya Chakula
Na ripoti mpya "Hali ya mifumo ya chakula duniani kote katika kuelekea mwaka 2030", iliyochapishwa leo na mradi wa shirika la chakula na kilimo la Umoja wa Mataifa FAO unaoangia mifumo hiyo kuelekea ukomo wa malengo ya maendeleo endelevu ifikapo mwaka 2030 (FSCI), inatoa tathimini ya kwanza ya ufuatiliaji wa kisayansi ili kuwaongoza watoa maamuzi wanapotaka kufanya mabadiliko ya jumla ya kilimo cha kimataifa na mifumo ya chakula.
FAO inasema mabadiliko haya yanahitajika haraka ili kupunguza athari za mazingira za mifumo hii ya chakula na za mabadiliko ya tabianchi. Lengo kuu ni kwamba watu wote haswa walio hatarini zaidi wapate fursa sawa ya lishe bora kupitia kilimo endelevu na chenye mnepo na mifumo bora ya chakula.