Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Uganda: Wanaume na wavulana washika hatamu kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake- Bwana Masereka

Mhudumu wa afya nchini Uganda, Timothy Mbene Masereka
UNFPA
Mhudumu wa afya nchini Uganda, Timothy Mbene Masereka

Uganda: Wanaume na wavulana washika hatamu kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake- Bwana Masereka

Wanawake
  • Alisaidia watu wenye Malaria lakini ukatili wa kijinsia 'akakwaa kigingi'
  • Mafunzo ya UNFPA kupitia Spotlight Initiative yakamjengea uwezo
  • Sasa yeye na familia yake na jamii wanaishi kwa kutumia falsafa ya usawa wa kijinsia

Kupitia kazi yake ya mjumbe katika kikundi cha afya kwenye kijiji chao kilichoko wilaya ya Kasese nchini Uganda, Timothy Mbene Masereka amebobea katika kutibu magonjwa ya malaria na vichomi au Pneumonia miongoni mwa wale wanaoambukizwa magonjwa hayo kijijini mwao.

Hata hivyo ubobezi huo ulikwaa ‘kigingi’ wakati akijaribu kukabiliana na changamoto moja kubwa aliyoshuhudia wakati akipita nyumba kwa nyumba kuitikia wito wa kaya; Ukatili dhidi ya wanawake na wasichana.

“Wakati wa kutoa huduma kwenye kaya za wanakijiji, nilibaini kuwa ukatili wa kijinsia ulikuwa ni tatizo na hivyo nikajaribu kutatua – lakini nilikosa stadi za kufanya hivyo,” Bwana Masereka amesema hayo akizungumza na UNFPA  ambalo ni shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya watu na Afya ya uzazi.

Mfumo dume Uganda haukupatia nafasi usawa wa kijinsia

“Katika jamii yangu, mfumo dume umeshamiri na hivyo ukatili wa kijinsia ni jambo ambalo halikujadiliwa kwa uwazi.”

Duniani kote, mada y ukatili wa kijinsia  inasalia kuwa mada ya aibu, ukimya na unyanyapaa, licha ya kuwa moja ya ukiukwaji mkubwa zaidi wa kibinadamu ulioshamiri maeneo mbali mbali duniani.

Ushirikishaji wa wanaume wachuuzi katika kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na watoto wa kike nchini Uganda.
UN Women/Eva Sibanda
Ushirikishaji wa wanaume wachuuzi katika kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na watoto wa kike nchini Uganda.

Kwa mujibu wa shirika la Umoja wa Mataifa la afya duniani, WHO, takribani mwanamke 1 kati ya 3 amekabiliwa na ukatili kutoka kwa mwenza wake, au ukatili wa kijinsia kutoka kwa mtu asiye mpenzi wake, au vyote viwili angalau mara moja katika maisha yake.

Hali ya ukatili dhidi ya wanawake nchini Uganda

Wakati huo huo, nchini Uganda, mwaka 2021 asilimia 95 ya wanawake na wasichana waliripotiwa kukumbwa na ukatili wa vipigo, kingono au vyote tangu wakiwa na umri wa miaka 15.

Bwana Masereka alikuwa anasaka mbinu ya kukabili unyanysaji huu kwenye jamii yake. Na katik safari yke hiyo y kuwa mchechemuzi wa wanawake na wasichana, alijifunza kuwa ingawa ukatili unaanzishwa na wanaume, vile vile unaweza kumalizwa na hao hao wanaume.

“Idadi kubwa ya watekelezaj iwa ukatili wa kijinsia ni wanawame,” anasema Bwana Masereka. Hata hivyo wanaume na wavulana wanaweza kuwa sehemu ya majawabu.”

Kubadili mwelekeo na kusaidia manusura

Ukatili wa kijinsia unachochewa na fikra potofu na maadili yanayoshamirisha ukosefu wa usawa wa kijinsia. Kubadili imani na tamaduni za jamii ni kazi ngumu – lakini ni kazi muhimu ili kukomesha mzunguko huu. 

Hiyo ni moja ya mambo ambayo Bwana Masereka alihamasika sana kufuatilia na kubeba jukumu hilo. Mwaka 2019 alipatiwa fursa ya kushiriki mafunzo juu ya kutatua ukatili wa kijinsia kupiti mpango wa Spotlight au Spotlight Initiative,  huu ni mpngo wa Umoja wa Mataifa wa kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na watoto wa kike.

Hapa alijifunza jinsi ya kuzungumza na wanaume na wavulana kuhusu ukatili wa kijinsia, jinsi ya kushauri wanandoa kutatua tofauti zao kwa njia ya mazungumzo na jinsi ya kubaini na kuelekeza kwenye mamlaka na usaidizi wanawake na wasichana wanaokabiliwa na ukatili wa kijinsia.

Kuna ukatili wa kiuchumi dhidi ya wanawake

Alijifunza pia jinsi ya kubaini aina zilizofichika za ukatili wa kijinsia, ikiwemo ukatili wa kiuchumi. “Kwa mfano, wanawake wanapanda mazao, lakini hawapatiwi fursa ya kuzungumza kuhusu mazao hayo. Wanaume ndio walifanya maamuzi yote.”

Bwana Masereka ni miongoni mwa zaidi ya wanaume 1,500 nchini Uganda ambao wamepatiwa mafunzo kupitia Mpango wa Spotlght na kuwa mfano wa wanaume wenye dhima chanya tangu mwaka 2019.

Mafunzo yanapatia wanaume hao fursa ya kujifunza mikakati ya kubadili mitazamo na tamaduni ambazo zinaweza kusababisha ghasia, na kusaidia manusura ili waweze kufikia huduma.

Majukumu ya Bwana Masereka wilayani Kasese

Katika wilaya ya Kasese, Bwana Masereka anahusika na kuongeza uelewa kuhusu ukatili wa kijinsia kwa kusambaza taarifa makanisani, mikusanyiko ya kijamii, kufanya ziara ya majumbani kusaidia wanandoa kumaliza tofauti zao kwa amani na kisha kuwezesha wanaume na wavulana kujadili hoja ya ukatili wa kijinsia.

Halikadhalika anafuatilia wasichana wanaoacha masomo shuleni na kufanya kazi kusaidia manusura wa ukatili wa kijinsia – ikiwemo kuwasindikiza polisi na ofisi za kata kutoa ripoti kuhusu visanga vilivyowafika.

“Wanaume na wavulana, wanaweza kutumia uwezo wao kubdili jamii iwe bora zaidi,” anasema mchechemuzi huyo.

Mabadiliko yanaanzia nyumbani

Katika miaka ya hivi karibuni, Uganda imekuwa na mafanikio makubwa katika kutokomeza fikra na imani potofu zinazoshamirisha ukosefu wa usawa wa kijinsia.

Mathalani kati ya mwaka 2000 na 2016, kiwango cha wanaume waliokubali kipengele kimoja au zaidi cha kuhalalisha ukatili wa kipigo dhidi ya mwenzi wake ilipungua kutoka asilimia 64 hadi asilimia 41.

Ingawa hivyo, bado kuna wengine wamekuwa wagumu kubadili fikra zao. Wengine hata wamediriki kuendesha mashtaka nyumbani kwa Bwana Masereka hadi pale alipopata mafunzo.

Mke wangu akichanga kuni, mimi nateka maji

“Nimejifunza kuwa kazi za nyumbani zinaweza kufanywa na wote wanaume na wanawake,” anasema Masereka. “Kwa kufanya hivyo, mambo yanakwenda haraka. Mfano, iwapo mke wangu anaandaa mlo, mimi ninaweza kusafisha vyombo. Iwapo mke wangu anachanja kuni, naweza kuteka maji. Kwa njia hii tunakula mapema.”

Watu walicheka mara ya kwanza walipomuona Bwana Masereka akifanya kazi za nyumbani. Lakini mitazamo yao ilibadilika pindi walipoona ni kwa vipi nyumba yake imekuwa na ufanisi.

Uhusiano ndani ya familia umekuwa bora; Bwana Masereka anasema uhusiano wake na mkewe na watoto sasa umeimarika.

“Najisikia furaha kwa sababu hivi sasa watoto wanaweza kunieleza chochote,” anasema akiongeza kuwa, “mke wangu hanifichi chochote – amekuwa dhahiri na muwazi kama mimi nilivyo kwake.”

Spotlight Initiative

Huu ni mpango wa Umoja wa Mataifa ukitekelezwa na Muungano wa Ulaya na wadau wengine kwa lengo la kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na wasichana. Nchini Uganda unatekelezwa na serikali, Muungano wa Ulaya, mashrika ya Umoja wa Mataifa ambayo ni UN Women, UNFPA, UNICEF, UNDP, UNHCR.

Kwa msaada kutoka Ofisi ya Kamisha Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu haki za binadamu, OHCHR, IOM, Pulse Lab na wengineo.

Tangu mwaka 2019, takribani watu 300,000 nchini Uganda wameshiriki programu za kijamii kuhusu haki za wanawake kupitia mpango huu.

Makala hii ni sehemu ya machapisho katika kuadhimisha siku ya kimataifa ya kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake, tarehe 25 mwezi Novemba, ambayo huashiria kuanza kwa siku 16 za harakati za kutokomeza ukatili huo, na kufikia kilele tarehe 10 Desemba ambayo ni siku ya Haki za Binadamu duniani.