Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Simulizi: Sijawahi kuona vita kama hii, hii ni Nakba kwa Wapalestina

Mashambulio ya makombora yamesababisha uharibifu mkubwa huko Gaza.
WHO
Mashambulio ya makombora yamesababisha uharibifu mkubwa huko Gaza.

Simulizi: Sijawahi kuona vita kama hii, hii ni Nakba kwa Wapalestina

Amani na Usalama

Watu wa Gaza wanakabiliwa na “mshtuko mkubwa” kutokana na mzozo unaoendelea baina yao na Israel, kwa mujibu wa mfanyakazi wa Umoja wa Mataifa anayefanya kazi katika eneo hilo.

Adnan Abu Hasna, msemaji wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi wa Kipalestina UNRWA alikuwa akizungumza wakati wanajeshi wa Israel wakiendelea kushambulia Gaza, huku wakiwazuia Wapalestina wengi kuondoka.

“Nilishuhudia vita nyingi hapo awali huko Gaza, lakini sijawahi kuona ukubwa wa janga kama hili hapo awali. Ni Nakba (janga) mpya kwa Wapalestina. Sikutarajia au kufikiria kuona mamia ya maelfu ya watu walioyakimbia makazi yao kuelekea kusini; wameacha kila kitu nyuma.”

Msemaji wa UNRWA Adnan Abu Hasna. (Maktaba)
Ziad Taleb
Msemaji wa UNRWA Adnan Abu Hasna. (Maktaba)

Katika maisha yangu yote sijawahi kuona vitongoji vyote vimefutiliwa mbali katika jiji la Gaza. Niliona watu, wakazi wa asili wa mji wa Gaza ambao hawakuwa wameondoka Gaza kwa maelfu ya miaka lakini leo wamekuwa wakimbizi na kuhamia eneo jipya.

Kila mtu yuko katika mshtuko mkali. Wanahisi ni ndoto mbaya. Watu wengine hawaamini kilichotokea. Leo nimekutana na mtu aliyekuja makao makuu yetu kuomba kusajiliwa katika kituo cha makazi katika shule ya UNRWA.

Alianza kuzungumza na kusema kwamba alipoteza watoto wake watano, mke wake na dada yake. Alikuwa akiongea katika hali ya kawaida, bado alikuwa hajui ukubwa wa msiba aliona nao, bado alikuwa katika hali ya mshtuko. Alisema anatafuta mahali pa kukaa kwa sababu hakuwa na fedha wala chochote. Akaniambia alikuja na nguo zake tu.

Alipojitambulisha, nilijua kwamba alikuwa anatoka katika familia moja ya watu matajiri huko Gaza ambayo ilikuwa na biashara, na sasa hakuwa na kitu chochote.

Amepoteza familia yake, amepoteza kazi yake, amepoteza kila kitu, na sasa anatafuta mahali pa kwenda ambako anahisi salama, ili tuweze kumpa maji na chakula ambacho hawezi kujipatia.

Wapalestina wanaendelea kukimbia kutoka sehemu hatari zaidi za Ukanda wa Gaza.
© UNRWA/Ashraf Amra
Wapalestina wanaendelea kukimbia kutoka sehemu hatari zaidi za Ukanda wa Gaza.

Hili ndilo tatizo kuu ambalo mamia ya maelfu ya Wapalestina wanakabiliana nalo, pamoja na ukosefu wa hisia za usalama. Ukiwa katika shule za UNRWA, na unapandisha bendera ya bluu (ya Umoja wa Mataifa), hujisikii salama, mtaani hujisikii salama, kwenye magari hujisikii salama. Hakuna mahali salama na kuna chakula kidogo na maji.

Ninaona mamia ya watoto wakiomba maji au chakula; watu wana njaa na kiu. Sijawahi kushuhudia hali hii hapa Gaza. Watu wamejaa sana, wanagombana, wanapiga kelele.

Mbele ya mashine za kuchuja maji ya chumvi, ambayo bado inafanya kazi, unaweza kuona maelfu ya watu wakisubiri maji ya kunywa. Kwa kweli, watu wamepoteza kila kitu, hawana fedha, walikuja tu na nguo zao. Hawana chochote. Hata hawakujitayarisha kwa majira ya baridi. Ni mtanziko mkubwa.

Na hali ni vivyo hivyo ukiwa mwanajamii au ukiwa unafanya kazi UNRWA. Nasi tumeyakimbia makazi yetu na tunapata hifadhi katika makazi ya wakimbizi. Hii ni hisia ambayo mimi na wenzangu wengine hatujawahi kuihisi hapo awali hapa Gaza.

Wakati mwingine mimi husimama na kufikiria, ninazungumza nini? Je, ninazungumzia mateso ya pamoja? Au mateso ya mtu binafsi? Kila mwanadamu ana hadithi, hadithi ya kupoteza familia, fedha, mali, ardhi, na kila kitu.

Kwa mara nyingine tena, Wapalestina wamerudi kwenye sifuri. Swali kuu wanalouliza kila wakati ni: Unayaonaje mambo haya, nini kinaweza kutokea? "Hakuna anayeweza kujibu kwa uaminifu."