Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Nawapenda dada zangu na siwezi kuwaacha nyuma kamwe - Simulizi ya Armen

Armen Gakani, Mkimbizi kkutoka DRC ambaye sasa anahifadhi katika  kambi ya Kalobeyei iliyoko kaunti ya Turkana nchini Kenya.
WFP Kenya
Armen Gakani, Mkimbizi kkutoka DRC ambaye sasa anahifadhi katika kambi ya Kalobeyei iliyoko kaunti ya Turkana nchini Kenya.

Nawapenda dada zangu na siwezi kuwaacha nyuma kamwe - Simulizi ya Armen

Wahamiaji na Wakimbizi

Migogoro ya miongo na miongo nchini Jamhuri ya kidemocrasia ya Congo, DRC imefurusha watu wengi kutoka makazi yao, wengine kubaki wakimbizi wa ndani na wengine kukimbilia nchi jirani. Kenya ni mojawapo wa nchi ambazo zinawahifadhi wakimbizi hao na katika Kaunti ya Turkana, tunakutana na Armen Gakani, msichana mwenye umri wa miaka 23.

Armen na familia yake walikimbia jimbo lao la Kivu Kusini kutokana na vita na yeye, akiwa na mama yake na wadogo wake wawili wenye ulemavu, wanaishi katika kambi ya wakimbizi ya Kalobeyei, anasema, “Niliondoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo mwaka wa 2017. Tuliondoka kwa sababu ya vita, kulikuwa na vita kali. Sababu nyingine ilikuwa kwamba wanamgambo walijaribu mara kadhaa kuwaua ndugu zetu wawili ambao wana ulemavu. Vitisho hivi vilitulazimisha kutafuta mahali salama, tukaishia hapa Kalobeyei.”

Armen Gakani  na ndugu zake, wakimbizi katika kambi ya Kalobeyei iliyoko kaunti ya Turkana nchini Kenya.
WFP/Kenya
Armen Gakani na ndugu zake, wakimbizi katika kambi ya Kalobeyei iliyoko kaunti ya Turkana nchini Kenya.

Kuwa na ulemavu ni changamoto kubwa hasa watu wakiwa ukimbizini. Na akiwa ndiye mtoto mkubwa kwa familia yake, na vilevile kwa sababu ya umri wa mama yake, Armen anawajibika kwa wadogo zake, wasichana wawili wenye ulemavu.

“Kama mkubwa katika familia hii, na kwa sababu mama yetu hawezi kufanya mengi kutokana na umri wake, ninatafuta kazi za hali ya chini ambazo zinaweza kutuletea pesa kidogo za kutunza familia, hasa watoto hao wadogo”

Na Armen angetamani yeye na ndugu zake wapate masomo ya elimu ya msingi lakini mambo bado ni magumu,

“Changamoto nyingine kwetu ni fursa duni ya mimi na ndugu zangu kusoma. Fursa ni ngumu kuzipata. Majukumu yangu hapa nyumbani ni kununua bidhaa za kujisafi na za lishe ya familia yangu, pia naogesha na kulea watoto hasa huyu wa umri wa miaka 10 ambaye hana uwezo wa kujisafi mwenyewe. Mimi peke yangu ndiye ninayeweza kumbeba kwani hawezi kusimama hivyo ninamuogesha, kumvisha na kumlisha.”

Armen Gakani, Mkimbizi kkutoka DRC ambaye sasa anahifadhi katika  kambi ya Kalobeyei iliyoko kaunti ya Turkana nchini Kenya.
WFP/Kenya
Armen Gakani, Mkimbizi kkutoka DRC ambaye sasa anahifadhi katika kambi ya Kalobeyei iliyoko kaunti ya Turkana nchini Kenya.

Kwa bahati mbaya, kazi zisizo na ujuzi pekee ndizo anaweza kupata, ilihali hazitoshi kukidhi mahitaji yao lakini ana matumaini kwa kuwa kaya yake ni moja ya wanufaika wa msaada wa Shirika La Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani, WFP.

“Kutoka WFP tunapata usaidizi wa chakula, tunapokea pesa taslimu kila mwezi. Tunajua wakati pesa imetolewa, kwa sababu tunaangalia salio kwa kutumia kadi ya benki. Kwa kadi, tunaenda kituoni, tunatoa pesa na kununua chakula. Tunapata Kshs 18,000 (Dola 120), kila mwezi ambazo tunazitumia kununua chakula cha kutuhudumia kwa mwezi mzima. Tunapopata fedha, tunapaswa kutanguliza tunachonunua kwa sababu bei ya vyakula imepanda. Tunatanguliza unga wa mahindi, maharage, mafuta, samaki waliokaushwa, mchele na unga wa ngano kwa kutengeneza mkate bapa”.

Kwa vile Armen anawapa ndugu zake upendo wa dada na vile vile wa mama, anamalizia kwa kusema, “Ndugu zangu hawa wote wawili ni walemavu na wana mahitaji maalum na mimi ndiye macho ambayo familia hii hutazama katika siku zijazo. Ninawapenda na siwezi kuwaacha nyuma kamwe”.

Shukrani sana kwa msaada wa WFP kwa kusaidia maelfu ya familia za wakimbizi kama ya Armen, ili waweze kujikimu kimaisha hususani kupata mahitaji ya msingi na lishe kwa jamii.