Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

HAITI: Hali ya usalama bado si shwari, kikosi cha kimataifa cha usalama ni tegemeo- Salvador

Moto unawaka barabarani katika eneo la Cité Soleil huko Port-au-Prince.
© UNOCHA/Giles Clarke
Moto unawaka barabarani katika eneo la Cité Soleil huko Port-au-Prince.

HAITI: Hali ya usalama bado si shwari, kikosi cha kimataifa cha usalama ni tegemeo- Salvador

Amani na Usalama
  • Magenge ya uhalifu yanazidi kutishia uhai wa raia 
  • Magenge hayo yamteka nyara mchana Katibu Mkuu wa Baraza la Taifa la Mpito 
  • Kikosi cha Kimataifa cha Usaidizi wa usalama ni nuru 
Tweet URL

Kwa bahati mbaya, hali ya usalama Haiti inaendelea kudorora kila uchao kwani magenge ya uhalifu yanazidi kusambaratisha maisha ya wananchi na vitendo vya uhalifu mkubwa vimevunja rekodi.  

Sehemu ya hotuba ya Mwakilishi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa MAtaifa nchini Haiti María Isabel Salvador kwa Baraza la Usalama lililokutana leo kupokea ripoti ya Katibu Mkuu kuhusu Suala la Haiti.  

Katibu Mkuu atekwa nyara  

Alipotaja vitendo vikubwa vya uhalifu alitolea mfano tukio la Jumatano iliyopita ambapo magenge ya  uhalifu yalimteka nyara Katibu Mkuu wa Baraza la Juu la Mpito nchini Haiti ‘mchana kweupe.’ Watu hao walikuwa wamevalia sare za jeshi la polisi Haiti.  

Vitendo ya mauaji, ukatili wa kingono ikiwemo ubakaji kwa makundi, ukataji watu viungo vinaendelea kutumiwa na magenge ya uhalifu kila uchao, amesema Bi. Salvador ambaye pia ni Mkuu wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa nchini Haiti, BINUH.  

Kati ya tarehe 24 mwezi Aprili na 30 Septemba mwaka huu, BINUH imesajili matukio 395 ya kuchomwa moto watu wanaodaiwa kuwa wafuasi wa magenge ya uhalifu kwenye mikoa yote 10 ya Haiti, na wamechomwa moto na kundi liitwalo “Bwa Kale” ambao ni sungusungu.  

Magereza nayo  yamefurika, akitolea mfano gereza la Les Cayes akisema hali ya mazingira humo ni duni kupindukia.  

Muarobaini wa magenge ya uhalifu  

Kutokana na ongezeko hilo la uhalifu, Mkuu huyo wa ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Haiti amepongeza hatua ya tarehe 2 mwezi huu wa Oktoba ya Baraza la Usalama ya kupitisha azimio 2699 lililoruhusu nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa kuunda Kikosi cha Kimataifa cha usaidizi wa usalama (MSS) na kwenda nchini Haiti kikiwa na majukumu pamoja na mambo mengine kujengea uwezo polisi wa kitaifa nchini humo.  

“Kikosi hicho kitajengea uwezo polisi wa Haiti kujenga tena mazingira bora kwa ajili ya uchaguzi,” amesema Bi. Salvador akiongeza kuwa kupelekwa kwa kikosi hicho cha kimataifa kunaleta matumaini kuwa hali ya usalama itaimarika.  

Polisi wa Kitaifa Haiti wanaweza kuwa na matokeo bora ya kudumu pale tu usalama wa umma utakaporejeshwa na serikali ianze kutekeleza majukumu yake, hasa kwenye maeneo dhalili yanayokumbwa na ghasia mara kwa mara.  

Kinachotakiwa sasa   

Ni kwa mantiki hiyo amesema ili taasisi za kitaifa ziweze kuwa na udhibiti mkubwa, juhudi lazima zielekezwe kwenye uratibu kati ya Polisi wa kitaifa wa Haiti na wadau waotoa msaada kupitia kikosi cha kimataifa cha usaidizi wa ulinzi (MSS) ili kuepusha urudiwaji wa hatua bila sababu ya msingi.  

Amesisitiza umuhimu wa kuelekeza rasilimali zinazohitajika kuwezesha kikosi hicho cha kimataifa kufanya kazi yake, halikadhalika Umoja wa Mataifa kuweza kutekeleza miradi na programu za kufanikisha uwepo wa kikosi hicho.  

Mathalani programu za masuala ya haki, uchaguzi na kusaidia polisi wa kitaiafa, miradi itakayotekelezwa kwa uratibu baina ya BINUH, MSS na Ofisi ya Umoja wa Mataifa Haiti.