Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Je akili mnemba AI ni faida au athari katika sekta ya filamu?: UNESCO

Idhaa ya Habari za ilizungumza na msanii wa taswira aliyeshinda tuzo Yvonne Muinde, ambaye alikuwa mmoja wa wazungumzaji walioshiriki mkutano wa UNESCO kuhusu Akili Mnemba..
UN News/Thelma Mwadzaya
Idhaa ya Habari za ilizungumza na msanii wa taswira aliyeshinda tuzo Yvonne Muinde, ambaye alikuwa mmoja wa wazungumzaji walioshiriki mkutano wa UNESCO kuhusu Akili Mnemba..

Je akili mnemba AI ni faida au athari katika sekta ya filamu?: UNESCO

Utamaduni na Elimu

Akili mnemba imebadili fani ya sanaa na utamaduni kwa njia ambazo ha ikutarajiwa. Hata hivyo mabadiliko hayo ni ya muda mrefu. 

Ili kuwapa jukwaa wataalam wa sanaa na masuala ya kidijitali, shirika la umoja wa mataifa la elimu, sayansi na utamaduni, UNESCO limeandaa mjadala maalum ili kujadili athari za akili mnemba kwenye sekta ya filamu. 

Ajenda inajikita kwenye manufaa na changamoto zitakazoikumba sekta za utamaduni na sanaa ukizingatia maadili na ubunifu. 

Yvonne Muinde ni msanii aliyebobea kwenye sekta ya ubunifu na dijitali na mshiriki wa mjadala huo wa UNESCO. 

Yvonne Muinde ni msanii aliyebobea katika kuchanganya picha za filamu na hapa ndipo kwenye ofisi na makaazi yake.

Safari yake ya sanaa ilianza na kuchora. Hiyo ndiyo njia yake ya kuwasiliana na umma hasa anapokutana na mada nzito zinazokirihi nafsi.

Yvonne aliamua kujiunga na sanaa ya ubunifu wa kidijitali baada ya kuchora kwa muda na kupata ujuzi mkubwa. Kwa mtazamo wake, kila binadamu ana kisa cha kusimulia, kwani,“ Napenda sana kuchora picha hasa za binadamu…. Upande wa pili wa shilingi ni simulizi yake. Kuelewa kinachoendelea duniani na yanayotusibu. Sina suluhu ila naweza kuchora ninachohisi.”

Yvonne Muinde akielezea picha alizochora kusimulia ulafi na ukatili katika jamii.
UN News/Thelma Mwadzaya
Yvonne Muinde akielezea picha alizochora kusimulia ulafi na ukatili katika jamii.

Akili mnemba na sekta ya filamu

Azma ya UNESCO katika majadiliano hayo ni kuwapa wadau wa sekta ya filamu na akili mnemba nafasi ya kuelewa mbinu hii mpya ya kidijitali ili kuwawezesha kutunga Sera mujarab kwa manufaa ya fani ya ubunifu.

Akili mnemba imeleta tishio kwa sekta ya ubunifu kwani Kasi ya wasanii na kifaa hicho kipya cha kidijitali haiambatani. 

Kwa Yvonne, alipotazama picha zilizotengezwa kwa akili mnemba kwanza alishtuka kisha akaingiwa na hofu.

Ni mfumo ulio na sura mbili.Unatosha ila pia upo nasi.Kwahiyo tutalazimika kuukubali, kuukumbatia na kuutumia kazini. Binafsi ni naona ni kitisho kwa msanii. Ninavyoielewa, sanaa ni kujieleza, kuweka bayana changamoto za maisha,kupata, kukosa, matatizo, mafanikio,… hisia zote hizi ambazo hazina fomula maalum. Akili mnemba inataka alfabeti na kubuni mbinu ya kufurahi. Wepesi wa akili mnemba wa kubuni picha katika muda mchache unanikanganya. Hata hivyo mfumo huo Upo nasi na itabidi tutafute njia ya kuutumia kazini.”

Filamu kidijitali

Sekta ya ubunifu iko mstari wa mbele katika masuala ya simulizi na teknolojia. Sanaa inatumika kuichagiza jamii ili kuleta mabadiliko. 

Mama Msanii na mbunifu, Yvonne anapenda kuchora na kujikita kwenye simulizi ya jamii kwani ndio njia mujarab ya kujieleza kwake.

Sekta ya filamu imegubikwa na wingu la wasiwasi ukizingatia matumizi ya akili mnemba na uwazi, hakimiliki na malipo ya kazi ya ubunifu kama anavyofafanua Yvonne Muinde, ambaye ni msanii wa filamu kuwa,“ Tatizo kubwa la mfumo huu ni wizi wa picha na kazi za wasanii.Kutumia bidhaa hizo bila kuwatambua wasanii… wanavuna maelezo na data kwa njia rahisi kwenye kompyuta. Hata hivyo tujilaumu kwani Sera zinatuangusha,taasisi husika zimelegea ilhali zinapaswa kutulinda. Kwa hiyo kuna masuali mengi ya maadili mintarafu akili mnemba japo inaweza kutumika kama kifaa.”

Baadhi ya picha za nyuso za viongozi wa ulimwengu wanaozua hisia mseto, kazi za sanaa za Yvonne Muinde.
UN News/Thelma Mwadzaya
Baadhi ya picha za nyuso za viongozi wa ulimwengu wanaozua hisia mseto, kazi za sanaa za Yvonne Muinde.

Mawasiliano na binadamu ni msingi wa sanaa

Kwa Yvonne, kila msanii anahitaji kuwa na uhusiano na mazingira na kufanya shughuli za kumtoa nje.

Kila anapokuwa nje ndipo Anaipa nafasi akili kufunguka na akaweza kupata mapya ya kusimulia kwenye Sanaa.

Mbali ya kuchanganya picha za filamu,Yvonne ni mpenzi wa mashindano ya mbio ,kuogelea na kuendesha basikeli.

Amekwea mlima Kenya, Kilimanjaro na azma yake ni kuipanda ile ya Ruwenzori.

Kwa Yvonne, Sanaa inaanzia mtaani ili kusimulia kila unachokiona ndipo teknolojia ya kisasa kama akili mnemba kuwa na nafasi yake,“ Mjadala huu sio wa sekta moja, ni wa kila mtu na wa jamii nzima. Mbinu iko sokoni tayari kwa hiyo tutayazungumza na kuwashirikisha wengi zaidi.

Yvonne Muinde anawashauri wasanii wanaoinukia kuwa wanyenyekevu na kutambua wakati wa kuuliza maswali na kukubali kuna baadhi wasivyovijua.

Anasisitiza kuwa upo umuhimu wa kutangamana na wakongwe wa fani ya sanaa na filamu kwa manufaa ya baadaye na kupata mawili matatu ya muhimu.

La msingi ni kukumbuka kuwa sanaa ni maisha na mawasiliano kwahiyo huwezi kuitenga na binadamu.

Yvonne anafahamika kwa kazi zake za filamu kidijitali zikiwemo za Avatar, Star Wars: Revenge of the Sith, Happy Feet na the new A-Team.

Amechora picha kadhaa maarufu kama vile Eyes of Monsters inayoonyesha macho ya viongozi wanaozua mitazamo mikali na nyengine nyingi.