Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Marekani yatumia kura ya turufu kupinga rasimu ya azimio la Gaza

Marekani yapiga kura ya turufu kupinga rasimu ya azimio liliongozwa na Brazil kuhusu Gaza
UN WebTV
Marekani yapiga kura ya turufu kupinga rasimu ya azimio liliongozwa na Brazil kuhusu Gaza

Marekani yatumia kura ya turufu kupinga rasimu ya azimio la Gaza

Amani na Usalama

Marekani leo imetumia kura ya turufu kupinga rasimu ya azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ambalo lingetaka "kusitishwa mapigano kwa ajili ya masuala ya kibinadamu" ili kuwasilisha misaada ya kuokoa maisha kwa mamilioni ya watu huko Gaza. 

Kushindwa kwa Baraza hilo kuingilia kati kwa mara ya kwanza hadharani katika mgogoro wa Israel na Gaza kulifuatia kukataliwa kwa rasimu iliyoungwa mkono na Urusi siku ya Jumatatu jioni.

Wakati wajumbe 12 kati ya 15 wa Baraza hilo wamepiga kura kuunga mkono azimio lililoongozwa na Brazil kwenye kikao kuhusu mzozo wa Mashariki ya Kati , mjumbe  mmoja  ambaye ni Marekani amepiga kura ya kuyapinga, na wawili ambao ni Urusi, na Uingereza hawakupiga kura.

Kura ya ‘hapana’ kutoka kwa yeyote kati ya wanachama watano wa kudumu wa Baraza la Usalama inasimamisha hatua yoyote iliyowekwa mbele ya baraza hilo. Wanachama wa kudumu wa Baraza la Usalama ni China, Ufaransa, Shirikisho la Urusi, Uingereza na Marekani.

Marekebisho ya Urusi

Kabla ya kura hiyo, marekebisho mawili yaliyopendekezwa na Urusi, yakitaka kusitishwa kwa mapigano mara moja, ambayo ni ya kudumu na kamili, na kusitisha mashambulizi dhidi ya raia na yalikataliwa na Baraza la Usalama.

Balozi wa Urusi Vassily Nebenzia alisema "Wakati wa mafumbo ya kidiplomasia umepita zamani. Yeyote ambaye hakuunga mkono rasimu ya azimio la Urusi kuhusu suala hili atawajibika kwa kile kinachotokea. 

Aliongeza kuwa rasimu ya sasa "haina wito bayana wa kusitishwa kwa mapigano" na haitasaidia kukomesha umwagaji damu".

Alisema marekebisho ya Urusi yalipendekeza mwito wa kukomesha mashambulizi ya kiholela dhidi ya raia na miundombinu huko Gaza, kulaaniwa kwa kitendo cha kuwekwa kizuizi kwenye eneo hilo na kuongeza hoja mpya ya wito wa kusitisha mapigano kwa ajili ya masuala ya kibinadamu.

"Ikiwa haya hayatajumuishwa katika rasimu ya sasa, haitasaidia kushughulikia hali ya kibinadamu huko Gaza na kuweka misimamo ya jumuiya ya kimataifa," alisema.

Mkutano wa pili wa hadhara

Mkutano wa leo umekuwa ni mkutano wa pili wa hadhara wa Baraza la Usalama kuhusu hali ya Gaza. 

Mabalozi wamekutana, haswa kwa faragha, juu ya changamoto hiyo, pamoja na mikutano ya tarehe 8 na 13 Oktoba.

Hatua hiyo ya rasimu ya azimio linaloongozwa na Brazil inafuatia kushindwa Jumatatu jioni kwa rasimu ya azimio lililoongozwa na Urusi ya kutaka kusitishwa kwa mapigano kwaajili ya masuala ya kibinadamu huko Gaza.

Azimio hilo lilipata kura tano za ndio  kutoka kwa China, Gabon, Msumbiji, Russia, na Falme za Kiarabu na nne za hapana kutoka kwa Ufaransa, Japan, Uingereza na Marekani, na wajumbe sita hawakupiga kura ambao ni Albania, Brazil, Ecuador, Ghana, Malta na Uswisi).