Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Sauti Kutoka Gaza: Wanawake wajawazito, wahudumu wa afya, wafanyakazi wa UNFPA

Familia ambazo zimekimbia makazi yao zimejenga makazi ya muda katika eneo la kusini mwa Gaza.
© UNRWA
Familia ambazo zimekimbia makazi yao zimejenga makazi ya muda katika eneo la kusini mwa Gaza.

Sauti Kutoka Gaza: Wanawake wajawazito, wahudumu wa afya, wafanyakazi wa UNFPA

Wanawake

Ushuhuda ufuatao kutoka kwa watu wa Gaza umekusanywa na wafanyakazi wa shirika la Umoja wa Mataifa la Idadi ya watu na fya ya uzazi, UNFPA katika wiki iliyopita, ambapo waandishi wa habari walishiriki katika mazungumzo hayo na ili kulinda utambulisho wa watoa ushuhuda, majina yao hayajajumuishwa.

 

Ushuhuda wa wanawake wajawazito

Mwanamke huyu mjamzito mwenye umri wa miaka 30, kutoka kaskazini mwa Gaza, amelazimika kuhama nymbani kwake mara nne, kila mara akiwa na begi ndogo la nguo. Anahofia usalama wa mtoto wake ambaye hajazaliwa na anaona kuwa haiwezekani kuishi katika mazingira yenye msongamano wa watu. Bila shaka, anaishi na familia yake katika shule moja inayohifadhi wakimbizi wa ndani baada ya nyumba yao kuharibiwa. Akipumzika kwenye sakafu yenye baridi, bila chakula cha kutosha au vifaa vya msingi vya kujisafi, ana wasiwasi juu ya mtoto wake, lakini anapohisi mtoto wake akipiga mateke tumboni mwake anasema, "Kila hatua ni kama mbio dhidi ya kifo, sikuweza kujizuia kutafakari na kufikiria jinsi ambavyo mtoto wangu alivyokuwa na nguvu. Sikujali ni wapi nitajifungulia, au jinsi nitakavyo jifungua mtoto wangu”.  

Ushuhuda wa muhudumu wa afya

Mama huyu alipoanza kuumwa, alienda katika wodi ya wazazi ya Al-Shifa. Watu waliojeruhiwa walikuwa wamelazwa kila pahali kwenye sakafu. Alipokelewa na akajifungua salama, lakini masaa matatu baadaye, ilibidi aruhusiwe kuondoka hospitalini ili kutoa nafasi kwa wajawazito wengine na majeruhi.

Mkurugenzi wa Hospitali ya Al Shifa  ambachi ni kituo kikubwa zaidi cha matibabu huko Gaza anasema, “hospitali yetu kwa sasa inafanyakazi kupita uwezo wake. Madaktari wamelemewa ingawa wamekuwa wakifanya kazi kwa bidii mchana na usiku tangu kuanza kwa vita dhidi ya Israeli na Palestina. Tunategemea usambazaji mdogo wa mafuta ili kudumisha shughuli zetu. Mafuta yakiisha, hospitali hii inabaki kama kaburi la watu wengi. Mgogoro huu unaoendelea sio tu unahatarisha ustawi wa haraka wa watu lakini pia unaweza kusababisha janga la afya ya umma."

Mkunga katika wodi ya wazazi Al-Shifa:

"Tangu kuzuka kwa hali hii, tumetenganishwa na familia zetu kwa vile, tunafanya kazi bila kupumzika, rasilimali ni chache na vifaa ambavyo havitoshi. Lakini pia hatuwezi kupuuza hali mbaya inayowakabili wanawake wajawazito wenyewe. Wengi wao sasa ni wakimbizi wa ndani shuleni, na kuna ukosefu wa vitu muhimu kama vile nguo na vifaa vya kujisafi, na pia bila faragha au mabafu ya kuoga. Huduma za afya ya msingi zimekuwa ndoto ya mbali. Wengine wanalazimika kujifungulia nyumbani au wakiwa njiani kwenda hospitalini."

Mkurugenzi wa hospitali ya Al Awda:

Anasema "Haiwezekani kuwahamisha wagonjwa wetu. Tunakaa na tutaendelea kusaidia wagonjwa wetu."

Ushuhuda wa wafanyakazi wa UNFPA:

Mustafa

Mustafa ni baba ya watoto 4, alikimbia makazi yake yalipoharibiwa katika shambulio la kijeshi na anasema, "Wakati wa kuhama kwa mara ya 4, tulikuwa tukikimbia bila sababu, tukiwa hatujui ni wapi pa kupata makao. Milio ya makombora ilirindima hewani, na vumbi likatufunika. Katikati ya hayo yote, mtoto wangu wa miaka 3 alipiga kelele akisema ‘kiatu changu kimeanguka, sitaki kufa bila viatu' .Tulipofika kwenye makazi hayo, tulipata umati wa watu waliokuwa wamekata tamaa na wamejawa na huzuni. Tukaungana na wale waliokuwa wakisaidia majeruhi kupitia kazi yetu ya UNFPA. Tunalia kwa ajili ya utu na haki za msingi za  wanawake. Nilihangaika nikitafuta maji safi ya kunywa. Tumetenganishwa na familia yangu. Ninapojaribu kulala usiku, ninahofia kwamba hata mmoja wetu hatakuwa hai asubuhi."

Mohammed

"Nimejawa na hofu na wasiwasi juu ya mama na dada zangu huko Gaza. Hili ni janga la kwanza kunipata nikiwa nje ya Gaza. Tulikuwa pamoja, tukisaidiana katika nyakati ngumu kama hizi, lakini sasa niko peke yangu. Jamii zimelazimika kuhama makazi yao mara 4, na siwezi kuwafikia kwa dakika moja au mbili kila siku ili kusikia sauti zao tu na kujua kwamba bado wako hai.”

Osama

"Mimi na familia yangu sote tuko watu 8. Sasa tuko kusini mwa mji wa Rafah. Watu wamehamia hapa kwa wingi, makazi yenye msongamano wa watu. Kuna ukosefu wa chakula, maji, umeme, na juu ya yote usalama. Vifaa vya matibabu katika vituo vya afya havipo, kwa hivyo watoa huduma za afya hawana uwezo wa kufanya kazi yao, tunaomba dunia mzima tuungane pamoja tukomeshe ukatili huu, napaza sauti yangu usikike dunia nzima. tunahitaji msaada wako. Hii lazima ikome. Mauaji haya, kichaa hiki kikome. Majeruhi karibu wote ni raia. Msiitusahau."

Shirika la UNFPA

Shirika la UNFPA linasema dola milioni 6.9 zinaitajika ili kusaidia huduma za dharura za afya ya uzazi na kuwahudumia waathirika wa kijinsia katika Ukanda wa Gaza na Ukingo wa Magharibi.

Tumewasilisha vifaa muhimu vya kujisafi kwenye makazi ya shirika la Umoja wa Mataifa la msaada kwa wakimbizi wa Kipalestina, UNRWA na vingine vimewekwa kwenye mpaka wa Rafah limeongeza sirika hilo.

UNFPA pia inaendesha huduma za msaada na linawashauri madaktari walio na taaluma ya kusaidia vijana na wanawake walio na matatizo ya msongo wa mawazo.