Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kupambana na taarifa potofu kwa ajili ya amani na usalama nchini DR Congo

SRSG Bintou Keita akikutana na watu walioathiriwa na maafa huko Kalehe, Kivu Kusini.
MONUSCO/Michael Ali
SRSG Bintou Keita akikutana na watu walioathiriwa na maafa huko Kalehe, Kivu Kusini.

Kupambana na taarifa potofu kwa ajili ya amani na usalama nchini DR Congo

Amani na Usalama

Taarifa potofu zinaleta hatari kubwa kwa operesheni za kulinda amani za Umoja wa Mataifa. Zikiiruhusiwa kushamiri, haziathiri tu mtazamo wa operesheni za ulinzi wa amani na kuleta mkanganyiko kuhusu jukumu la walinda amani, bali pia zinaweza kuweka maisha yao hatarini.

Amesisitiza hilo Bintou Keita, mwakilishi maalum wa Umoja wa Mataifa nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na mkuu wa ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini humo MONUSCO, na kuongeza kwamba makundi yenye silaha yanaeneza uongo kwa makusudi ili kuchochea hali ya kutoridhika dhidi ya ujumbe huo wa Umoja wa Mataifa.

Wanafanya hivyo kwa sababu wana nia ya kuizuia MONUSCO kuwa shahidi wa vitendo vyao, Bi. Keita ameiambia UN News katika mahojiano ya kina muda mfupi baada ya kutoa taarifa kwenye Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, ambalo linasimamia operesheni zote za kulinda amani duniani kote.

Ameeleza jinsi MONUSCO inavyopambana na taarifa potofu na upotoshaji mashinani, na kushirikiana na vijana ili kuwawezesha kuzuia kuenea kwa taarifa za uongo.

Aliwataarifu mabalozi kuhusu hali nchini humo, kwa kuzingatia wito wa Rais Félix-Antoine Tshisekedi Tshilombo kwenye Mjadala Mkuu wa Umoja wa Mataifa wiki iliyopita, kwa wito wa kutaka kuharakisha mpango wa uondokaji wa MONUSCO nchini humo.

Timu ya MONUSCO kwenye misheni ya kushirikisha jamii huko Uvira na Sange, Kivu Kusini.
MONUSCO/Kevin Jordan
Timu ya MONUSCO kwenye misheni ya kushirikisha jamii huko Uvira na Sange, Kivu Kusini.

Swali: Katika mjadala mkuu wa hivi majuzi, Rais wa DRC alisema ilikuwa muhimu kuharakisha kujiondoa kwa MONUSCO. Unakubaliana naye kwamba hali ya sasa inahitaji kuongeza kasi ya kuondoka?

Bintou Keita: Ili kuandaa mazungumzo, dhana ya kuongeza kasi ni muhimu, lakini muhimu pia ni ukweli kwamba ujumbe wa MONUSCO, tayari umekuwa ukihama majimbo mengi nchini DRC. Kwa mfano, tumejiondoa katika jimbo la Kasai tangu Juni 2021. Pia tulijiondoa katika jimbo la Tanganyika mwezi Juni 2022.

Na kwa ukubwa wa nchi hiyo, ambapo kuna majimbo 26, MONUSCO sasa iko katika majimbo matatu tu, Ituri, Kivu Kaskazini na Kivu Kusini, na haya ni majimbo matatu ambayo kuna migogoro inayoendelea na vikundi vyenye silaha  vikundi vyote vya wenyeji vyenye silaha na pia vya kigeni.

Kwa hivyo, kuongeza kasi ya kuondoka au kujiondoa kwetu kutoka DRC kutakuwa kutoka kwenye majimbo haya matatu, na itafanyika katika majadiliano na mazungumzo na mamlaka ya kitaifa na mamlaka za mkoa, ili kuamua, kwa kuzingatia maeneo ambayo Ujumbe  wetu unatoa ulinzi kwa wananchi. Na hakuna jeshi la kutosha au polisi wa kutosha kuhakikisha kwamba watakuwepo. 

Kwa sasa tunajiondoa na wao ndio watasimamia na kuchukua jukumu la kulinda raia. Hilo litafanyika hivi karibuni kwa sababu tunaelewa kuwa ni jitihada ya pamoja, mmoja anapanda ngazi ya mamlaka ya kitaifa na moja anatoka, ambaye ni MONUSCO.

Nchini DRC, majimbo 26 yenye wilaya 145, kati ya majimbo hayo 26 tuko katika majimbo matatu ambayo ni maeneo yenye changamoto kubwa ambazo tunaziangalia katika mikoa mitatu, tunapoongelea maeneo, ni zaidi au chini ya 15 hadi 20 ambapo tunapaswa kupigilia msumari kwenye suala la ulinzi kwa raia, kwa sababu pia tunafanya ulinzi kupitia njia nyingine ambayo ni utetezi na uelimishaji ambao ni sehemu ya operesheni ya MONUSCO kufanya kazi na mamlaka ya mkoa na ya kitaifa.

Bi. Keita akizungumza na wanahabari huko Kalehe, Kivu Kusini.
MONUSCO/Michael Ali
Bi. Keita akizungumza na wanahabari huko Kalehe, Kivu Kusini.

Swali: Maandamano yameandaliwa dhidi ya MONUSCO. Je, unafikiri kwamba jukumu la walindaamani halieleweki na kwamba taarifa potofu zina sehemu katika mtazamo wa jukumu la ujumbe wa Umoja wa Mataifa?

Bintou Keita: Nadhani ndiyo, kwa sababu kuna mgawanyiko kati ya matarajio ya ya watu kuhusu utekelezaji wa mamlaka na hasa yale yanayohusiana na jeshi, kwa sababu hii ni sehemu ambayo ni ulinzi wa raia.

Watu wana maoni kwamba ikiwa mtu yeyote atapoteza maisha yake au mbele ya jeshi la MONUSCO, inamaanisha kuwa MONUSCO haifanyi kazi yake ipasavyo. Hii bila shaka ni mtengano mkubwa, kwa sababu ukweli ni kwamba ulinzi wa kimwili ni ukaribu na uwepo, na pia inapokonya silaha kwa njia kadhaa kwa makundi yenye silaha kuja karibu na watu.

Upotoshaji huo ni sehemu ya kuelezea hasira na kufadhaika kutoka kwa wananchi lakini pia ni ghiliba kutoka kwa mashirika kadhaa kwa sababu yana nia ya kuchafua uhalali wa uwepo wa MONUSCO pamoja na kwamba yana nia ya kutotaka kuwepo kwa ujumbe huo kama shahidi wa baadhi ya mambo wanayofanya katika majimbo hayo matatu.

Swali: Je, una mfano maalum wa hatua zilizochukuliwa na MONUSCO kupambana na taarifa potofu?

Bintou Keita: Ndiyo, tangu mwaka jana tumeongeza jinsi tunavyokabiliana na upotoshaji. Moja ya shughuli hizo ni kupitia kufanya warsha na vijana ambapo wenzetu katika mawasiliano wanawafundisha vijana kuelewa tofauti kati ya habari za uwongo, tarifa potofu na upotoshaji.

Tunawafundisha vijana kuamua, kujizuia, kusimama na kujiuliza je, ninaweza kushiriki hili? Ndiyo au hapana

Tunawafundisha kuamua, kunyamaza, kusimama na kuuliza “Je, ninaweza kushiriki hili? Ndiyo au hapana”.

Na ninapoona mwitikio wa vijana inaonekana kama wanaelewa, wanafahamu zaidi mitandao ya kijamii ambayo kwa namna fulani kila kitu kinaenda, ikiwa ni pamoja na upotoshaji na tarifa za uongo.

Nikupe mfano mmoja tu, wakati sehemu ya mjadala mkuu wa Baraza Kuu ukiendelea, nilikuwa Kinshasa wakati mtu alipoamua kutengeneza habari ya uongo ambayo ilikuwa ni picha yangu niliyopia nadhani miaka mitatu iliyopita, nikiwa msaidizi wa Katibu Mkuu kwa masuala ya Afrika huko New York na ilikuwa na maandishi ambayo yalikuwa yakisema kimsingi kwamba mimi, kama mkuu wa MONUSCO, nilikuwa nikipinga kuondoka kwa ujumbe wa Umoja wa Mataifa. Hili si kweli kwa sababu, kwanza, sikuwa hapa kwenye mkutano mkuu nilikuwa Kinshasa.

Tulikuwa na mjadala juu ya nini tunafanya, tutasema kwamba hii ni habari potofu? Mwishowe tunafanya nini? Nadhani wenzangu waliamua, sawa, ni habari potufu na ilikwenda.

Moja ya mambo ambayo ni muhimu zaidi ni ufuatiliaji wa mitandao ya kijamii, na wenzangu wa MONUSCO sasa wana ripoti za wiki mbili kila mwezi ili kuona mwenendo na mwelekeo wa mijadala kuhusu MONUSCO na kwa msaada wa wenzetu hapa Makao Makuu New York wanatusaidia sana kuweka mambo katika njia fulani na maelezo kuhusu nini kinafanywa na Ujumbe wa Umoja wa Mataifa na niniambacho hakihusiani na ujumbe huo. 

Afisa wa MONUSCO akizungumza katika maingiliano na jamii ya eneo hilo kuhusu ushiriki wa wanawake katika ujenzi wa amani, mjini Kinshasa.
MONUSCO/Lydie Betyna
Afisa wa MONUSCO akizungumza katika maingiliano na jamii ya eneo hilo kuhusu ushiriki wa wanawake katika ujenzi wa amani, mjini Kinshasa.

Swali: Swali langu la mwisho ni kuhusu uchaguzi. Uchaguzi huo mkuu umepangwa kufanyika mwishoni mwa mwaka huu. Ni aina gani ya msaada MONUSCO inatoa kwa mamlaka kuandaa chaguzi hizi?

Bintou Keita: Tuna majukumu tofauti:

Mojawapo ya majukumu ni kutoa msaada wa vifaa kwa Tume ya Uchaguzi, haswa, katika majimbo matatu ambayo tumetumwa  huko Ituri, Kivu Kaskazini na Kivu Kusini ambayo tunaifanya.

Pili ni uchagizaji wa kuhakikisha kwamba vigezo na kanuni za kuhakikisha ubora wa uchaguzi, unaohusiana na uwazi na uaminifu wa uchaguzi, utulivu wa mwenendo wa uchaguzi na ujumuishwaji. Tukiona vitendo, maneno au uingiliaji kati ambao hauendani na kanuni hizo, tutakuwa tunazungumza na wadau wote popote pale walipo. Na tunafanya hivi sio peke yetu, tunafanya hivi na washirika, jumuiya ya kidiplomasia nchini DRC na pia mashirika ya kiraia, ili iwe juhudi za ushirikiano na za pamoja.

Pia tunapanga, pamoja na wizara ya mambo ya ndani, kuhusu usalama wakati wa uchaguzi. Njia tunayofanya hivi  sasa ni kuwa na mtaalam wetu kuingizwa ndani ya kikosi kazi cha kiufundi chini ya uwakilishi wa wizara.

Pia tunayo mengi yanayoendelea kuhusiana na kujumuishwa katika uchaguzi, hasa katika utekelezaji wa azimio la Baraza la Usalama namba 1325, ambapo kwetu sisi uwakilishi wa wanawake, ushiriki wa wanawake, ni muhimu kabisa, iwe kama mpiga kura au mgombeaji uchaguzi wa majimbo au Bunge la kitaifa, lakini pia kama wagombea urais.

Kwa hivyo, tunafanya mafunzo mengi kwa wagombea wanawake ili kuwa na uthubutu, kuingia katika masomo ambayo kwa kawaida watu hawawatarajii kwenda.