Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Fahamu kuhusu Kifua Kikuu au TB, kwa nini wengine huugua mara kwa mara?

Mkimbizi wa Kisomali ambaye aligunduliwa kuwa na ugonjwa wa kifua kikuu mwaka wa 2017 akiweka x-ray ya kifua chake katika kambi moja huko Djibouti anakoishi na familia yake.
UNDP/Aurélia Rusek
Mkimbizi wa Kisomali ambaye aligunduliwa kuwa na ugonjwa wa kifua kikuu mwaka wa 2017 akiweka x-ray ya kifua chake katika kambi moja huko Djibouti anakoishi na familia yake.

Fahamu kuhusu Kifua Kikuu au TB, kwa nini wengine huugua mara kwa mara?

Afya

Kifua Kikuu au (TB) ni ugonjwa wa kuambukiza ambao huathiri mapafu na kusababishwa na bakteria. Ugonjwa huu husambazwa kwa njia ya hewa wakati watu walioambukizwa wanapokohoa, kupiga chafya au kutema mate. 

Shirika la Umoja wa Mataifa la Afya ulimwenguni, WHO linataja kimelea au bakteria anayesababisha ugonjwa huo kuwa ni Mycrobacterium Tuberculosis ambaye huathiri mfumo wa hewa. 

Dokta Abdallah Keresa kutoka  kitengo cha Kliniki ya kifua kikuu na Virusi vya Ukimwi (VVU)  Hospitali ya Rufaa ya kanda ya Bugando, Tanzania.
UN News/Evarist Mapesa
Dokta Abdallah Keresa kutoka kitengo cha Kliniki ya kifua kikuu na Virusi vya Ukimwi (VVU) Hospitali ya Rufaa ya kanda ya Bugando, Tanzania.

Vimelea vya TB vinapenda kukaa eneo la mwili lenye hewa 

Daktari Abdallah Keresa kutoka Kitengo cha Kliniki ya kifua kikuu na Virusi vya Ukimwi (VVU) kutoka Hospitali ya Rufaa ya kanda ya Bugando, mkoani Mwanza nchini Tanzania ameiambia UN News kuwa mfumo huo “ndiyo maana unaona mtu akiwa na vimelea hivyo kwenye kifua chake, anapokuwa akiimba, akikohoa, akicheka au kupiga chafya wale vimelea wanaweza kuruka kutoka kwa mtu mmoja kwenda kwa mtu mwingine”. 

Hivyo anasema sehemu ambayo bakteria hao wanakaa ni eneo la mapafu, kwa sababu eneo hilo ni laini na limetengenezwa katika namna ambayo kuna sehemu ambamo kuna vitu kama vimepangwa, kwa hiyo wakiingia wanakaa pale, kwasababu vimelea vinapenda hewa na sehemu ambayo ina hew ani  kwenye mapafu ndiyo maana ni rahisi kuambukizwa kwa njia ya hewa. 

Daktari akihudumia mgonjwa hospitalini anayeugua kifua kikuu huko Mumbai, India.
© WHO/David Rochkind
Daktari akihudumia mgonjwa hospitalini anayeugua kifua kikuu huko Mumbai, India.

Dalili za TB ni zipi? 

Kwa mujibu wa Dokta Keresa, dalili za TB huanza kuonekana siku chache tu baada ya mgonjwa kuambukizwa na hivyo ni rahisi kueneza TB kwa wengine bila kujua. 

Dalili hizo ni pamoja na Kikohozi cha muda mrefu (mara nyingine na damu), Maumivu kifua, Udhaifu, Uchovu, Upungufu wa uzito, Homa, Kupiga jasho usiku. 

“Mtu anapopata maambukizi ya TB ndani ya wiki tatu hadi tisa anaweza kuanza kuonesha dalili, katika muda huu yule bakteria anakuwa anatengeneza njia ya kuutafuna mwili, ndiyo maana uzito unaweza kupungua kwa kasi”. 

“Kwa hiyo hizo dalili za homa, kikohozi zaidi ya wiki mbili, kupungua uzito, jasho nyakati za usiku hadi mtu analowanisha pale alipo lala hizo ndizo zinaweza kutufanya tujue mtu ana kifua kikuu”. 

Mchoro wa mfano wa bakteria sugu ya kifua kikuu ya Mycobacterium.
CDC/Alissa Eckert, James Archer
Mchoro wa mfano wa bakteria sugu ya kifua kikuu ya Mycobacterium.

Kwanini TB bado ni tatizo? 

Tarehe 24 mwezi Machi kila mwaka dunia huadhimisha siku siku ta TB au Kifua Kikuu, ambapo huweka kauli mbalimbali zenye lengo la kukuza uelewa na kupambana na janga hilo ambalo limekuwa likizidi kupoteza Maisha ya watu Ulimwenguni. 

Takwimu za shirika la Umoja wa Mataifa la afya ulimwenguni, WHO zilizochapichwa katika tovuti yake mapema Aprili, 2023, zinaonesha kuwa watu milioni 1.6 (ikiwa ni pamoja na watu 187,000 wenye maambukizi ya ukimwi) walikufa kwa ugonjwa wa Kifua Kikuu duniani. 

Mwaka 2021, inakadiriwa kuwa watu milioni 10.6 walipata ugonjwa wa TB ulimwenguni kote, wanaume milioni 6, wanawake milioni 3.4, na Watoto milioni 1.2 waliambukizwa maradhi hayo katika maeneo mbalimbali duniani. 

Takwimu za WHO zinaonesha kuwa tangu mwaka 2000 watu milioni 74 wamesalimika baada ya kupona Kifua Kikuu kutokana na mashirika mbalimbali ulimwenguni kuweka mikakati ya kupambana na ugonjwa huo.  

Dokta Keresa anasema, “ongezeko la wingi wa watu, misongamano ambavyo watu wanakutana kwa wingi hasa katika nchi zilizopo kusini mwa janga wa Sahara, na ukiangalia ugonjwa huu unaambukiza kwa njia ya hewa inakuwa ni rahisi mtu kupata maambukizi”. 

“Pia ongezeko la magonjwa hasa yale yanayoshusha kinga ya mwili, kwasababu TB inamuathiri pia mtu ambaye anamagonjwa yanayoshusha kinga ya mwili kama kisukari, saratani, Maambukizi ya Virusi vya Ukimwi, pamoja na watu wenye lishe duni, inapelekea watu kuendelea kuugua TB”, Alisema Dokta Keresa. 

Mkimbizi kutoka Sudan akisubiri matibabu katika kituo cha afya cha UNHCR Tripoli, Libya
UNOCHA/Giles Clarke
Mkimbizi kutoka Sudan akisubiri matibabu katika kituo cha afya cha UNHCR Tripoli, Libya

Kuna uwezekano wa mtu kupona TB kisha Kuugua Tena? 

TB ni ugonjwa wa kuambukizwa kutoka kwa mtu mmoja kwenda kwa mwingine, na ili kuweza kupona ama kutibu tatizo hilo ni sharti mtu aliye na tatizo hilo kuwahi kupata huduma ya matibabu ikiwemo kumaliza dozi ya dawa anazopewa na wataalam wa afya. 

Lakini mtu anaweza kupona tatizo hilo na kisha kuugua tena hii itategemeana na namna atakavyo weza kujiepusha na mikusanyiko pamoja na kuchukua tahadhari zote ambazo wataalam wa afya huwa wanasisitiza kuzifuata. 

“Ugonjwa wa TB ni wa kuambukizwa, unaweza kutumia dawa leo ukapona baadaye ukaja kuambukizwa tena, kama mtu huyo ataingia kwenye tabia hatarishi. Kama umeshaugua sasa hivi na ukatumia dawa vizuri na wakati wa kutumia hizo dawa ukawa unafuatiliwa vizuri na ukaacha kujihusisha kwenye makundi au kukaa na mtu mwenye Kifua Kikuu, hauwezi kupata maambukizi”. 

Lakini kama utaenda kukaa tena na mtu anayekohoa akakuambukiza ni rahisi kuugua tena TB, pia kuna wale ambao wanatumia dawa akianza kujisikia vizuri anakatisha dozi, mtu huyu atakuwa katika hatari tena ya kuja kuugua tena kwasababu hao wadudu ni kama wanakuwa wamelala tu, baadaye wataamsha tena ule ugonjwa kumbe ndiyo yeye tu aliwafubaza tu, hakumaliza matibabu”.alisema Dokta Keresa. 

chanjo
©UNICEF/UN0265424/Chute
chanjo

Chanjo ya TB 

Kwa sasa chanjo dhidi ya Kifua Kikuu au TB inaitwa bacille Calmette-Guérin (BCG) ambayo imeanza kupatiwa binadamu tangu mwaka 1921. Chanjo hii ni miongoni mwa chanjo zilizomo katika programu za utoaji chanjo kwa watoto wachanga.