Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Nalaani vikali uporaji katika ofisi za WFP Khartoum mwishoni mwa wiki: Guterres

Ghala za WFP katika bandari ya Sudan zinahifadhi bidhaa za chakula kwa ajili ya usambazaji wa dharura.
© WFP/Mohamed Elamin
Ghala za WFP katika bandari ya Sudan zinahifadhi bidhaa za chakula kwa ajili ya usambazaji wa dharura.

Nalaani vikali uporaji katika ofisi za WFP Khartoum mwishoni mwa wiki: Guterres

Msaada wa Kibinadamu

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres leo amelaani vikali uporaji wa makao makuu ya shirika la Umoja wa Mataifa la mpango wa chakula duniani WFP, mjini Khartoum mwishoni mwa juma.

Guterres kupitia taarifa iliyotolewa na naibu msemaji wake mjini New York Marekani hii leo amesema “Huu ni ukiukaji wa hivi karibuni kabisa dhidi ya vituo vya misaada ya kibinadamu tangu kuanza kwa mzozo huo, ambao sasa uko katika wiki yake ya nne.”

Farhan Haq akiwasilisha taarifa hiyo mbele ya waandishi wa habari amesema "Wengi wao kama sio wote, mashirika ya Umoja wa Mataifa na washirika wetu wa kibinadamu wameathiriwa na uporaji mkubwa."

Kulingana na Haq, "Katibu Mkuu anasisitiza haja ya pande zote kulinda na kuheshimu wafanyikazi wa kibinadamu na vifaa vyao, pamoja na hospitali. Raia na miundombinu ya kiraia lazima ilindwe ili kuokoa maisha. Mahitaji ya watu wa Sudan, ambao wamekumbwa na maafa ya kibinadamu, lazima yapewe kipaumbele."

Msemaji huyo ameongeza kuwa "Sisi na washirika wetu tunafanya kazi kupanua shughuli za kibinadamu. Hii ni pamoja na juhudi za kuhamisha vifaa ndani na nje ya nchi, tunaposhughulikia mahitaji yanayokua kwa kasi”.

Msaada unaotolewa na mashirika ya UN

Ameendelea kusema kuwa, "Katika Jimbo la Blue Nile, shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF na washirika wake wanasaidia programu za afya na lishe, ikiwa ni pamoja na chanjo, uchunguzi na matibabu ya utapiamlo, pamoja na huduma za ujauzito na afya ya uzazi."

Haq pia ameripoti, kuwa "Katika eneo la Darfur Kaskazini, washirika wetu wa kibinadamu wanasaidia vituo vya afya na dawa, maji na vitu vingine. Vituo 20 vya kutolea huduma za afya vimepokea msaada wa maji, usafi wa mazingira na usafi, na angalau lita 100,000 za maji zimeingizwa ndani.”

Naibu Msemaji huyo wa Umoja wa Mataifa pia amesema, "Tarehe 5 Mei, tani 30 za vifaa vya matibabu ziliwasili Port Sudan na kwa ushirikiano wa shirika la afya la Umoja wa Mataifa duniani WHO, na Umoja wa Falme za Kiarabu.

Usafirishaji huo ulikuwa na vifaa vya kutosha zikiwemo dawa muhimu na vifaa vya upasuaji wa dharura ili kuweza kufikia watu 165,000 kupitia vituo 13 vya afya.

Kulingana naye, hiyo ni mara ya kwanza kwa WHO kupeleka ndege nchini Sudan tangu mzozo huo kuzuka.

Haq amebainisha kuwa "Wakati huo huo, kibali cha forodha kimekamilika kwa tani 80 za vifaa vya matibabu ambavyo vilishushwa huko Port Sudan wiki iliyopita. Hii ni pamoja na drip za maji na vifaa kwa ajili ya matibabu ya majeraha, kiwewe na utapiamlo mkali sana."

Haq amehitimisha kwa kusema kuwa, "Hii ni mara ya kwanza WFP itatoa msaada wa dharura wa chakula huko Gezira, ambapo tunaona familia mpya zilizokimbia makazi yao zikikimbia mzozo wa Khartoum."