Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Zaidi ya watu 1,000 wanasafiri kila siku kutoka Sudan hadi Ethiopia - IOM

Maelfu ya watu wamewasili katika mji wa Metema, mpakani kati ya Sudan na Ethiopia, tangu mapigano nchini Sudan.
IOM
Maelfu ya watu wamewasili katika mji wa Metema, mpakani kati ya Sudan na Ethiopia, tangu mapigano nchini Sudan.

Zaidi ya watu 1,000 wanasafiri kila siku kutoka Sudan hadi Ethiopia - IOM

Amani na Usalama

Zaidi ya watu 12,000 wamewasili Metema, mji wa mpakani kati ya Sudan na Ethiopia, tangu mapigano yalipozuka tarehe 15 Aprili mwaka huu 2023, wengi wao wakiwa wamechoka baada ya safari ndefu na hatari kuelekea kwenye usalama, imeeleza taarifa ya Shirika la Uhamiaji la Umoja wa Mataifa, IOM iliyotolewa hii leo Geneva - Uswisi na Metema-Ethiopia.

Kupitia IOM, ufuatiliaji wa  wanaofurushwa kwa sasa umerekodi zaidi ya watu elfu moja wanaowasili kila siku, miongoni mwao wakiwa raia wa Sudan, Waethiopia wanaorejea na raia wa nchi ya tatu kutoka Uturuki, Eritrea, Somalia, Kenya na zaidi ya nchi nyingine 50. 

IOM inawasaidia wale wanaowasili Ethiopia, wakiwemo kutoka nchi ambazo balozi zao zilituma maombi ya kusaidia raia wao. 

Msaada huo unajumuisha usafiri kutoka mpakani hadi Gondar na Addis Ababa, pamoja na malazi katika Vituo vya Usafiri vya IOM kwa baadhi. Wengi wa wale wanaokimbia Sudan wanaingia Ethiopia bila rasilimali na mali zao. Bila msaada, wana hatari ya kukwama katika mji mdogo wa mpakani. 

Takriban Wakenya 200, baadhi yao wakiwa wanafunzi, zaidi ya Waganda 200 na zaidi ya raia 800 wa Somalia ni miongoni mwa wale ambao wamesaidiwa. 

Nuru*, (jina lake lililotumika hapa si halisi) mwanafunzi Mkenya anayesomea shahada ya uzamili ya sheria nchini Sudan alipokuwa akifanya kazi ya muda ya kibinadamu, anaeleza jinsi alivyonaswa vita ilipozuka na hakuweza kupata nyaraka na mali zake kabla ya kukimbia. 

"Nilisikia kwamba gorofa iliyo karibu na yangu ilikuwa imelipuliwa na kuharibiwa kabisa," amesema, “Hapo ndipo niliamua kuondoka bila nyaraka zangu. Maafisa wa ubalozi waliweza kunipa kitambulisho cha muda kwa ajili ya kusafiri.” 

IOM pia iliwezesha familia ya Kitanzania kupata matibabu ya haraka na hatimaye kurejea Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Gondar kwa usaidizi wa ubalozi wao mjini Addis Ababa. 

Wengi wa waliowasili ni Waethiopia (asilimia 39), Wasudan (asilimia 17) na Waturuki (asilimia 13). Asilimia 20 ya wanaowasili ni watoto. 

Kituo cha Kukabiliana na Uhamiaji cha IOM (MRC) huko Metema kinaendelea kusaidia Waethiopia walio katika mazingira magumu wanaorejea, kutoa usaidizi muhimu, ikiwa ni pamoja na makazi huko, kabla ya kurejea katika jamii  zao za asili. 

"Tunashukuru msaada kutoka kwa wafadhili wetu ambao walituruhusu kutoa msaada mara moja huku tukiiomba jumuiya ya kimataifa ufadhili zaidi ili kukidhi mahitaji muhimu," anasema Abibatou Wane-Fall, Mkuu wa IOM Ethiopia. 

Miongoni mwa mahitaji muhimu zaidi ni vifaa vya ziada vya Maji, Usafi wa Mazingira na Usafi (WASH), maji, chakula, malazi kwa maeneo ya kusubiri, msaada wa matibabu na usafiri wa kuendelea mbele.