Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Papa Benedict XVI hakuchoka kutafuta amani na kutetea haki za binadamu: Guterres

Papa Benedict XVI akisalimiana na Wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa wakati wa ziara yake katika Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa mwezi Aprili 2008.
Picha ya UN/Eskinder Debebe
Papa Benedict XVI akisalimiana na Wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa wakati wa ziara yake katika Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa mwezi Aprili 2008.

Papa Benedict XVI hakuchoka kutafuta amani na kutetea haki za binadamu: Guterres

Masuala ya UM

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres ametoa waraka wa masikitiko kutokana na kifo cha Papa wa zamani wa kanisa katoliki, Benedict XVI, kilichotokea mapema leo Jumamosi.

 

 

Katika taarifa ya Katibu Mkuu iliyotolewa na msemaji wake, Bwana Guterres ameonesha "huzuni kubwa" na kusema kwamba papa huyo wa zamani alikuwa mtu mnyenyekevu, wa maombi na masomo.


Papa Benedict XVI aliongoza Kanisa Katoliki duniani kote kwa takribani miaka nane kuanzia mwaka 2005 hadi 2013.


Ulinzi wa haki za binadamu


Kwa mujibu wa mashirika ya habari, papa huyo wa zamani amefariki dunia mjini Vatican Jumamosi hii asubuhi na Jumatano, wakati wa hadhara ya kila wiki, Papa wa sasa, Francis alikuwa tayari ameomba maombi kwa ajili ya mtangulizi wake Benedict XVI, ambaye ugonjwa ulikuwa umeshamzidia.


Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amekumbushia ziara ambayo papa huyo wa zamani aliifanya kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York mwaka 2008, alipopokelewa na kiongozi wa Umoja wa Mataifa wakati huo, Ban Ki-moon.


Guterres amesema kuwa Papa mstaafu alilinda kanuni za imani, hakuchoka katika harakati zake za kutafuta amani na kuamua katika kutetea haki za binadamu.


Pia Mkuu wa Umoja wa Mataifa ameeleza kuwa Benedict XVI alikuwa mwongozo wa kiroho kwa mamilioni ya watu duniani kote na mmoja wa wasomi wakubwa wa theolojia wa kizazi chake.


Maisha ya maombi na kujitolea kwa amani


Alipozuru Umoja wa Mataifa mwaka wa 2008, Papa Benedict alitoa wito wa "kujenga uhusiano wa kimataifa kwa njia ambayo inaruhusu kila mtu na watu wote kuhisi kwamba wanaleta mabadiliko."


Kwa mujibu wa Guterres, wito wenye nguvu wa Benedict wa 16 wa mshikamano na watu waliotengwa na wito wa dharura wa kuziba pengo kati ya matajiri na maskini unasalia kuwa muhimu zaidi kuliko hapo awali.


Bwana Guterres amehitimisha ujumbe huo kwa kutoa salamu za rambirambi kwa Wakatoliki na watu wengine duniani kote ambao wamehamasishwa na maisha ya sala na kujitolea kwa dhati kupinga ghasia na amani kulikooneshwa na Benedict XVI.


Benedict XVI atazikwa Januari 5 huko Vatican


Papa huyo wa zamani aliongoza Kanisa Katoliki kuanzia mwaka 2005 hadi 2013 na kujiuzulu wadhifa huo, akifuatiwa na Papa Francis wa sasa. Anajulikana kwa jina la Kardinali Joseph Ratzinger wa Ujerumani, kabla ya kuchaguliwa kuwa papa akiwa na umri wa miaka 78, alichukuliwa kuwa msaidizi wa karibu wa Papa John Paul II. Vatican imesema kuwa mwili wa Benedict XVI utalazwa katika Kanisa kuu la Mtakatifu Petro kuanzia Januari 2, na mazishi yataongozwa na Papa Francis mnamo Januari 5.

Rais wa Baraza Kuu 

Kwa upande wake Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataiafa, Csaba Kőrösi kupitia ukurasa wake wa Twitter ameandika, “Baba Mtakatifu Mstaafu Benedict XVI alikuwa ni mtu anayeongozwa na maadili, imani, ujasiri na upendo wake. Nilibahatika kukutana naye Vatican. Tabasamu lake la upole na sauti nyororo zilikuwa na nguvu sana. Aliona changamoto kubwa mbele yetu na alikuwa na uwezo wa kuonesha njia.”