Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNESCO imeshtushwa na kifo cha nguli wa soka duniani Pelé

Gwiji wa soka wa Brazil Pele akizungumza wakati wa uzinduzi wa muungano wa watoto kati ya FIFA na UNICEF katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa
© UNICEF/Susan Markisz
Gwiji wa soka wa Brazil Pele akizungumza wakati wa uzinduzi wa muungano wa watoto kati ya FIFA na UNICEF katika makao makuu ya Umoja wa Mataifa

UNESCO imeshtushwa na kifo cha nguli wa soka duniani Pelé

Utamaduni na Elimu

Mwanasoka nguli  kuwahi kushuhudiwa duniani Pelé amefariki dunia katika hospitali ya Sao Paulo nchini Brazil akiwa na umri wa miaka 82.

Jabali huyo wa kandanda alikuwa akitibiwa saratani ya utumbo mpana tangu mwaka jana. 

Shirika la Umoja wa Mataifa la elimu, sayansi na utamaduni linalotetea nguvu ya michezo duniani kote, UNESCO, limeandika kwenye ukurasa wake wa Twitter kwamba "limehuzunishwa sana na kifo chake, na kutoa rambirambi kwa watu wa Brazil, na familia pana ya wanakandanda duniani"  

Akiwa na umri wa miaka 17, Pele alishinda kombe la dunia la soka kwa mara ya kwanza mwaka 1958, na kutwaa taji hilo mara mbili zaidi, mwaka 1962 na 1970. Alifunga mabao 1,281, na kuweka rekodi ya dunia katika miechi 1,363 wakati wa taaluma yake, ambayo ilianza akiwa na umri wa miaka 15 tu. 

Safari ya kabumbu ya Pele 

Pele alizaliwa kama Edson Arantes do Nascimento, mwaka 1940, gwiji huyo wa mpira wa miguu, aliyepewa jina la utani "Lulu Nyeusi", na "Mfalme", alistaafu mchezo wa soka mwaka 1977. 

Mwaka 1999, mchezaji huyo wa Santos na nyota anayeheshimika zaidi wa Brazil, alichaguliwa kuwa mchezaji bora wa karne katika kura ya maoni ya washindi wa awali wa Ballon d'Or  wachezaji ambao walishinda tuzo ya kila mwaka ya kandanda ya kimataifa kwa kuwa wachezaji bora mwaka huo. 

Balozi Mwema wa Shirika la Umoja wa Mataifa kuhusu Mazingira na Maendeleo (UNCED) Pelé (anayekumbatia watoto) wa Brazil, akipokelewa na watoto wakati akielekea katika ukumbi wa Plenary mjini Rio de Janeiro, Brazil.
UN Photo/Joe B. Sills
Balozi Mwema wa Shirika la Umoja wa Mataifa kuhusu Mazingira na Maendeleo (UNCED) Pelé (anayekumbatia watoto) wa Brazil, akipokelewa na watoto wakati akielekea katika ukumbi wa Plenary mjini Rio de Janeiro, Brazil.

Bao kwa ajili ya Umoja wa Mataifa 

Nguli huyo wa soka Pele alitumia muda mwingi alipostaafu kusaidia Umoja wa Mataifa na kazi yake, kama balozi wa mwema wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF, na kama bingwa wa UNESCO wa michezo, kutoka mwaka 1994. 

Pia aliteuliwa kuwa balozi mwema wa mkutano muhimu wa Umoja wa Mataifa wa dunia, huko Rio de Janeiro, mwaka 1992, moja ya mikutano mikuu ya kwanza ya maendeleo ya kimataifa na mazingira inayojikita na mustakabali endelevu zaidi kwa wote. 

Katibu mkuu wa mkutano huo, Maurice Strong, alimuelezea Pele kuwa sio tu mwanasoka bora zaidi ulimwenguni, lakini "mtu wa ulimwengu wote", mwenye asili ya Brazil. 

Aliwaambia waandishi wa habari kwamba "Kujitolea kwake kwa watu, kwa sayari, kumtofautisha na wengine na kudhihirisha kuwa ni raia wa kweli wa dunia yetu". 

UNESCO imesema katika tweet yake, kwamba Pele "amefanya kazi bila kuchoka kukuza michezo kama chombo cha amani. Atakumbukwa sana na daima.” 

Taarifa zaidi zitafuata…..