Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ushiriki wa wanawake katika utoaji na ufikishaji wa misaada Afghanistan lazima uendelee: UN na wadau

Muuguzi akiwa amesimama katika wodi ya watoto wachanga katika hospitali moja mjini Gardez, Afghanistan
© UNICEF/Mihalis Gripiotis
Muuguzi akiwa amesimama katika wodi ya watoto wachanga katika hospitali moja mjini Gardez, Afghanistan

Ushiriki wa wanawake katika utoaji na ufikishaji wa misaada Afghanistan lazima uendelee: UN na wadau

Haki za binadamu

Uamuzi wa mamlaka ya Afghanistan wa kuwapiga marufuku wanawake kufanya kazi katika mashirika ya kibinadamu yasiyo ya kiserikali NGO’s umeendelea kulaaniwa na wadau mbalimbali kutoka jumuiya ya kimataifa yakiwemo mashirika ya Umoja wa Mataifa wakisema ni pigo kubwa kwa jamii zilizo hatarini, kwa wanawake, kwa watoto, na kwa nchi nzima kulingana. 

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo na wakuu wa kamati ya kudumu ya mashirika mbalimbali kwa asjili ya Afghanistan “Wafanyakazi wa wanawake ni muhimu kwa kila kipengele cha hatua za kibinadamu nchini Afghanistan. Ni walimu, wataalam wa lishe, viongozi wa timu, wahudumu wa afya ya jamii, watoa chanjo, wauguzi, madaktari na wakuu wa mashirika. Wanaweza kufikia idadi ya watu ambayo wenzao wa kiume hawawezi kuifikia na ni muhimu katika kulinda jumuiya tunazohudumia.” 

Taarifa hiyo imeongeza kuwa wanawake pia wanaokoa Maisha na utaalam wao wa kitaaluma ni wa lazima.  

Pia imesisitiza kuwa “Ushiriki wao katika utoaji wa misaada ya kibinadamu hauwezi kujadiliwa na lazima uendelee.” 

Mtoto akipatiwa chanjo dhidi ya ugonjwa wa polio wakati wa kampeni ya uhamasishaji wa polio huko Kandahar, Afghanistan.
© UNICEF/Frank Dejongh
Mtoto akipatiwa chanjo dhidi ya ugonjwa wa polio wakati wa kampeni ya uhamasishaji wa polio huko Kandahar, Afghanistan.

Kuwazuia wanawake ni hasara kwa taifa zima 

Taarifa hiyo ya kamati imeweka bayana kwamba kupiga marufuku wanawake na kuwalazimisha kutoka kwenye kazi ya kibinadamu kuna matokeo ya papo hapo ya kutishia maisha kwa Waafghanistan wote.  

Tayari, baadhi ya programu muhimu kwa wakati huu zimelazimika kusimama kwa muda kutokana na ukosefu wa wafanyakazi wa kike.  

“Haya yanajiri wakati ambapo zaidi ya watu milioni 28 nchini Afghanistan, wakiwemo mamilioni ya wanawake na watoto, wanahitaji usaidizi ili kujikimu wakati nchi hiyo ikikabiliana na hatari ya janga la njaa, kuzorota kwa uchumi, umaskini uliokithiri na majira ya baridi kali”. Imehitimisha taarifa hiyo. 

Wito wa UNHCR kwa serikali Afghanistan 

Kwa upande wake kamishina mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR Filippo Grandi ameungana na wakuu wengine wa mashirika ya kibinadamu kutoa wito kwa serikali ya mpito ya Afghanistan kubadili maamuzi yake ya kuwazuia wanawake kufanya kazi na mashirika yasiyo ya kiserikali NGOs.  

Amesisitiza kwamba “kuzuia wanawake kufanyakazi ya kibinadamu ni kukanusha ubinadamu wao na itasababisha tu mateso na shida zaidi kwa Waafghan wote, hasa wanawake na watoto. Na marufuku hii lazima iondolewe,”  

Hofu ya UNDP kuhusu mustakbali wa Afghanistan 

Naye Achim Steiner, mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la mpango wa maendeleo UNDP, amesema ana wasiwasi mkubwa juu ya mustakabali wa Afghanistan, na ripoti za mamlaka ya Taliban za kupiga marufuku wanawake kufanya kazi kwa mashirika ya kitaifa na kimataifa yasiyo ya kiserikali. 

Bwana Steiner amesema "Pamoja na mipaka iliyowekwa katika elimu ya wasichana na wanawake, vitendo hivi vinawakilisha mmomonyoko unaoongezeka wa kuheshimu haki za binadamu na uhuru wa msingi nchini Afghanistan".  

Ameongeza kuwa, "Kuwanyima wanawake na wasichana haki hizi za msingi pia kutaongeza kasi ya Afghanistan ya kurudi nyuma katika umaskini uliokithiri na kuiweka katika hali ya hasara za kiuchumi na usawa wa kijamii vitu ambayo vinaweza kuchukua miongo kadhaa kubadilika.” 

Wadau wote wa kimataifa wamesisitiza wito wao kwa mamlaka ya Afghanistan kubadili maamuzi hayo kwa faida ya kudumisha usawa wa kijinsia, haki za binadamu na faida ya taifa zima ambalo bado linaghubikwa na jinavizi la vita vya muda mrefu.