Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Onesho la aina yake: Mhamiaji na ndoto kubwa katika eneo lisilotarajiwa

“Vipi kama ningalisalia” ni onesho lililoandikwa na kuongozwa na Hervé ili kuongeza uelewa kuhusu uhamiaji salama.
PICHA: Maktaba ya Hervé
“Vipi kama ningalisalia” ni onesho lililoandikwa na kuongozwa na Hervé ili kuongeza uelewa kuhusu uhamiaji salama.

Onesho la aina yake: Mhamiaji na ndoto kubwa katika eneo lisilotarajiwa

Wahamiaji na Wakimbizi

Kama ilivyo kwa vijana wengi wa Côte d'Ivoire, makuzi ya Hervé kwa kiasi kikubwa yamepata ushawishi kutoka kwenye vyombo vya habari. “Vilitufanya tuamini kuwa maisha ni bora zaidi barani Ulaya,” anasema Hervé.

Makala iliyochapishwa kwenye wavuti wa shirika la Umoja wa Mataifa la Uhamiaji, IOM, inasema wazazi mara nyingi huahidi watoto wao kuwa watawasafirisha kwenye nje ya nchi, kama njia ya kuwahamasisha wafanye vizuri shuleni. “Wajomba zangu walituahidi kuwa watatupeleka Ulaya na Marekani iwapo tutashika nafasi za kwanza darasani,” anakumbuka Hervé. 

Hata hivyo Hervé alikuwa na mipango mingine. “Nikiwa mtoto, nilikuwa natoa burudani kwenye sherehe, hivi ndivyo ambavyo nilianza kupenda dansi: kila mara nimekuwa na ndoto ya kuingia katika tasnia ya Sanaa nchini Côte d'Ivoire ili kufuata hatua za magwiji kama vile Serge Beynaud au Marie Rose Guiraud.” 

Bibi yangu pekee ndiye aliunga mkono ndoto yangu ya kuwa mcheza dansi

Kwa bahati mbaya, ndoto hii ya Hervé, haikuwa na nafasi kwenye makazi ya wazazi wake, ambako sanaa haikuonekana kama fursa ya kujiendeleza kiajira na hata nchini mwao Côte d'Ivoire  wakati ikigubikwa na janga la muda mrefu la kiuchumi na kijamii. 

“Nililelewa na bibi/nyanya yangu ambaye alinihamasisha wakati wote wa uhai wake masuala ya sanaa, lakini alipofariki tu, maisha yalianza kuwa magumu. Kulikuwa na shinikizo kubwa la mimi kutakiwa kufanikiwa, shinikizo ambalo halikuendana na mwelekeo wangu. Baba yangu hakupenda mimi ninavyopenda kudansi kwa hioy sikuwa na jambo lingine la kufanya zaidi ya kuondoka,” anasema Hervé. 

Mwaka 2010, kufuatia vurugu zilizoibuka baada ya uchaguzi mkuu, Hervé  aliondoka nyumbani kwao na kwenda mji mkuu wa kibiashara wa Côte d'Ivoire , Abidjan. Wakati huo hakuwa na fedha za kujikimu. “Kwangu mimi Abidjan ndio ilikuwa tegemeo langu la mwisho – nifanikiwe au nife nikijaribu kufanikiwa.” 

Sanaa ni njia yangu ya kuelezea hisia zangu,” anasema  Hervé  na kikundi cha sanaa cha Mably mara kwa mara hufanya maonesho yake kwenye mji mkuu wa Chad, N’Djamena ili kuinua uelewa kuhusu uhamiaji salama miognoni mwa vijana.
Picha: IOM
Sanaa ni njia yangu ya kuelezea hisia zangu,” anasema Hervé na kikundi cha sanaa cha Mably mara kwa mara hufanya maonesho yake kwenye mji mkuu wa Chad, N’Djamena ili kuinua uelewa kuhusu uhamiaji salama miognoni mwa vijana.

Baada ya kifo cha bibi yangu niliondoka nyumbani ili kusaka mbinu za kufikia ndoto yangu

Kwa msaada wa marafiki zake, aliweza kupata makazi kwenye mji wa Dabou, ulioko kilometa 45 kutoka Abidjan, ambako kwa miezi 6 alifanya kazi ya uvuvi na familia iliyompatia makazi. Aliweka akiba ya fedha ya kutosha na baada ya ghasia kupungua Abidjan aliamua kurejea ili aweze kujiandikisha katika shule ya Dansi na Mabadilishano ya Utamaduni, shule iliyoanzishwa na mbunifu wa mitindo ya dansi ambaye anavutiwa naye sana, Marie Rose Guiraud. 

Baada ya kuhitimu, Hervé alishiriki kwenye maonesho ya dansi mara kwa mara mjini Abidjan, fursa ambayo ilimwezesha kukutana mara kwa mara na wasanii au kuonekana kwenye matukio ya kisanii ya mjini na ndipo akapata taarifa kuhusu Chad. 

“Mwaka 2016, nilitafutwa na mbunifu wangu wa mitindo ya dansi  kwa ajili ya kwenda kufanya onesho nchini Chad,” anasema Hervé  akiongeza “ilikuwa ni fursa ya kuungana na wacheza dansi wa nchini humo amao walikuwa wanajiandaa kwa ziara ya kimataifa.” 

Wakati huo mcheza dansi huyu kijana hakuwa anafahamu chochote kuhusu Chad, na alikuwa na hofu ya kwenda eneo hilo. “Nilipoingia kwenye mtandao kutafuta taarifa kuhusu Chad, nilichoona ni picha za vita,” anakumbuka Hervé na kisha akaamua kukataa fursa hiyo. 

Niliamua kuelekea Chad ili kustawisha kipaji changu

Mwaka 2019, fursa hiyo iliibuka tena, sasa Hervé  akaamua kuondoa Abidjan kwa ajili ya kujionea kwa mara ya kwanza  kilichoko nchini Chad. Baada ya siku 10 za safari njiani, Hervé na wacheza dansi wengine wawili, hatimaye waliwasili N’Djamena, mji mkuu wa Chad. 

Siku za kwanza hazikuwa rahisi, anakumbuka kijana huyo akigusia kwanza viwango vya juu vya joto nchini Chad ikilinganishwa na viwango vya joto la kawaida nchini mwake  Côte d'Ivoir. Ilihitaji moyo wa kipekee kuweza kuhimili maisha kwenye mji huo wa N’Djamena, ambao pia ni mij mkubwa zaidi nchini Chad. 

Katika ukanda wa kusini mwa N'Djamena, unaojulikana pia kama wilaya ya Paris-Congo ndiko alikopata makazi na taratibu akaanza mchakato wa kujumuika kwenye jamii ya wananchi wa Chad. “Nakumbuka kunywa uji wa mtama kila siku kwa sababu sikuweza vyakula vya Chad,” anasema huku akicheka. 

“Vipi kama ningalisalia” ni onesho lililoandikwa na kuongozwa na Hervé ili kuongeza uelewa kuhusu uhamiaji salama.
Maktaba ya Hervé
“Vipi kama ningalisalia” ni onesho lililoandikwa na kuongozwa na Hervé ili kuongeza uelewa kuhusu uhamiaji salama.

Sasa akiwa mwenye umri wa miaka ya 30, Hervé anaishi N'Djamena na anafanya kazi kama msanii, mbunifu wa miondoko ya dansi na mjasiriamali. Anasimamia pia kkundi la vijana waafrika wanaopenda kufanya sanaa kwa ajili ya sababu za kijamii na kitamaduni liitwalo Mably Inter Association

Mchezo wa kuigiza waakisi maisha ya wahamiaji ugenini

Halikadhalika ameandika mchezo uitwao Vipi kama nikisalia, au What If I Stayed, onesho ambalo limechochewa na kifo cha mmoja wa marafiki zake wa utotoni ambaye alijaribu kwenda Ulaya kwa njia ya bahari. “Taarifa hizi zilinihuzunisha sana na ndio zilinichochea kuandika mchezo huu.” Onesho hilo linalenga kuongeza uelewa miongoni mwa vijana kuhusu hatari za uhamiaji usiofuata taratibu. 

Kwa Hervé , onesho hilo ilikuwa ni njia ya kuelezea hisia zake juu ya tukio hilo lililogharimu maisha ya mmoja wa marafiki zake wa karibu. Tabasamu lake angavu linaelezea pia simulizi yake ya safari ya hatari ya kuvuka Afrika Magharibi kabla ya kuishia Chad. 

Hervé  anasema“Sina uhakika kwa nini nilibakia, lakini kitu kimoja nina uhakika nacho ni kwamba Chad ni taifa lenye mtazamo wa kusonga mbele.
PICHA: IOM/ François-Xavier Ada Affana
Hervé anasema“Sina uhakika kwa nini nilibakia, lakini kitu kimoja nina uhakika nacho ni kwamba Chad ni taifa lenye mtazamo wa kusonga mbele.

Zaidi ya mapenzi yake kewnye sanaa, Hervé amejikita kwenye kubadili mitazamo ya watu kuhusu wahamiaji. “Watu wanaonekana kuamini kwamba wahamiaji wanakuja tu kuchukua au kubeba, lakini nataka niwaoneshe kuwa pia tuna uwezo wa kuchangia kwenye maendeleo ya kiuchumi na kijamii ya nchia ambayo inatukaribisha,” anasema. 

Chad ni nyumbani kwangu sasa

Licha ya changamoto, na ijapokuwa fursa za kurejea nyumbani Côte d'Ivoire au kwenda mataifa mengine zimefunguka, Hervé ameamua kubaki Chad.  

Kwa kipindi alichokuwemo nchini humo, kupitia kupenda sanaa ya kudansi, uvumilivu na ustahimilifu , Hervé amekua na kuipenda Chad ambayo sasa ndio anaita nyumbani. 

“Nyumbani tuna msemo ya kwamba, unapowasili kwenye Kijiji na wanakupatia kiti uketi na kukupatia kinywaji, unapaswa ubakie hapo kwa sababu chakula kinakuja. Chad inaponipatia kinywaji, nalazimika kubakia kwa sababu kuna mengine mengi yanakuja,” anatamatisha Hervé.