Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Zaidi ya watoto 11,000 wameuawa au kujeruhiwa Yemen: UNICEF

Watoto wakiwa wamesimama katika jengo la darasa la zamani lililoharibiwa vitani katika mji wa Saada, Yemen (Maktaba).
© UNOCHA/Giles Clarke
Watoto wakiwa wamesimama katika jengo la darasa la zamani lililoharibiwa vitani katika mji wa Saada, Yemen (Maktaba).

Zaidi ya watoto 11,000 wameuawa au kujeruhiwa Yemen: UNICEF

Amani na Usalama

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF limesema watoto zaidi ya 11,000 nchini Yemen wameuawa au kujeruhiwa hadi kufikia sasa ikiwa ni sawa na wastani wa watoto 4 kwa siku tangu kushika kasi kwa machafuko nchini humo mwaka 2015. 

Shirika hilo limesema linahofia kwamba idadi kamili ni kubwa zaidi kwani hizi ni takwimu tu za matukio yaliyothibitishwa na Umoja wa Mataifa. 

Kwa mujibu wa UNICEF wakati usuluhishi uliosimamiwa na Umoja wa Mataifa ulisaidia kupunguza kwa kasi kwa mzozo huo, watoto wengine 62 wameuawa au kujeruhiwa kati ya mwisho wa kumalizika kwa makubaliano ya usitishaji uhasama mwanzoni mwa mwezi Oktoba na mwisho wa Novemba.  

Takriban watoto 74 walikuwa miongoni mwa watu 164 waliouawa au kujeruhiwa na mabomu ya kutegwa ardhini na risasi zisizolipuka kati ya mwezi Julai na Septemba 2022 pekee. 

Mtoto huyu pichani mwenye umri wa miezi miwili ni mkazi wa Hajjah, nchini Yemen na ana unyafuzi. Mzozo unaoendelea nchini Yemen unasababisha mamilioni ya watu wawe hatarini kukumbwa na baa la njaa.
WFP/Marco Frattini
Mtoto huyu pichani mwenye umri wa miezi miwili ni mkazi wa Hajjah, nchini Yemen na ana unyafuzi. Mzozo unaoendelea nchini Yemen unasababisha mamilioni ya watu wawe hatarini kukumbwa na baa la njaa.

Takriban miaka minane ya kuendelea kwa machafuko

Takriban miaka minane tangu kuongezeka kwa mzozo huo Yemen, UNICEF inasema zaidi ya watu milioni 23.4, wakiwemo watoto milioni 12.9, wanahitaji msaada wa kibinadamu na ulinzi ikiwa ni sawa na karibu robo tatu ya wakazi wote wa taifa hilo.  

Shirika hilo limeongeza kuwa  watoto wapatao milioni 2.2 nchini Yemen wana utapiamlo mkali, wakiwemo karibu watoto 540,000 walio chini ya umri wa miaka mitano wanaokabiliwa na unyafuzi na wanahaha kuishi. 

Mkurugenzi mtendaji wa UNICEF Catherine Russell, ambaye alizindua ombi la hatua za kibinadamu kwa ajili ya watoto akiwa Yemen wiki iliyopita amesema "Kwa watoto kama vile Yasin mwenye umri wa miezi 7 na mama yake Saba, ambaye nilimtembelea katika hospitali moja huko Aden, maisha yamekuwa mtihani ili kuendelea kuishi. Maelfu ya watoto wamepoteza maisha, mamia ya maelfu zaidi wamesalia katika hatari ya kifo kutokana na magonjwa yanayoweza kuzuilika au njaa. Yasin ni mmoja tu wa watoto wengi sana wenye utapiamlo nchini Yemen. Wote wanahitaji msaada wa haraka kwani huduma za msingi zimesambaratika.”  

Takwimu za UNICEF zinaonyesha kwamba zaidi ya watu milioni 17.8, wakiwemo watoto milioni 9.2, wanakosa huduma za maji salama, usafi wa mazingira na kujiusafi (WASH).  

Na zaidi ya hapo shirika hilo la kuhudumia watoto limesema kwa miaka mingi, mfumo wa afya nchini humo umekuwa dhaifu sana, ni asilimia 50 tu ya vituo vya afya ndivyo vinavyofanya kazi, na kuwaacha karibu watu milioni 22 ikiwa ni pamoja na karibu watoto milioni 10 bila upatikanaji wa kutosha wa huduma za afya. 

Wasichana wadogo baada ya kupokea chanjo yao ya polio wakati wa mzozo nchini Yemen.
© UNICEF/Mahmoud Fahdl
Wasichana wadogo baada ya kupokea chanjo yao ya polio wakati wa mzozo nchini Yemen.

Huduma ya chanjo inakabiliwa na changamoto 

Kwa mujibu wa UNICEF utoaji wa chanjo pia umedorora kitaifa, huku asilimia 28 ya watoto walio chini ya mwaka 1 wakikosa chanjo za muhimu za kawaida.  

Sambamba na ukosefu wa maji salama, na hii inawaweka watoto katika hatari kubwa huku kukiwa na milipuko ya mara kwa mara ya kipindupindu, surua, diphtheria na magonjwa mengine yanayozuilika kwa chanjo limeonya shirika hilo. 

Wakati huo huo, shirika hilo limeongeza kuwa Yemen inakabiliwa na mgogoro mkubwa wa elimu, unaosababisha madhara makubwa ya muda mrefu kwa watoto.  

Kwani watoto milioni mbili hawako shuleni, na idadi hii inaweza kuongezeka hadi watoto milioni 6 wanaopata changamoto ya elimu yao kwani angalau shule moja kati ya nne nchini Yemen imesambaratishwa au kuharibiwa. 

Bi. Russel amesisitiza kwamba "Ili watoto wa Yemen waweze kuwa na nafasi yoyote ya mustakabali mzuri, basi wahusika katika mzozo, jumuiya ya kimataifa na wale wote wenye ushawishi lazima wahakikishe wanalindwa na kuungwa mkono. Hiyo inajumuisha watoto kama Mansour, ambaye nilikutana naye katika kituo cha urekebishaji na viungo bandia kinachoungwa mkono na UNICEF. Mguu wake ulikatwa kwenye goti baada ya kupigwa risasi. Hakuna mtoto anayepaswa kuteseka hivyo. Urejeaji upya na wa haraka wa usitishaji vita itakuwa hatua chanya ya kwanza ambayo ingeruhusu ufikiaji muhimu wa msaada wa kibinadamu. Hatimaye, ni amani endelevu pekee ndioyo itaruhusu familia kujenga upya maisha yao yaliyosambaratika na kuanza kujipanga kwa ajili ya siku zijazo.” 

Msichana mdogo akila banda lenye njugu wakati akitibiwa utapiamlo katika hostpial huko Sa'ana, Yemen.
© UNICEF/Mohammed Huwais
Msichana mdogo akila banda lenye njugu wakati akitibiwa utapiamlo katika hostpial huko Sa'ana, Yemen.

Fedha za kukidhi mahitaji ya kibinadamu 

UNICEF imesema inahitaji haraka dola milioni 484.4 ili kukabiliana na mgogoro wa kibinadamu nchini Yemen kwa mwaka 2023.  

Ukosefu wa ufadhili unaotabirika kwa ajili ya uingiliaji kati wa dharura unaleta changamoto ya kuendelea kwa huduma muhimu, na hivyo kuweka maisha ya watoto na ustawi katika hatari. 

Licha ya changamoto hizo, mwaka 2022 UNICEF iliweza: 

• Kusaidia matibabu ya utapiamlo mkali kwa zaidi ya watoto 260,000 katika vituo 4,584 vya huduma za afya ya msingi na vituo 34 vya kulishia watoto chakula. 

• Iliweza kutoa msaada wa fedha za dharura kwa karibu kaya milioni 1.5 kila robo mwaka na hivyo kunufaisha karibu watu milioni 9. 

• Iliweza kutoa huduma ya maji salama na endelevu ya kunywa kwa watu milioni 4.7 kupitia wigo mpana wa shughuli mbalimbali ikiwa ni pamoja na kutumia lori la kusambaza maji, uwekaji wa vituo vya kusambaza maji, na upanuzi wa mifumo ya usambazaji wa maji kwa kambi za wakimbizi wa ndani.  

UNICEF pia inatoa mafuta kusaidia uzalishaji na usambazaji wa maji safi kwa mashirika 36 ya maji na usafi wa mazingira ya mitaa katika mikoa 15. 

• Pia ilitoa chanjo dhidi ya surua na polio kwa watoto milioni 1.6 ambao wana fursa ndogo ya kupata huduma za afya ya msingi. 

• Iliweza kufikia zaidi ya watoto 254,000 na walezi wao katika maeneo yaliyoathiriwa na migogoro kwa usaidizi wa kisaikolojia na kijamii, na zaidi ya watoto 423,000 na wanajamii kwa elimu ya kuokoa maisha dhidi ya mabomu ya kutegwa ardhini. 

• Pia iliwafikia zaidi ya watu milioni 1.6 wanaoishi katika maeneo ya vijijini na kuwapa huduma za vituo vya afya vya umma. 

• Na iliweza kusaidia kutoa huduma za afya ya mama, mtoto mchanga na huduma zingine za watoto (MNCH) katika hospitali 24 zinazotoa usaidizi wa uendeshaji, pamoja na vifaa na vifaa.  

Aidha, kupitia msaada kwa vituo 4,500 vya mpango wa tiba kwa wagonjwa wa nje (OTP) na timu 288 zinazohamahama, matibabu na huduma za kuzuia utapiamlo ziliongezwa.