Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Baada ya haki yake kutambulika, sasa Elizabeth kutimiza ndoto ya kuwa rubani

Elizabeth Ayebare, (mwenye fulana ya manjano) akiwa darasani na wanafunzi wengine kwenye shule ambayo ilimkubali
OHCHR Video
Elizabeth Ayebare, (mwenye fulana ya manjano) akiwa darasani na wanafunzi wengine kwenye shule ambayo ilimkubali

Baada ya haki yake kutambulika, sasa Elizabeth kutimiza ndoto ya kuwa rubani

Haki za binadamu

Nchini Uganda, harakati za serikali , wadau na Umoja wa Mataifa zimeweza kuleta ahueni na matumaini makubwa kwa watu wenye ualbino na sasa haki zao zinatambuliwa kisheria. 

Miongoni mwa walioanza kunufaika na hatua hiyo ni Elizabeth Ayebare ambaye ndoto yake tangu mdogo ilikuwa siku moja awe rubani. 

Binti huyu mwenye umri wa miaka 14 mwenye ualbino alikumbwa na changamoto kama anavyoelezea mama yake aitwaye Scovia Nsimeta. 

Olive Namutebi, (kulia) Mkurugenzi Mtendaji wa shirikisho la watu wenye ualbino nchini Uganda.
OHCHR Video
Olive Namutebi, (kulia) Mkurugenzi Mtendaji wa shirikisho la watu wenye ualbino nchini Uganda.

Kutaka kujiunga na shule ya msingi ya bweni ilikuwa tatizo 

Bi. Nsimeta anasema, “mwanangu Elizabeth alipozaliwa, alibainika kuwa na hali ya ualbino. Wakati anakua, hakuwa na changamoto nyingi. Alianza shule ya chekechea, akahitimu na kisha akajiunga na shule ya kutwa ya msingi.  Akiwa darasa la 5 akataka kujiunga na shule ya msingi ya bweni. Hapo sasa ndipo changamoto nyingi zikaanza. Msimamizi wa shule alikataa kumsajili shule ya bweni akidai kuwa hawawezi kuhudumia mtoto mwenye ualbino. Walihofia kuwa jambo lolote linaweza kumpata mtoto huyo mwenye ualbino na washindwe kumhudumia.” 

Kamisheni ya Uganda ya Fursa Sawa kwa Wote ilichukua hatua 

Kwa mujibu wa video ya ofisi ya Umoja wa Mataifa ya haki za binadamu, kitendo hicho cha kukataa kumsajili kwa madai kuwa hawawezi kumhudumia, kilitangazwa na Kamisheni ya Uganda ya Fursa Sawa kwa Wote kama ubaguzi na ukiukwaji wa haki za binadamu. 

Joel Cox Ojuko ni Kamishna wa Tume hiyo na anafafanua akisema mamlaka ya shule ilikiri kosa. Halikadhalika ilikubalika kuwa huyu mtoto alipata kiwewe na aliathirika kisaikolojia. Na kutokana na hilo alilipwa fidia ya kifedha. 

Baada ya hapo, Elizabeth aliandikishwa katika shule mpya, na katika video anaonekana amevalia sare ya shule ya fulana ya manjano na sketi nyeusi na kisha anafunguka akisema“watoto wenye ualbino hawapaswi kutengwa. Wanapaswa kuhudumiwa kama watoto wengine. “ 

Serikali ya Uganda katika sheria iliyopitishwa mwaka 2020 inatambua ualbino kuwa ni ulemavu, suala ambalo harakati zake zilihusisha pia Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya haki za binadamu. Ofisi hiyo pia inahusisha wadau wengine katika kutatua suala la hadhi ya ulemavu.  

Scovia Nsimeta, mama mzazi wa mtoto Elizabeth Ayebare
OHCHR Video
Scovia Nsimeta, mama mzazi wa mtoto Elizabeth Ayebare

OHCHR inasaidia jamii kuondokana na fikra potofu kuhusu  ualbino 

Robert Kotchani ni Mwakilishi wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Haki za binadamu nchini Uganda na anasema, “tunafanya uchechemuzi wa utambuzi na ujumuishaji kwa mujibu wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Haki za watu wenye ulemavu, CRPD na hususan kwa watu wenye ualbino kuwajengea uwezo ili wasongeshe haki zao, kwa ubia na watu wengine. Kuwapatia mfano mafuta ya kupaka kwenye ngozi kuzuia jua, na pia kuelimisha watu  kuhusu watu wenye  ualbino kama njia ya kuzielewa na kuzitokomeza fikra potofu kuhusu watu wenye ualbino na vile vile kuhakikisha haki zao kuhusu afya zinaheshimiwa. “ 

Sasa nuru inazidi kuangazia watu wenye ualbino nchini Uganda na Olive Namutebi, Mkurugenzi wa chama cha watu wenye ualbino Uganda anasema sheria iliyopitishwa Uganda ni hatua ya kihistoria na inapaswa kushangiliwa, na zaidi ya yote, “leo tunafurahia kwamba na sisi ni sehemu ya sheria kuhusu watu wenye ulemavu. Haikupatikana kwa urahisi, ni kwa kupitia wadau kama Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya haki za binadamu na wengine kama Kamisheni ya Uganda ya FUrsa Sawa kwa Wote na wengine wengi. Kupitia wao, tumeona milango inafunguka. Serikali imeridhia kama nyaraka yake yenyewe. Kwa hiyo kwetu sisi tunatambua kuwa serikali itakuwa na mipango kuhusu sisi, hiyo ni hatua kubwa sana kwetu.” 

Na video inamalizikia mtoto Elizabeth akiwa anabembea huku akitabasamu akiwa na matumaini kuwa sasa ndoto yake ya kuwa rubani itatimia.