Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Umoja wa Mataifa walaani mauaji ya raia nchini Mali

Walinda amani wakifanya doria katika mkoa wa Menaka nchini Mali eneo ambalo kuna makundi ya magaidi
MINUSMA/Gema Cortes
Walinda amani wakifanya doria katika mkoa wa Menaka nchini Mali eneo ambalo kuna makundi ya magaidi

Umoja wa Mataifa walaani mauaji ya raia nchini Mali

Amani na Usalama

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amelaani vikali shambulio lililofanywa dhidi ya raia tarehe 3 Disemba karibu na kijiji cha Songho katikati mwa nchini Mali, ambako takriban watu 30 waliuawa na wengine kadhaa kujeruhiwa. 

Taarifa iliyotolewa leo kutoka jijini New York, Marekani inasema Katibu Mkuu ametuma salamu za rambirambi kwa familia zilizofikwa na msiba, na anawatakia nafuu ya haraka majeruhi. 

Tayari kikosi cha Umoja wa Mataifa cha Kulinda amani nchini Mali -MINUSMA kimetuma askari wake katika eneo hilo.

“Mashambulizi hayo ya makusudi dhidi ya raia yanajumuisha ukiukwaji mkubwa wa sheria za kimataifa za haki za binadamu na sheria za kimataifa za kibinadamu. MINUSMA iko tayari kusaidia mamlaka ya Mali katika kuwafikisha wahusika wa uhalifu huu mbele ya sheria.” Amesema Guterres 
  
Katibu Mkuu anasisitiza kwamba Umoja wa Mataifa unaendelea kuunga mkono, na kuwa na mshikamano na watu, serikali ya Mali, pamoja na kuimarisha uwezo wa MINUSMA kulinda raia katikati mwa nchi ya Mali na kuunga mkono mkakati unaoongozwa na Serikali wa kuleta utulivu katika eneo hilo.