Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ushirikiano wa kimataifa ingawa ni jawabu, bado ni dhaifu

Naibu Katibu Mkuu wa UN Amina J. Mohammed akitembelea banda la UN kwenye maonesho ya Dubai, Dubai Expo 2020 huko Falme za Kiarabu
Dubai 2020 Expo
Naibu Katibu Mkuu wa UN Amina J. Mohammed akitembelea banda la UN kwenye maonesho ya Dubai, Dubai Expo 2020 huko Falme za Kiarabu

Ushirikiano wa kimataifa ingawa ni jawabu, bado ni dhaifu

Masuala ya UM

Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Amina J. Mohammed amesema licha ya ushirikiano wa kimataifa kusalia kuwa njia pekee ya kutatua changamoto zinazokabili dunia, bado dunia inahaha kusaka njia bora zaidi ya kutekeleza ushirikiano huo wa kimataifa kivitendo.

 

Ametoa kauli hiyo huko Dubai, Falme za Kiarabu wakati wa maadhimisho ya siku ya Umoja wa Mataifa, maadhimisho yaliyofanyika kwenye maonesho makuu ya Dubai Expo2020 yakileta pamoja nchi mbalimbali wanachama wa Umoja huo.

Banda hili katika maonesho ya Dubai, Dubai Expo 2020 limepatiwa jina banda la fursa. Kila jambo linawezekana.
Expo 2020 Dubai/Suneesh Sudhakaran
Banda hili katika maonesho ya Dubai, Dubai Expo 2020 limepatiwa jina banda la fursa. Kila jambo linawezekana.

Bi. Mohammed amesema kusuasua kwa ushirikiano wa kimataifa kivitendo ni dhahiri kwa kuwa “katika kipindi cha miezi sita cha janga la ugonjwa wa Corona au coronavirus">COVID-19, ushirikiano baina ya wanasayansi wa ngazi ya juu ulimwenguni uliwezesha kutengenezwa kwa chanjo dhidi ya coronavirus">COVID-19, na ushirikiano wa kimataifa ulifanikisha kuundwa kwa jukwaa la COVAX la kusaka na kusambaza chanjo duniani kote.”

Hata hivyo amesema leo hii “bado tunahaha kusaka rasilimali na ushirikiano unaohitajika kuhakikisha kuna uwiano wa mgao wa chanjo hizo na vile vile kujenga njia mpya ya kuibuka kutoka janga la Corona, njia ambayo itakuwa bora zaidi kuliko awali.”

Bado kuna mengi ya kufanya

Naibu Katibu Mkuu amegusia pia mkataba wa Paris wa mabadiliko ya tabianchi uliopitishwa mwaka 2015, sambamba na Ajenda 2030 kwa ajili ya maendeleo endelevu akisema vilipitishwa ili kukabili janga la tabianchi na umaskini ifikapo mwaka 2030.

Lakini amesema bado kuna mahangaiko ya kutafsiri nyaraka hizo kivitendo zaidi na pia hakuna utashi wa kutosha kutekeleza ahadi za kitaifa na kimataifa ikiwemo kutoa fedha za kuwezesha nchi kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

Amesema ingawa dunia ina mbinu zote, pamoja na ufahamu na majukwaa ya kuzuia mizozo,  bado dunia inaendelea kukumbwa na majanga makubwa zaidi ya kibinadamu kuwahi kutokea baada ya Vita Kuu ya Pili ya Dunia.

Bi. Mohammed amesema hali ya sasa ni kiashiria dhahiri kuwa bado kuna safari ndefu, ushirikiano wa kimataifa na Umoja wa Mataifa vimetoka mbali lakini bado safari ni ndefu.

Naibu Katibu Mkuu wa UN Amina J. Mohammed akihutubia hii leo huko Dubai Falme za kiarabu wakati wa maadhimisho ya siku ya Umoja wa Mataifa.
Sara Shatila
Naibu Katibu Mkuu wa UN Amina J. Mohammed akihutubia hii leo huko Dubai Falme za kiarabu wakati wa maadhimisho ya siku ya Umoja wa Mataifa.

Kuzingatia malengo

Katika maonesho hayo Dubai, nchi 192 zinashiriki ambapo Naibu Katibu Mkuu wa UN amesema ni fursa ya kipekee kuadhimisha miaka 76 ya Umoja wa Mataifa ya kusongesha ushirikiano wa kimataifa kwa misingi ya Katiba ya Umoja wa Mataifa.

“Msisitizo wa Expo 2020 kuhusu uendelevu na kuunganisha fikra ili kubadili mustakabali wa dunia ni jambo ambalo limejikita katika Ajenda Yetu ya Pamoja, dira ya kuhakikisha ushirikiano wa kimataifa unatoa hakikisho la sisi kama wanafamilia moja tunavuka pamoja,” amesema Bi. Mohammed

Ni kwa kuzingatia kuwa hivi sasa kuna janga la kutoaminiana na ukosefu wa hatua za pamoja, Bi. Mohammed akasema kuna umuhimu wa kuwa na ushirikiano wa kimataifa wa dhati, tuingie upya mkataba wa kijamii, tuimarishe mshikamano na uwekezaji thabiti kwa vijana huku malengo ya maendeleo endelevu, SDGs yakiwa ndio msingi.

“Ni kwa ujumuishi tu ndio tunaweza kuingia upya mkataba wa kijamii na kujenga tena imani. Na hii itawezekana pindi wanawake na vijana wakiwa kitovu cha mipango yetu,” amesisitiza.

Tushirikiane tujenge pamoja amani

Katika maonesho hayo hii leo kwaya ya vijana ya Falme za Kiarabu ilitumbuiza wimbo mahsusi kwa Umoja wa Mataifa, wimbo uliotungwa miaka 50 iliyopita na mtunzi na mwongoza kwaya mashuhuri Pablo Casals kuadhimisha kazi za Umoja wa Mataifa tarehe 24  mwezi Oktobwa maka 1971.

Akizungumza katika maonesho hayo, Kamishna Mkuu wa UN katika Expo 2020 Maher Nasser amesema “uwepo wetu hapa unatoa fursa ya kujenga uelewa kuhusu SDGs, na umuhimu wa vitendo vya kila mtu mmoja moja, mshikamano, matumaini na ushiriki.”

Dubai  Expo 2020 ilianza tarehe 1 Oktoba mwaka huu wa 2021 na itamalizika tarehe 31 mwezi Machi mwaka 2022.