Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu
Mfanyakazi wa usafi akideki kwa kutumia gari maalum kwenye ukumbi wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.

Shoroba za UN zitakuwa kimya,UNGA 75 itafanyika kupitia mtandao, mambo 5 ya kuyafahamu

UN Photo/Manuel Elías
Mfanyakazi wa usafi akideki kwa kutumia gari maalum kwenye ukumbi wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.

Shoroba za UN zitakuwa kimya,UNGA 75 itafanyika kupitia mtandao, mambo 5 ya kuyafahamu

Masuala ya UM

Kikao cha 75 cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UNGA 75) kitaanza rasmi Septemba 15, na mwaka huu kutokana na janga la corona au COVID-19 linaloendelea mjadala utakuwa tofauti kabisa kuwahi kutokea katika historia ya chombo hicho kinachotimiza miaka 75 mwaka huu. 

Mwaka huu hakutakuwa na mpishempishe na vikumbo vilivyozoeleka vya kukutana na marais au watu mashuhuri wa kimataifa kwenye kumbi za Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa New York. 

Hakutakuwa na mashamsham ya misururu ya magari ya marais yanayosindikizwa na ulinzi mkali kwenye barabara ya kwanza, wala watu kusimama ndani ya ukumbi wa Baraza Kuu , kisa kumefurika katika wakati ambao huwa na pilika nyingi kuliko wakati mwingine wowote kwenye kazi za Umoja wa Mataifa, sababu bado dunia inapambana na coronavirus">COVID-19. 

Viongozi wengi hawatakuja uso kwa uso kwenye mjadala wa mwaka huu na mikutano mingi itafanyika kwa njia ya mtandao, lakini hii haimaanishi kwamba magurudumu ya diplomasia ya kimataifa na maendeleo endelevu hayatozunguka kwa kasi ya kawaida. 

Haya ni mambo matanno ya kuyafahamu katika UNGA 75 

Katalin Bogyay, Mwakilishi wa kudumu wa Hungary katika Umoja wa Mataifa, akiandaa kura zake wakati wa uchaguzi kwenye Ukumbi wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.
UN Photo/Eskinder Debebe)
Katalin Bogyay, Mwakilishi wa kudumu wa Hungary katika Umoja wa Mataifa, akiandaa kura zake wakati wa uchaguzi kwenye Ukumbi wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.

 

1)Marais na wakuu wa nchi watarekodi na kutuma hotuba zao 

Kilele cha kikao chochote cha Baraza Kuu jipya la Umoja wa Mataifa huwa ni mjadala wa wazi wa ngazi ya juu (UNGA) ambao utaanza tarehe 22 Septemba wiki moja baada ya kikao kufunguliwa rasmi. 

Tukio hilo la kimataifa huwa ni la kipekee ambapo marais na wakuu wa nchi na serikali au wakati mwingine makamu wao au mawaziri wa mambo ya nje huchukua fursa ya kupanda jukwaani na kuhutubia umma wa kimataifa kuhusu masuala waliyoyachagua. 

Mwaka huu kwa sababu ya janga la COVID-19, viongozi wa dunia hawatokuja Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa, badala yake wamealikwa kutuma video za hotuba zao ambazo wamezirekodi na zitaonyeshwa kama za moja kwa moja kwenye ukumbi wa Baraza Kuu. 

Hotuba hizo zitatambulishwa na mwakilishi wa kila nchi ambaye yuko hapa kwenye Makao Makuu na ambaye atakuwepo moja kwa moja ndani ya ukumbi wa mkutano. 

Hata hivyo kiongozi yeyote wa dunia ana haki ya kuja uso kwa uso kutoa hotuba yake, fursa ambayo angalau Rais mmoja anayetaka kuchaguliwa tena kisiasa mwaka huu ameripotiwa kutaka kuitumia. 

Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa na sehemu ya majengo marefu ya Manhattan, 24 Oktoba 1955
UN Photo.
Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa na sehemu ya majengo marefu ya Manhattan, 24 Oktoba 1955

 

2) Maadhimisho ya miaka 75 

Umoja wa Mataifa ulianzishwa mwaka 1945 na unafanya maadhimisho ya miaka 75 kwa kile ambacho Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amekiita “mjadala wa watu wa muendelezo” ambao unaahidi kuwa ni mkubwa zaidi na utakaowafikia watu wengi zaidi katika mazungumzo ya kimataifa kuwahi kushuhudiwa kuhusu ujenzi wa mustakbali tunaoutaka. 

Tukio litakalofanyika Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa tarehe 21 Septemba ambalo pia litakuwepo mtandaoni litalenga “kuchagiza upya msaada kwa ajili ya mshikamano wa kimataifa, suala ambalo wengi wanaamini sasa ni laharura kuliko wakati mwingine wowote , wakati dunia ikipambana na janga la CVID-19". 

Inarajiwa kwamba Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa atatoa hotuba yake moja kwa moja wakati wa kikao cha ngazi ya juu cha kuadhimisha miaka 75 ndani ya ukimbi wa Baraza Kuu. 

Mwanamke akivuna maharage katika shamba la ushirika nchini Kenya
© FAO/Fredrik Lerneryd
Mwanamke akivuna maharage katika shamba la ushirika nchini Kenya

 

3) Malengo ya Maedeleo Endelevu 

Malengo ya maendeleo endelevu au SDGs, ambayo ni malengo 17 yaliyokubalika kimataifa kupunguza umasikini na kudumisha amani, huku yailinda sayari dunia, yamesalia kuwa kipaumbele cha ajenda za Umoja wa Mataifa kwa mwaka 2020, huku wengi akiwemo Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa wakisema janga la COVID-19 limezidi kutia msisitizo ni kwa nini malengo hayo ni muhimu sana. 

Wakati wa kikao cha 75 cha Baraza Kuu malengo ya SDG yatamulikwa katika kile kinachoelezwa kuwa ni matangazo ya aina yake ya dakika 30, yaliyoandaliwa na mwandishi na muongoza filamu, ambaye pia ni mpiga debe mkubwa wa masuala ya SDGs Richard Curts, matangazo ambayo yawaipeleka hadhira kote duniani ili kutathimini ulimwengu na nyakati tunazoishi, changamoto zinazoikabili dunia yetu na hatua ambazo zinaweza kubadili dunia yetu ifikapo mwaka 2030 ambao inatarajiwa malengo ya SDGs yatawa metimizwa. 

Wakati huohuo kitengo cha hatua kwa ajili ya SDGs ambacho kila mwaka wakati wa kikao cha Baraza Kuu hutumika kama eneo la kuchagiza malengo hayo mwaka huu kinahamishiwa mtandaoni kikiwaleta pamoja viongozi , wachagizaji, na Umoja wa Mataifa kwa kushirikiana na matangazo ya mitandao ya kijamii ya Al Jeera katika mfululizo wa majadiliano kuhusu SDGs. 

Sehemu ya matumbawe makubwa duniani katika eneo lililoko nchini Australia.
Coral Reef Image Bank/Matt Curno
Sehemu ya matumbawe makubwa duniani katika eneo lililoko nchini Australia.

 

4)Upotevu mkubwa wa bayoanuwai 

Bayoanuwai ya dunia na viumbe vyake inapungua katika kiwango ambacho Umoja wa Mataifa umeonya kwamba ni kisichotarajiwa. 

Viumbe zaidi ya milioni 1 viko katika hatari ya kutoweka, ekari zaidi ya bilioni 2 zimemomonyoka hivi sasa na asilimia 66 ya bahari , asilimia 50 ya matumbawe na asilimia 85 ya maeneo oevu vimeharabiwa kwa kiasia kikubwa na shughuli za binadamu. 

Mkutano mkubwa wa kujadili jinsi gani ya kubadili mwenndo huo wa kasi wa kupotea kwa mazingira asililia na jinsi gani yanaathiri maisha ya watu utafanyika mwaka huu mjini Kunming China lakini sasa umeahirishwa hadi Mei 2021.

Wakati huohuo kutakuwa na siku ya mikutano kwa njia ya mtandao ambayo itafanyika chini ya mwamvuli wa Baraza Kuu tarehe 30 Septemba.

Mwanamke akiendesha kigari cha kunyanyua mizigo mizito katika kiwanda nchini Jordan
UNDP/Sumaya Agha
Mwanamke akiendesha kigari cha kunyanyua mizigo mizito katika kiwanda nchini Jordan

 

5)Usawa wa kijinsia:miaka 25 baada ya Beijing

Hatua zilizopigwa katika kusongesha mbele usawa wa kijinsia na haki za wanawake zimeathirika vibaya na janga la COVID-19, kwani wanawake na wasichana ndio wanaoathirika zaidi kijamii na kiuchumi kutokana na janga hilo kwa mujibu wa Katibu Mkuu Antonio Guterres.

Mnamo tarehe 31 Oktoba suala hili na mengine yanayohusu usawa wa kijinsia na uwezeshaji wanawake yatajadiliwa kwenye Umoja wa Mataifa kwa minajili ya kuadhimisha miaka 25 na mkataba wa kimataifa wa kuchukua hatua uliojulikana kama jukwaa la Beijing kwa ajili ya hatua ambalo hadi sasa linachukuliwa kuwa mpango bora wa kusongesha mbele haki za wanawake na wasichana.

Siku ya malipo: hapo tarehe 18 Septemba ni siku ambayo itajikita katika kulinganisha malipo baina ya wanaumme na wanawake.

Na kwa wananchi wa New York ambao hukumbana na mitaa yao kufungwa, polisi kutapakaa kila kona wakati wa vikao vya Baraza Kuu mwezi Septemba kila mwaka, mwaka huu bila shaka licha ya changamoto lukuki zilizoletwa na janga la COVID-19 ambazo zinajumuisha kupotea kwa mabilioni ya dola kutoka kwa wageni na watalii, watafurahia hali ya utulivu.

Jengo la Empire State likiwa limewasha taa nyekundu katika kuwaenzi watu wa kwanza kutoa huduma wakati wa mlipuko wa janga la  COVID-19 mjini New York.
UN Photo/Evan Schneider
Jengo la Empire State likiwa limewasha taa nyekundu katika kuwaenzi watu wa kwanza kutoa huduma wakati wa mlipuko wa janga la COVID-19 mjini New York.