Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Huduma za afya zimevurugwa katika asilimia 90 ya nchi wakati wa COVID-19:WHO 

Washauri wakisaikolojia  wanazungumza na mama wa mtoto wa miaka tisa katika Kituo cha Tiba ya Antiretroviral Therapy (ART) katika hospitali ya Mumbai, India.
© UNICEF/Hiraj Singh
Washauri wakisaikolojia wanazungumza na mama wa mtoto wa miaka tisa katika Kituo cha Tiba ya Antiretroviral Therapy (ART) katika hospitali ya Mumbai, India.

Huduma za afya zimevurugwa katika asilimia 90 ya nchi wakati wa COVID-19:WHO 

Afya

Shirika la afya la Umoja wa Mataifa WHO, leo limechapisha utafiti wake wa kwanza wa athari za janga la corona au COVID-19 kwa mifumo ya afya duniani.

Katika utafiti huo uliofanyika na takwimu kukusanywa katika nchi 105 duniani tangu mwezi Machi hadi Juni mwaka huu wa 2020, unaonyesha kuwa takriban asilimia 90 ya nchi hizo huduma zake za afya zimekabiliwa na changamoto huku nchi za kipato cha chini na cha wastani zikiarifu matatizo makubwa zaidi. 

 

Utafiti unasema nchi nyingi zimesema utaratibu na huduma maalum zimesitishwa huku huduma za muhimu kama za upimaji wa saratani na matibabu ya VVU yamekuwa katika hatari kubwa ya kuingiliwa katika nchi masikini. 

Akizungumzia utafiti huo mkurugenzi mkuu wa WHO Dkt. Tedros Adhanom Ghebreyesus amesema, “utafiti huu unaweka wazi nyufa zilizopo katika mifumo yetu ya afya , lakini pia unatumika kutujuza mikakati mipya ya kuboresha utoaji wa huduma za afya wakati wa majanga na zaidi. COVID-19 inapaswa kuwa somo la kujifunza kwa nchi zote ambazo afya sio suala la msingi, ni lazima tujiandae vyema kwa majanga ya ghafla lakini pia kuendelea kuwekeza katika mifumo ya afya ambayo itaweza kutimiza mahitaji ya watu wakati wote wa maisha yao.” 

 

Kwa mujibu wa utafiti huo miongoni mwa huduma  zilizoathirika zaidi ni 25 ikiwemo za chanjo za kawaida, huduma za nje za kuwatembelea wagonjwa, huduma za kwenye vituo, huduma za magonjwa yasiyo ya kuambukiza, za uzazi wa mpango, za matibabu ya afya ya akili, za saratani, matibabu ya malaria, kifua kikuu au TB, dawa za kupunguza makali ya VVU, huduma za meno  na nyinginezo.