Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Zimbabwe iko katika hatihati ya janga la njaa:WFP

Ukame nchini Zimbabwe umesababisha wakulima kushindwa kulima chakula toshelezi. Hali kama hii pia imeshuhudiwa katika nchi nyingine ya kusini mwa Afrika, Zambia.
WFP/Tatenda Macheka
Ukame nchini Zimbabwe umesababisha wakulima kushindwa kulima chakula toshelezi. Hali kama hii pia imeshuhudiwa katika nchi nyingine ya kusini mwa Afrika, Zambia.

Zimbabwe iko katika hatihati ya janga la njaa:WFP

Tabianchi na mazingira

Zimbabwe iko katika hati hati ya janga la njaa limesema shirika la Umoja wa Mataifa la mpango wa chakula duniani WFP likiongeza kuwa karibu watu milioni 8 sawa na nusu ya watu wote wa nchi hiyo hawana uhakika wa chakula. 

Kufuatia hali hiyo WFP sasa inatoa wito wa uwekezaji wa haraka ili kuongeza mara mbili idadi ya watu inayowasaidia ikisema mamilioni ya Wazimbabwe wamelazimika kutumbukia katika zhma ya njaa kutokana na ukame wa muda mrefu na mgogoro wa kiuchumi  na msaada usipopatikana haraka shirika hilo limeonya hali itakuwa mbaya zaidi.

WFP inataka kuongeza idadi ya watu wanaopokea msaada mara mbili hadi kufikia milioni 4.1 na ili kuweza kufanya hivyo inahitaji zaidi ya dola milioni 200 katika nusu ya kwanza ya mwaka 2020 pekee. Niels Balzer ni naibu mkurugenzi wa WFP nchini Zimbabwe anasema

"Mwaka 2019 umekuwa mgumu sana kwa Wazimbabwe wote . Tumeona ni kutokana na sababu au mchanganyiko wa sababu ukiwemo mdororo wa kiuchumi, mabadiliko ya tabianchi, na ukame mkali ambao umesababisha zaidi ya watu milioni 8 kutokuwa na uhakika wa chakula. Kama WFP tunaangalia kuongeza hatua zetu kwa wiki chache zijazo ili kuweza kuwafikia takriban wat umara mbili ya tulivyokuwa tumepanga.”

Amesisitiza kuwa jinsi mambo yalivyo sasa tutaishiwa kabisa chakula mwishoni mwa Februari tukigongana na kilele cha msimu wa njaa wakati mahitaji ndio huwa makubwa zaidi. Ahadi thabiti zinahitajika haraka kwani inaweza kuchukua hadi miezi mitatu kwa fedha zilizoahidiwa kugeuzwa chakula kwa wahitaji mezani.

Ameongeza kuwa miaka mingi ya ukame imepunguza uzalishaji wa chakula Zimbabwe kwa kiasi kikubwa nchi ambayo awali ilijulikana na kapu la mkate barani Afrika. Mavuno ya mahindi yalipungua kwa asilimia 50 mwaka 2018, na kufikia Agosti 2019 WFP ililazimika kuzindua msaada wa dharura wa msimu wa muambo ili kukidhi mahitaji yaliyoongezeka  mapema kuliko ilivyotarajiwa.

Msimu huu kwa mujibu wa WFP mvua zimechelewa tena na hazitoshi kwa kilimo huku mbegu nyingi zilizopandwa hazijaoota hivyo  utabiri unaonyesha kwamba kutakuwa na muendelezo wa jua kali na ukame, vikiashiria mavuno hafifu mwezi Aprili na kuyaweka maisha ya mamilioni ya watu na mifugo katika hatari kubwa.