Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Rwanda na DRC wachukua hatua kuimarisha uhusiano mpakani

Mhudumu wa afya akipima joto la mwananchi kwenye eneo la mpakani mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC na Uganda. Wahudumu wa afya kwenye kituo hiki wamekuwa wakichukua vipimo kubaini iwapo wananchi wana Ebola au la. (12 Feb 2019)
UNICEF/Jimmy Adriko
Mhudumu wa afya akipima joto la mwananchi kwenye eneo la mpakani mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC na Uganda. Wahudumu wa afya kwenye kituo hiki wamekuwa wakichukua vipimo kubaini iwapo wananchi wana Ebola au la. (12 Feb 2019)

Rwanda na DRC wachukua hatua kuimarisha uhusiano mpakani

Afya

Serikali za Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC zimekuwa na mazungumzo huko Goma, jimboni Kivu Kaskazini kuona ni jinsi gani ya kuimarisha uhusiano wao mpakani na kuleta mazingira bora kwa mataifa yote ya ukanda wa Maziwa Makuu. Sifa Magoro wa Radio Okapi ya ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini DRC, ana taarifa zaidi.

Wakikusudia kujiunga pamoja katika hatua za kuepuka kusambazwa kwa magonjwa na hata kulinda usalama wa wakazi kwenye mipaka, viongozi wa Rwanda na DRC wamezungumzia kutamani kuboresha shughuli za uchumi kwa faida za wananchi wa nchi zote za maziwa makuu.

Akifafanua zaidi, Waziri wa Afya wa DRC, Pierre Kangugya amesema kuwa, “nadhani ni kwa fainda ya nchi zote jirani na DRC. Tena sisi na Rwanda katika mazungumzo tuliyokuwa nayo, tumesisitiza kuwa ni kwa faida ya wananchi wote wa maeneo ya Maziwa Makuu kama vile wale wanaotoka Sudan Kusini, Uganda, Rwanda, Burundi na Tanzania. Ni nchi zote zilizo katika hatari ya kuambukizwa na magonjwa kutoka DRC.”

Kutokana na mazungumzo hayo, wataalamu mbalimbali wa Rwanda watakwenda DRC, ili kuimarisha ushirikiano huo, huku wajumbe wa DRC na washirika wao wa kimataifa walikuwa na mazungumzo kwa siku 3 huko Goma jimboni Kivu Kaskazini.

Ziara hiyo imefanyika siku chache baada ya sintofahamu iliyotokea kwenye mpaka wa Rwanda na DRC huku ikidaiwa kuwa Rwanda imefunga mpaka kwa hofu ya Ebola, taarifa ambazo baadaye zilikanushwa.