Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Msumbiji ni mwathirika wa mabadiliko ya tabianchi inastahili msaada.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres akipokea maua kutoka kwa binti mdogo alipowasili mjini Maputo Msumbiji leo 11 Julai 2019
UN Photo/Eskinder Debebe)
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres akipokea maua kutoka kwa binti mdogo alipowasili mjini Maputo Msumbiji leo 11 Julai 2019

Msumbiji ni mwathirika wa mabadiliko ya tabianchi inastahili msaada.

Tabianchi na mazingira

Katibu Mkuu wa Umoja wa Umoja wa Mataifa António Guterres, amewasili nchini Msumbiji hii leo kwa ziara ya siku mbili: mjini Maputo amekutana na rais na maafisa wengine wa serikali kujadili hali ya nchi baada ya kimbunga Idai na Keneth. Kesho Ijumaa, Bwana Guterres anatarajiwa kuzuru maeneo yaliyoathirika kukutana na manusura.

Mara baada ya kuwasiri hii leo, Guterres amesema, “Msumbiji ina kila haki ya kuomba msaada kutoka kwa jumuiya ya kimataifa baada ya vimbunga viwili vikali vilivyoipiga nchi mwezi Machin a Aprili mwaka huu wa 2019.”

Katibu Mkuu Guterres amekutana na wanahabari mara baada ya kukutana na Rais Filipe Jasinto Nyusi na maafisa wengine wa serikali. Vimbunga hivvo viwili vilisababisha vifo vya takribani watu 648 na kuwaathiri watu milioni 2.2.

Akizungumza kwa lugha ya kireno, Bwana Guterres ameongeza kusema, “Msumbiji ni kama haichangii chochote katika ongezeko la joto la dunia lakini iko mstari wa mbele katika waathirika wa ongezeko la joto duniani.Hii inaipa Msumbiji haki ya kutaka ushirikiano madhubuti na msaada wa kina kutoka kwa jumuiya ya kimataifa, kwa pande zote mbili yaani kusaidia waliopatwa na kiwewe kutokana na majanga hayo na pia kuandaa urekebishaji wa miundombinu na kujiandaa kwa ajili ya hali ya siku za usoni.”

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataidfa Antonio Guterres akikutana na wanaharakati wa kumbana na ubaguzi na unyanyapaa dhidi wa watu wenye Ualbino mjini Maputo Msumbiji
UN Photo/Eskinder Debebe)
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataidfa Antonio Guterres akikutana na wanaharakati wa kumbana na ubaguzi na unyanyapaa dhidi wa watu wenye Ualbino mjini Maputo Msumbiji

Hatua

Akirejelea uharibifu uliosababishwa na kimbunga Idai na Kenneth, Guterres amesema, “mashirika ya Umoja wa Mataifa yaliichukulia Msumbiji kuwa ya kipaumbele cha kwanza tangu mwanzo na waliandaa njia nzuri waliyokuwa nayo kuwa na watu wa Msumbiji.”

Aidha Guterres amesifu kile alichokiita “uhamasishaji mzuri sana wa serikali na pia ujasiri wa ajabu wa watu wa Msumbiji,” na pia akaziita juhudi za miezi minne ya mwisho “hatua za ajabu.”

Naye Rais Nyusi katika hotuba yake amemshukuru Bwana Guterres na Umoja wa Mataifa akisema “ulikuwa mtu wa kwanza na taasisi ya kwanza kuungana na watu wa Msumbiji” baada ya janga la asili. Ameeleza kazi za mashirika kadhaa ya Umoja wa Mataifa na akaongeza kuwa “walifanya kazi ya kuokoa maisha zaidi na kupunguza mateso ya wanamsumbiji.”

Msaada

Rais Nyusi pia ameeleza kuhusu baadhi ya misaada ambayo Msumbiji imepokea kuwa imepatikana kutokana na Umoja wa Mataifa na viongozi wake, “ni matokeo ya maombi ya Kabu Mkuu aliyoyafanya yeye mwenyewe binafsi lakini pia kama taasisi.”

Guterres ameeleza kuhusu ombi la dola milioni 280 la Umoja wa Mataifa la kusaidia Msumbiji akisema, “liko mbali sana kufikiwa.” Amekumbuka pia kuwa katika mkutano wa wachangiaji mnamo mwezi Mei katika mji wa Beira, serikali ya Msumbiji iliomba bilioni 3.2 za Marekani ili kufadhili juhudi za ukarabati wa miundombinu na ikapokea ahadi ya dola bilioni 1.2. 

Ni wazi mengi zaidi yatahitajika,” Bwana Guterres ameeleza wakati akikisisitiza umuhimu wa utekelezaji wa haraka wa msaada ulioahidiwa.”

“Hatutakiwi kusaidia tu, bali kusaidia katika muda unaofaa,” ameongeza.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres akiwa na Rais filipe Nyusi wa Msumbiji
UN Photo/Eskinder Debebe)
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres akiwa na Rais filipe Nyusi wa Msumbiji

Ziara

Baada tu ya kutua mjini Maputo hii leo kwa ziara ya siku mbili, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amepokelewa kwa gwaride la kijeshi, ngoma za asili na akakabidhiwa maua na kundi la watoto. Ameshiriki pia katika mkutano kuhusu kupambana na ubaguzi dhidi ya watu wenye ualbino. Amesikiliza moja kwa moja kutoka kwa wataalamu kadhaa na watoto wenye ualbino kuhusiana nan a masuala wanayotakiwa kukabiliana nayo.

Ijumaa hii, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa atazuru mji wa pili kwa ukubwa nchini Msumbiji, Beira ambao uliathirika sana na kimbunga Idai. Umoja wa Mataifa unakadiria kuwa asilimia tisini ya miundombinu yote ya Beira iliharibiwa. 

Huko Beira, Guterres atakutana na mamlaka za mji huo, atatembelea moja ya shule zilizoathirika, atafanya mkutano na watu wenye ulemavu, kundi la wanawake na pia atatembelea kambi ya wasio na makazi.

Bwana Guterres amesema kuitembelea Msumbiji ni suala linalogusa Moyo na mara zote ambazo ametembelea nchi hiyo amepokelewa kwa urafiki mkubwa na bashasha, “ mara zote ninajisikia nyumbani, katikati ya marafiki, ninaweza hata kusema katikati mwa ndugu zangu.”

Bwana Guterres amwwahi kuitembelea Msumbiji alipokuwa Waziri Mkuu wa Ureno nchi ambayo ilipata kuwa wakoloni wa Msumbiji na pia alitembelea nchi hiyo alipokuwa rais wa Socialist International kabla hajarejea akiwa Kamishina mkuu wa UNHCR na hivi sasa kama Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa.