Raisi Barack Obama wa Marekani alipohutubia Baraza Kuu la UM aliwaambia wajumbe wa kimataifa kwamba taifa lake lipo tayari kuanzisha mlango mpya kwenye uhusiano wa kimataifa na nchi wanachama. Aliyataka mataifa yajihusishe kwenye awamu yenye lengo la kukidhi masilahi ya pamoja ya umma wote wa dunia, na kwenye mazingira ambapo mataifa yatahishimiana. Aliutaka ulimwengu kuongeza juhudi zao, mara mbili zaidi, zitakazohakikisha UM utatumiwa kama ni kipengele muhimu cha kuendeleza masilahi ya pamoja ya umma wote wa ulimwengu. Alisisitiza kwamba ukubwa wa matatizo yalioukabili ulimwengu sasa hivi, bila shaka yanahitajia mchango wa Mataifa Wanachama yote, mchango utakaoipa taasisi ya UM maana hakika ya jina lake, kama ni taasisi inayosimamia masilahi ya Mataifa Yalioungana. Alisema mwelekeo huo ndio Marekani ungelipendelea kuuona unatumiwa kuendeleza uhusiano wa kimataifa katika siku za baadaye - hali itakayokuwa ya amani na yenye ustawi, ambayo walimwengu wote wanaweza kuifikia, tukitambua kwamba kila taifa lina haki na dhamana ya kutekeleza majukumu hayo. Makubaliano haya, alitilia mkazo, ndio yenye uwezo wa kuyafikia malengo yanayoridhisha katika uhusiano wa kimataifa.