Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Chuja:

Habari Mpya

Mapigano Usomali kuwalazimisha maelfu ya raia kuhajiri Yemen kutafuta hifadhi

Shirika la UM juu ya Huduma za Wahamiaji (UNHCR) kwenye taarifa iliyoiwasilisha Geneva, Ijumanne asubuhi, ilieleza mapigano yenye kuendelea hivi sasa kwenye mji wa Mogadishu, na katika eneo la kati la Usomali, yamesababisha maelfu ya raia kuhatarisha maisha kwa kuhama makwao, na kuamua kufanya safari hatari ya kuvuka Ghuba ya Aden, kuelekea Yemen kuomba hifadhi.

Hapa na pale

Shirika la Vikosi vya Mchanganyiko vya UM-UA kwa Darfur (UNAMID) liomeripoti Kamisheni ya Uchaguzi wa Taifa Sudan imewaarifu ya kuwa imeshakamilisha kuweka mipaka ya maeneo ya kupiga kura kwenye uchaguzi mkuu ujao unaotarajiwa kufanyika mwezi Aprili 2010. Vile vile Kamisheni ilisema imeshaanzisha kamati tatu zitakazoshughulikia upigaji kura kwenye majimbo yote matatu ya Darfur. Taarifa ya Kamisheni ya Uchaguzi wa Taifa Sudan pia ilisema makundi ya kiraia yataruhusiwa kuendeleza shughuli za kuhamasisha wapiga kura kutekeleza haki zao za kimsingi, bila ya kuingiliwa kati na serikali, hususan kutoka zile idara za usalama na ulinzi au ile Kamisheni juu ya Misaada ya Kiutu, na walihakikishiwa masuala yote yenye mvutano yatapelekwa kusailiwa na Kamisheni ya Uchaguzi.

Hapa na pale

Catherine Bragg, Naibu Mkurugenzi wa UM Kuhusu Huduma za Dharura na KM Msaidizi wa Misaada ya Kiutu ameanza ziara rasmi ya siku tano katika Jamhuri ya Afrika ya Kati (JAK). Ijumatatu alizuru Birao, kaskazini-mashariki ya JAK. Wakati atakapokuwepo JAK, Bragg anatarajiwa kufanya tathmini ya hali ya kiutu ilivyo nchini na kuhakikisha misaada ya kihali itahudumiwa, kwa mfululizo, lile fungu la umma muhitaji wenye kutegemea misaada ya kimataifa kunusuru maisha. Bragg analizuru eneo la Birao sasa hivi mwezi mmoja tu baada ya kuripuka mapigano ya kikabila, ambapo watu waliyanganywa mali, nyumba 600 ziliunguzwa moto na raia 3,700 walilazimika kuhajiri makazi kwa sababu ya vurugu.

Mashirika ya kimataifa yameandaa mradi wa kutoa hadhari za mapema dhidi ya miripuko ya moto

Shirika la UM juu ya Chakula na Kilimo (FAO) likijumuika na Shirika la Ulaya juu ya Anga Nje ya Dunia (ESA), pamoja na Shirika la Marekani Linalosimamia Uchunguzi wa Anga (NASA) yameripoti juu ya umuhimu wa kudhibiti haraka miripuko ya moto ilioshuhudiwa kutukia ulimwenguni katika siku za karibuni, kwenye sehemu mbalimbali za dunia, hasa yale maeneo ya karibu na Bahari ya Mediterranean, kusini ya Jangwa la Sahara, Australia na katika Amerika ya Kaskazini.

Ban ausihi ulimwengu ujirekibishe kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa

KM Ban Ki-moon, kwenye hotuba alioitoa Ulaanbaatar, mji mkuu wa Mongolia Ijumatatu ya leo, kuhusu "Marekibisho ya Kudhibiti Athari za Mabadiliko ya Hali ya Hewa Duniani" alieleza kwamba nchi zilizozungukwa na bara husumbuliwa sana na vizingiti vinavyokwamisha juhudi za kusukuma mbele maendeleo yao, hususan katika kipindi ambacho nchi hizi zisio na pwani huwa zinaathirika pia kutokana na mabadiliko ya hali ya hewa,

Hapa na pale

Shirika la UM juu ya Hifadhi ya Mazingira (UNEP) limetoa mwito wenye kuyahimiza Mataifa Wanachama kutumia zile taratibu za kilimo zitakazotunza na kuimarisha, kwa muda mrefu, ardhi na mazingira, taratibu zitakazojulikana kama ‘mazoezi ya kilimo cha kijani\'. Utaratibu huu ukitekelezwa,kwa mujibu wa UNEP, utasaidia kuleta natija kemkem kwa idadi ya umma wa kimataifa unaozidi kukithiri kwa kasi kuu. Utaratibu huu unaashiriwa pia utasaidia kupambana na athari za mabadiliko ya hali ya hewa, kuondosha ummaskini na kukuza uzalishaji wa chakula, nidhamu ambayo inaweza kuwa ndio chanzo cha kupata mbao zisioharibu kilimo kwa wananchi wa mataifa yanayoendelea, baada ya miti kukatwa."

KM ameteua Kamanda Mkuu mpya wa UNAMID kutoka Rwanda

KM amewaariifu wajumbe wa Baraza la Usalama kwamba kutokana na maafikiano na Mwenyekiti wa Kamisheni ya UA, wamemteua Liuteni Jenerali Patrick Nyamvumba wa Rwanda kuwa Kamanda Mkuu mpya wa Vikosi vya Mchanganyiko vya UM-UA kwa Darfur (UNAMID), kuanzia tarehe mosi Septemba, mwaka huu.