Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Chuja:

Habari Mpya

Hapa na Pale

Kwenye tafrija maalumu iliyofanyika katika mji wa Davos, Uswiss Alkhamisi KM wa UM aliadhimisha miaka kumi ya tangu kupitishwa yale Mapatano ya UM juu ya Maadili Mema ya Kibiashara kwa Makampuni ya Kimataifa au UN Global Compact. KM alisema kwenye risala yake kwamba mapatano ya UN Global Compact yanajumuisha mradi mkubwa, unaosarifika, na wa kutia moyo wenye kuonogoza shughuli za kibiashara zinazohishimu haki za binadamu, ajira halali, mazingira bora na kupiga vita karaha ya ulaji rushwa. Makampuni ya kibiashara 6,000 kutoka mataifa 130 ziada ni washiriki wa Mapatano ya UN Global Compact.

UNRWA inakana tetesi zinazodai misaada kwa Ghaza hunyakuliwa na makundi haramu

Christopher Gunness, Msemaji wa Shirika la UM Linalofarajia Misaada ya Kiutu kwa WaFalastina wa Mashariki ya Karibu (UNRWA) ametoa taarifa maalumu yenye kukana zile tetesi zilizoenezwa kwenye vyombo vya habari, zenye kudai ya kwamba misaada ya UM, inayopelekwa kwenye eneo liliokaliwa la WaFalastina la Tarafa ya Ghaza huibiwa au hutekwa nyara [na makundi fulani ya kisiasa].

MONUC itasaidia majeshi ya Rwanda/JKK dhidi ya waasi wa FDLR

Shirika la Ulinzi Amani la UM katika JKK (MONUC) limetoa taarifa yenye kueleza kwamba litatuma msaada wa usafiri na huduma za tiba kwa vikosi vya Rwanda na JKK ambavyo vinashirikiana kupambana na waasi wa KiHutu katika eneo la mashariki ya nchi, na ilisisitiza kwamba vikosi vya MONUC havitoshiriki kabisa kwenye operesheni hizo.

Mada zinazosailiwa katika BU

Wajumbe wa Baraza la Usalama wamekutana Ijumatano, kwenye kikao cha faragha, kushauriana juu ya masuala yanayohusu hali katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo (JKK), Sudan na pia masuala mengine juu ya amani ya kimataifa. ~

Hapa na Pale

Alan Doss, Mjumbe Maalumu wa KM kwa JKK, ameripoti kuridhia rasmi ombi la serikali ya Kongo la kutaka isaidiwe katika kuandaa mipango ya zile operesheni za pamoja za vikosi vya JKK/Rwanda dhidi ya waasi wa KiHutu kutoka Rwanda, waliopo kwenye eneo la mashariki. Uamuzi huu ulitolewa Ijumanne baada ya Doss kuzuru sehemu ya mashariki ya nchi, ambapo alipata fursa ya kutathminia athari za operesheni za vita kwa raia. Shuirika la Ulinzi Amani la UM katika JKK (MONUC) linatarajiwa kupeleka Goma, yalipo makao ya operesheni za vikosi vya JKK/Rwanda, timu ya maofisa wa kijeshi watakaowasiliana na kusaidia kupanga udhibiti bora wa operesheni zao, kwa makusudio ya kuwajumlisha watumishi wa kiraia watakaosimamia kadhia za kiutu kwa umma muhitaji kwenye eneo la uhasama.

Wapiganaji waasi wa Rwanda waliopo JKK wapatiwe fursa ya kurudi makwao, bila kulazimishwa, inasema UM

Alan Doss, Mjumbe Maalumu wa KM kwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo (JKK) ameripotiwa akisema kwamba rai ya kuruhusu Wanyarwanda waliokuwa wakipigana na majeshi ya mgambo nchini Kongo kuzuru makwao na kuchunguza kama hali inafaa kwao kurejea, ni moja ya taratibu ambazo zikitekelezwa kama inavyopasa, zitasaidia kupunguza vurugu na uhasama unaofufuka mara kwa mara kwenye eneo la uhasama Kongo. Mradi huo, alisisitiza Doss, unabashiria “mapatano mema kati ya Serikali za Rwanda na JKK, yalioamua hatua za kuchukuliwa, zilizo salama,” za kuwarejesha makwao wale wapiganaji waliotokea Rwanda ikiwa wapiganaji hawo wataridhia kurejea kwa hiyari.