Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Chuja:

Habari Mpya

KM bado anasubiri idhini ya Sudan juu ya vikosi vya mseto vya UM/AU kwa Darfur

KM Kofi Annan alikuwa na mashauriano na Baraza la Usalama wiki hii kuhusu hali katika Darfur,Sudan. Baada ya mkutano wake huo na Baraza la Usalama aliwaambia waandishi habari wa kimataifa waliopo Makao Makuu kwamba Serekali ya Sudan bado haijamtumia jawabu yao ya kuidhinisha maafikiano ya kimsingi, waliokubaliana pamoja wiki iliopita, ya kupeleka vikosi vya mseto vya UM na AU katika Darfur ambayo yanahitajika kidharura kukomesha uhasama na maafa yaliofumka na kutanda kwenye eneo hilo, na kuathiri vibaya maisha ya malaki ya raia.

Huduma za UM kusaidia mamia elfu ya waathiriwa wa mafuriko Kenya

Mashirika ya UM yanayohusika na miradi ya chakula duniani (WFP), wahamiaji (UNHCR), na pia mfuko wa maendeleo ya watoto (UNICEF) yalijumuika nchini Kenya wiki hii kuongoza operesheni za kugawa misaada ya kiutu kwa mamia elfu ya wahamiaji wa Usomali walioajikuta kunaswa na mafuriko yaliozuka kwenye zile kambi walizokuwa wakiishi kaskazini-mashariki ya Kenya.

Kenya kuchachamaa kutunza mazingira dhidi ya uharibifu wa hali ya hewa

KM wa UM Kofi Annan alipohutubia kikao cha wawakilishi wa Hadhi ya Juu kwenye Mkutano Mkuu juu ya Mabadiliko ya Hali ya Hewa alisisitiza ya kuwa ni lengo la jamii ya kimataifa kuhakikisha kuwepo maelewano mazuri miongoni ya watu, na vile vile kuhakikisha kuna mlingano wa kimaumbile kati ya wanadamu na mazingira asilia, mazingira ambayo uhai wetu huyategemea kumudu maisha.