Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mashirika ya kibinadamu yanasaidia kuondoa watu huko Kharkiv Ukraine

Mratibu wa Misaada ya Kibinadamu na Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Ukraine, Denise Brown (katikati kulia), akizungumza na wakazi wa Hroza ambako vita ya silaha inaendelea nchini Ukraine.
© UNOCHA/Saviano Abreu
Mratibu wa Misaada ya Kibinadamu na Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Ukraine, Denise Brown (katikati kulia), akizungumza na wakazi wa Hroza ambako vita ya silaha inaendelea nchini Ukraine.

Mashirika ya kibinadamu yanasaidia kuondoa watu huko Kharkiv Ukraine

Msaada wa Kibinadamu

Mashirika ya kibinadamu yanafanya kazi bila kuchoka kusaidia kuwaondoka raia katika eneo la Kharkiv ambalo siku za hivi karibuni limeshuhudia kuzorota kwa hali ya usalama na kutanda kwa wimbi la mapigano ambayo yamesababisha vifo vya raia na majeruhi ikiwa ni pamoja na watoto.

Video ya ofisi kuratibu misaada ya kibinadamu na masuala ya dharura ya Umoja wa Mataifa, OCHAinaanza kwa kuonesha watu wakishuka katika bus, hawa ni raia walioondolewa huko Kharkiv ambako mapigano kati ya Ukraine na Urusi yanaendelea. 

Uokoaji unaendelea kupitia mabasi yanayoratibiwa na mashirika ya misaada ya kibinadamu, watu binafsi wanaojitolea na serikali za mitaa. Kwa mujibu wa OCHA kati ya tarehe 10 na 15 Mei, karibu watu 2,400 wamefanikiwa kuhamishwa na kuletwa kwenye kituo cha muda ambapo wanapokea usaidizi. Mmoja wa watu hao ni Bibi huyu aitwaye Valentyna anayetujuza hali ilivyokuwa huko alipotoka..

Sisi kwetu ni Okhrimivka. Tunaishi pamoja na binti yangu ambaye ni mlemavu.  Kijiji chetu kilipigwa na makombora. Kila kitu kimeharibiwa. Ni nyumba 35 tu zimesalia. Wakati wa milipuko ya mabomu tulikuwa tukijificha ghorofa ya chini.”

Dmytro Filipskyi kutoka OCHA anasema zaidi ya watu 1,700 wameandikishwa kituoni hapo na wamepatiwa msaada, “Katika eneo hili utaona mashirika yasiyo ya kiserikali na ya misaada ya kibinadamu, mashirika ya Umoja wa Mataifa na ya kimataifa yakitoa msaada wa vifaa vya usafi na kujisafi, chakula, fedha, msaada wa kisaikolojia, ulinzi kwa watoto na makundi mengine yote. Mashirika yote yanahusika katika mchakato huu.” 

Mwanamke akipokea chakula cha msaada nchini Ukraine. (Maktaba)
© UNOCHA/Matteo Minasi
Mwanamke akipokea chakula cha msaada nchini Ukraine. (Maktaba)

Mashirika ya kibinadamu yalikusanya rasilimali kwa haraka ili kutoa usaidizi wa dharura kwa watu wanaokimbia kusaka usalama. Wamekuwa wakifanya kazi katika kituo hicho ambacho ndio nimekuwa kitovu cha kupokea watu wote wanaokimbia machafuko katika Jiji la Kharkiv na kuratibu usambazaji wa misaada ya kibinadamu tangu kuongezeka kwa mapigano tarehe 10 mwezi huu wa Mei.