Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

WHO: Kipindupindu chazidi kusambaa duniani

Watoto katika eneo la Lichinga Msumbiji wanasoma kuhusu hatari za kipindupindu
© UNICEF/Ricardo Franco
Watoto katika eneo la Lichinga Msumbiji wanasoma kuhusu hatari za kipindupindu

WHO: Kipindupindu chazidi kusambaa duniani

Afya

Shirika la Umoja wa Mataifa la Afya ulimwenguni WHO hii leo limetoa muhtasari wa ugonjwa wa kipindupindu ulimwenguni ambao mpaka sasa umetajwa kuenea katika mataifa 24 katika kanda tano za shirika hilo huku Afrika ikirekodi idadi kubwa ya wagonjwa. 

Kwa mujibu wa muhtasari huo kutoka Januari mosi mpaka April 28 mwaka huu kuna jumla ya wagonjwa 145,900 walioripotiwa huku vifo 1766 vikirekodiwa. 

Hatua mbalimbali za kupambana na ugonjwa huo zinaendelea kuchukuliwa ulimwenguni kote hata hivyo WHO wameeleza kuwa changamoto kubwa iliyopo sasa ni upungufu mkubwa wa chanjo ya kipindipindu ya kumeza.

“Tangu Januari 2023, maombi ya chanjo ya kumeza yameongezeka, dozi milioni 82 ziliombwa na nchi 15, ambazo ni karibu mara mbili ya dozi milioni 46 zinazozalishwa katika kipindi hiko. Mapema mwezi Machi, hifadhi ya kimataifa ya chanjo ilipungua. Kufikia tarehe 6 Mei 2024, hifadhi hiyo ina dozi milioni 3.2, ambazo ni chini ya lengo la kimataifa la hifadhi ya dozi milioni tano.”

Mwezi Januari mwaka huu  Shirika hilo la Afya ulimwenguni liliainisha kuibuka kwa ugonjwa huo wa kipindupindu duniani kuwa ni dharura daraja la tatu likiwa ni kiwango chake cha juu zaidi cha dharura. Na kulingana na idadi ya milipuko na kuendelea kuenea kwa ugonjwa huo kijiografia, pamoja na uhaba wa chanjo na rasilimali nyingine, WHO ilitathmini tena hatari katika kiwango cha kimataifa kuwa kubwa sana na ugonjwa huo unasalia kuainishwa kama dharura ya daraja la 3.