Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Takriban watu milioni 9 wamelazimika kukimbilia sehemu nyingine za Sudan au nchi jirani

Picha iliyopigwa kutoka juu ikionesha watoto na familia zao wakiwa wamesimama karibu na makazi ya muda kwenye kituo cha Khamsa Dagiga kwa watu waliokimbia makazi yao katika Mji wa Zelingei, Darfur ya Kati, Sudan.
© UNICEF/Spalton
Picha iliyopigwa kutoka juu ikionesha watoto na familia zao wakiwa wamesimama karibu na makazi ya muda kwenye kituo cha Khamsa Dagiga kwa watu waliokimbia makazi yao katika Mji wa Zelingei, Darfur ya Kati, Sudan.

Takriban watu milioni 9 wamelazimika kukimbilia sehemu nyingine za Sudan au nchi jirani

Amani na Usalama

Mwakilishi mkazi na Mratibu wa misaada ya kibinadamu wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan, Clementine Nkweta-Salami hii leo amewaambia waandishi wa habari mjini New York Marekani kwamba "baada ya zaidi ya mwaka mmoja wa vita, watu wa Sudan wamenaswa katika moto mkali wa ukatili,"huku njaa, magonjwa, na mapipigana “vikizidi kujongea.”

Akitoa taarifa mbele ya waandishi wa habari kuhusu hali katika eneo la El-Fasher, lililoko katika mji mkuu wa Darfur Kaskazini, Bi. Nkweta-Salami amesema, "mapigano yaliyotokea mwishoni mwa juma yaliripotiwa kusababisha makumi ya majeruhi ambao ni raia. Watu wengi zaidi walilazimika kuyakimbia makazi yao. Wengi wakisaka usalama sehemu ya kusini mwa jiji.”

Iwapo pande zinazohusika katika mzozo huu "hawatarudi nyuma, hii itakuwa na matokeo mabaya kwa raia 800,000 huko El-Fasher."

Nkweta-Salami alisema, "zaidi ya malori kumi, yakibeba kidhaa za chakula, lishe na vifaa vingine muhimu kwa zaidi ya watu 120,000 yamekuwa yakijaribu kufika jijini huko kwa wiki kadhaa sasa."

Kwa upande wa Khartoum, alisema, "imeharibiwa" na "hakuna mtu na hakuna kitu kilichosalia."

Mratibu huyo wa masuala ya kibinadamu alisema, "ukatili wa kutisha unafanywa kwa kuachwa bila kujali. Ripoti za ubakaji, mateso na ghasia zinazochochewa na ukabila zinaenea. Mashambulizi ya kiholela yanaua raia, wakiwemo watoto wadogo. Sudan hivi sasa ndiyo janga kubwa zaidi duniani la watu kuyahama makazi yao.”

Alisema takriban watu milioni 9, "wamelazimika kukimbilia sehemu nyingine za Sudan au nchi jirani."

Nkweta-Salami alibainisha kuwa operesheni zinazofanyika "kinyume na hali ya msimu wa mvua inyokaribia," huku barabara zikiwa "hazipitiki" katika mwezi Juni na Julai.

Alisema, "tunachojaribu kufanya ni kuhakikisha tunaweza kusema - tuna akiba hapa sio tu ya chakula,lishe, maji na usafi wa mazingira, vifaa vya WASH pia - ambayo itaturuhusu kushughulikia na mahitaji ya idadi ya watu kwa njia iliyojumuisha."

Nkweta-Salami alisema, “hivyo, je tuna hazina ya bidhaa? Hapana. Je, tunahitaji kupata hazina? Haraka iwezekanavyo."

Tarehe 15 mwezi Aprili 2023, mapigano makali yalizuka kati ya Jeshi la Sudan (SAF) na Jeshi la Wanajeshi wa Msaada wa Haraka (RSF) nchini Sudan, na kusababisha zaidi ya watu milioni 8.6 kuyahama makazi yao, wakiwemo wakimbizi wa ndani (IDPs), waomba hifadhi na wakimbizi. Mgogoro huu ulizidisha changamoto nyingi zilizopo Sudan, ikiwa ni pamoja na migogoro inayoendelea, milipuko ya magonjwa, kuyumba kwa uchumi na kisiasa, na dharura ya mabadiliko ya tabianchi.