Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Suluhu ya kudumu ya amani inahitajika Yemen ambako kipindupindu kinasambaa: UN

Miaka ya mizozo imewaacha mamilioni kote Yemen wakihitaji msaada wa kibinadamu na ulinzi.
© UNICEF/Waleed Qadari
Miaka ya mizozo imewaacha mamilioni kote Yemen wakihitaji msaada wa kibinadamu na ulinzi.

Suluhu ya kudumu ya amani inahitajika Yemen ambako kipindupindu kinasambaa: UN

Amani na Usalama

Mateso ya raia nchini Yemen, ambayo yamedumu kwa takriban muongo mmoja wa vita, bado ni makali na yanazidishwa na mlipuko wa kipindupindu, ameonya leo afisa mkuu wa Umoja wa Mataifa wa masuala ya kibinadamu.

Martin Griffiths, Mratibu wa Misaada ya Dharura wa Umoja wa Mataifa, amesisitiza hitaji muhimu la juhudi za amani endelevu wakati wa akitoa tarifa kwenye mkutano Baraza la Usalama hii leo uliofanyika mjini New York Marekani .

Amesema "Mgogoro nchini Yemen umekuwa kichocheo kikuu cha mahitaji ya kibinadamu. Umedhoofisha sana uchumi wa nchi, umepunguza nusu ya vituo vyake vya afya, umehamisha mamilioni ya watu, na kuruhusu njaa na magonjwa kushamiri chini ya hali hizi, ".

Ameendelea kusema kwamba kinachozidisha changamoto hizi ni mlipuko wa kipindupindu unaosambaa kwa kasi, huku zaidi ya visa 40,000 vinavyoshukiwa na kuongezeka kwa idadi ya vifo, hasa katika maeneo yanayodhibitiwa na Wahouthi pia wanajulikana kama Ansar Allah, ambako mamia ya maambukizo mapya yanaripotiwa kila siku.

Bwana. Griffiths, ambaye pia ni mkuu wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu OCHA, katika tarifa yake ameangazia wasiwasi kuhusu mvua kubwa zinazokaribia kunyesha na mafuriko yatakayozidisha mgogoro katika wiki zijazo.

Watu kufurushwa na operesheni za kijeshi vinashika kazi Rafah
© UNRWA
Watu kufurushwa na operesheni za kijeshi vinashika kazi Rafah

Kivuli cha vita ya Gaza

Hans Grundberg, Mjumbe Maalumu wa Katibu Mkuu kwa ajili ya Yemen, pia ametoa taarifa kwa Baraza la Usalama, akibainisha kuwa mwezi Disemba, Serikali na Ansar Allah wote walikubaliana "kuweka ahadi ikiwa ni pamoja na kusimamisha vita nchi nzima.”

Amesema ahadi hizi zinalenga kuhakikisha unafuu wa kibinadamu kwa Wayemen na kuanzisha mchakato shirikishi wa kisiasa ili kumaliza mzozo huo kwa njia endelevu.

Hata hivyo, changamoto zinaendelea kutokana na vita huko Gaza na ukosefu wa utulivu wa eneo hilo, na matangazo ya Ansar Allah ya kupanua wigo wa mashambulizi ni "uchochezi wa kutisha katika hali ambayo tayari ni tete."

Kinda hatua zilizopigwa nchini Yemen

Akitafakari juu ya athari za migogoro ya kikanda, Mratibu wa Misaada ya Dharura wa Umoja wa Mataifa Griffiths amesisitiza haja ya kulinda maendeleo yaliyopatikana nchini Yemen.

Amesisitiza kuwa "Hatuwezi kuruhusu kukatika kwa biashara ya kimataifa kuzunguka Bahari ya Sham na kutatiza juhudi za amani nchini Yemen".

Bwana Griffiths ameonyesha wasiwasi wake mkubwa kwa raia wa Yemen, akitetea uungwaji mkono wa pamoja wa kimataifa na kukomesha hatua za uhasama za kiuchumi, pamoja na pande zinazozozana kufanya sehemu yao ili kupunguza hali hiyo.

Amehimiza kuanza tena mauzo ya mafuta ili kuleta utulivu wa uchumi na kuimarisha huduma muhimu za umma.

Martin Griffiths (kwenye skrini), mkuu wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu OCHA, akiakizungumza katika mkutano wa Baraza la Usalama kuhusu Yemen.
UN Photo/Manuel Elías
Martin Griffiths (kwenye skrini), mkuu wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu OCHA, akiakizungumza katika mkutano wa Baraza la Usalama kuhusu Yemen.

Tafakari ya binafsi

Katika tafakari ya binafsi, Bwana. Griffiths, ambaye anajiandaa kuachia ngazi mwezi Juni kutokana na sababu za kiafya, ameangazia umuhimu wa Yemen kwake akisema "Taarifa yangu ya kwanza kwa Baraza la Usalama kama Mratibu wa Misaada ya Dharura, karibu miaka mitatu iliyopita, ilikuwa juu ya Yemen. Inaonekana inafaa kwamba nizungumze nawe kuhusu Yemen leo kwa moja ya tarifa zangu wa mwisho." 

Ameongeza kuwa "Baada ya karibu miaka 10 ya migogoro mikali, watu wa Yemen wanastahili afueni," amehitimisha,tarifa hiyo akisisitiza umuhimu wa kuwalinda raia, kuhakikisha upatikanaji wa misaada ya kibinadamu, na kusonga mbele kuelekea amani ya kudumu.