Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

TANZBATT-11 ya MONUSCO yapatia huduma za afya wakazi na wakimbizi huko Beni, DRC

Kikosi cha 11 cha walinda amani wa Umoja wa Mataifa kutoka Tanzania, TANZBATT-11 wakipatia huduma za afya wakazi wa kijiji cha Matembo huko Beni jimboni Kivu Kaskazini, mashariki mwa DRC.
MONUSCO/TANZBATT 11
Kikosi cha 11 cha walinda amani wa Umoja wa Mataifa kutoka Tanzania, TANZBATT-11 wakipatia huduma za afya wakazi wa kijiji cha Matembo huko Beni jimboni Kivu Kaskazini, mashariki mwa DRC.

TANZBATT-11 ya MONUSCO yapatia huduma za afya wakazi na wakimbizi huko Beni, DRC

Afya

Huko nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, kikosi cha 11 cha walinda amani kutoka Tanzania, TANZBATT-11 kinachohudumu kwenye ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani nchini humo, MONUSCO wametekeleza wajibu wao wa kulinda raia kwa kuwapatia huduma ya matibabu kwenye Kijiji cha Matembo kilichoko mjini Beni jimboni Kivu Kaskazini.

Shughuli hii ya kutoa  huduma ilianza majira ya saa tatu asubuhi hadi saa nane adhuhuri kwa saa za hapa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, ambapo wanakijiji wapatao 50 walinufaika na huduma hizo. Miongoni mwao ni Kavira Malyamkono. 

Bi. Malyamkono akiwa amembeba mtoto wake anasema, “mimi ni mkulima shambani, waasiw wanatukimbiza hivyo hatuna fedha na tunakosa chakula. Lakini tunashukuru watanzania kutoka MONUSCO wamekuja na kutupatia msaada wa dawa.” 

Huduma ya TANZBATT-11 kwenye hospitali hii ya kijiji inafuatia ombi lake kwa walinda amani wa Umoja wa Mataifa kutoka Tanzania kutokana na changamoto za uhaba wa vifaa vya matibabu, dawa na wagonjwa kushindwa kulipia gharama za matibabu. 

Kikosi cha 11 cha walinda amani wa Umoja wa Mataifa kutoka Tanzania, Tanzbatt11 wakipatia huduma za afya wakazi wa kijiji cha Matembo huko Beni jimboni Kivu Kaskazini, mashariki mwa DRC.
MONUSCO/TANZBATT-11
Kikosi cha 11 cha walinda amani wa Umoja wa Mataifa kutoka Tanzania, Tanzbatt11 wakipatia huduma za afya wakazi wa kijiji cha Matembo huko Beni jimboni Kivu Kaskazini, mashariki mwa DRC.

Daktari wa hospitali hii ya Kijiji katembo nyambezia anasema “watanzania hawa walifika hapa Beni na tukawapatia wito wa msaada wa dawa, na ndipo waliitikia wito wetu haraka. Tayari wamefika hapa na kutuletea dawa. Tuna wakimbizi pia wanafika hapa. Watu hawana fedha hata ukiwapatia risiti ya malipo hawawezi kulipa. Na sisi hatuwezi kuwakatalia huduma wagonjwa.” 

Anaendelea kusema kuwa “tutafurahi sana iwapo huduma hii itaendelea, hasa dawa. WAkimbizi wanatoka mbali na wana matatizo mengi. Wasaidie hata kupatia kitu kidogo wahudumu wa afya ili waweze kuendelea kutoa huduma kwenye kituo cha afya. Wakimbizi ambao wanatoka maeneo mengine kama vile Matembo, Mutaba na kwingineko.” 

Wananchi waliojitokeza kwa huduma za matibabu walibainika kuwa na magonjwa kama vile malaria, kisukari, homa ya matumbo, na shinikizo la damu. Luteni Albert Ngulla ni Mkuu wa kikundi cha madaktari wauguzi wa TANZBATT-11. 

“Tumekuja kwa ajili ya kutoa huduma za afya kwenye zahanati ya Matembo na tumetoa huduma za vipimo kw amagonjwa yasiyo ya kumbukiza kama vile kisukari na kiharusi na vile vile magonjwa yanayojikita zaidi eneo hili kama Malaria na pia tumewapatia dawa.” 

TANZBATT-11 ilipokea jukumu la ulinzi wa amani kwenye eneo hili la Beni, Kivu Kaskazini tarehe 15 mwezi Machi mwaka huu kutoka kwa watangazuli wao TANZBATT-10 

 

Taarifa hii imeandaliwa na Kapteni Fadhila Nayopa, Afisa Habari TANZBATT-11