Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

GAZA: Miezi 6 ya mzozo Guterres akemea matumizi ya Akili Mnemba

Mvulana anakimbia katika mitaa iliyoharibiwa ya Gaza.
© UNRWA/Ashraf Amra
Mvulana anakimbia katika mitaa iliyoharibiwa ya Gaza.

GAZA: Miezi 6 ya mzozo Guterres akemea matumizi ya Akili Mnemba

Amani na Usalama

Kesho kutwa jumapili ikiwa ndio itatimu miezi sita ya mzozo wa Gaza, huko Mashariki ya Kati, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres hii leo amezungumza na waandishi wa habari jijini New York, Marekani akirejelea wito wake wa sitisho la mapigano kwa misinigi ya kiutu, kuachiliwa kwa mateka wote bila masharti, ulinzi wa raia na misaada ya kiutu ifikie walengwa bila vikwazo vyovyote huku akikgusia pia Israeli kutumia akili mnemba kwenye operesheni zake. 

Tweet URL

Hakuna kinachohalalisha mashambulizi ya Hamas Oktoba 7 

Guterres akianza hotuba yake kwa kuelezea kuwa Jumapili hii inatimu miezi sita tangu mashambulizi hayo na kuelezea kuwa tarehe 7 Oktoba ni siku ya machungu kwa Israel na dunia, kwani Umoja wa Mataifa na yeye binafsi wanaomboleza vifo vya waisrael 1,200 waliouawa hadi sasa. 

Hakuna kinachohalalisha mashambulizi yale ya Hamas, amesema Guterres akisema pia katika kipindi cha miezi sita pia wapalestina zaidi ya 32,000 wameuawa na wengine zaid iya 75,000 wamejeruhiwa. Maisha ya watu yametwamishwa na heshima ya sheria ya kimataifa ya kibinadamu imesambaratishwa 

Milango ya misaada inapofungwa ile ya njaa inafunguliwa 

Akarejelea ziara yake ya hivi karibuni kwenye kivuko cha Rafah ambako anasema nilikutana na wasaidizi wa kiutu wabobezi walionieleza wazi kuwa janga hili na machungu ya Gaza si ya kawaida na hawajawahi kushuhudia kokote. 

Na zaidi ya yote anasema aliona misururu mirefu ya malori yenye shehena za misaada yakiwa yamezuiwa kuingia Gaza. Amesema pindi milango ya misaada inapofungwa, milango ya njaa inafunguliwa. Zaidi ya watu milioni moja wanakabiliwa na njaa. Watoto hivi sasa wanakufa kwa njaa na kukosa maji. Hakuna kinachohalalisha adhabu hii ya jumla kwa wananchi wa Palestina. 

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres akizungumza na waandishi wa habari 5 Oktoba 2024 kuelekea miezi 6 ya mzozo Gaza.
UN /Eskinder Debebe
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres akizungumza na waandishi wa habari 5 Oktoba 2024 kuelekea miezi 6 ya mzozo Gaza.

Katu Akili Mnemba isitumike vitani, Azimio la Baraza la Usalama litekelezwe 

Amezungumzia pia matumizi ya Akili Mnemba kwenye vita hivyo akisema. “ninachukizwa sana na ripoti kuwa kampeni ya mashambulizi ya jeshi la Israel inahusisha Akili Mnemba kama mbinu ya kutambua maeneo lengwa, hasa kwenye makazi ya watu wengi, na kusababisha idadi kubwa ya vifo.”

Amesema kuwa hakuna sehemu ya maamuzi yoyote ya uhai au vifo yanayoathiri familia nzima yanapaswa kuamuliwa na mchakato wa kimahesabu usio na hisia

Nimeonya kwa miaka mingi juu ya hatari ya kutumia Akili Mnemba kwenye silaha na kupunguza dhima muhimu ya binadamu, “AI inapaswa kutumika kwa manufaa ya dunia; na sio kuchangia kwenye kusongesha vita kwa kiwango cha juu na kuficha uwajibikaji.”

Wafanyakazi wa UNRWA mjini Amman, Jordan, wanahudhuria hafla ya kuwakumbuka wafanyakazi wenzao waliopoteza maisha huko Gaza.
UNRWA/Shafiq Fahed
Wafanyakazi wa UNRWA mjini Amman, Jordan, wanahudhuria hafla ya kuwakumbuka wafanyakazi wenzao waliopoteza maisha huko Gaza.

Waliouawa pia ni watumishi wanaotoa misaada

Amekumbusha kuwa wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa na mashirika ya kiraia na waandishi wa habari nao wameuawa kwenye mzozo huo akisema kuwa “watoa misaada ya kiutu 196 wameuawa wakiweko wafanyakazi zaidi ya 175 wa Umoja wa Mataifa, wengi wao wakiwa ni wale shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wapalestina, UNRWA.”

Na zaidi ya yote amesema vita dhidi ya habari imeongeza machungu.. kuficha ukweli na kurushiana lawama. Kuwanyima waandishi wa habari wa kimataifa kibali cha kuingia Gaza kunaruhusu kusambaa kwa habari potofu na za uongo.

Mbinu za kijeshi zibadilike

Na kufuatia mauaji ya kutisha ya wahudumu saba wa shirika la kiutu la World Central Kitchen, Katibu Mkuu amesema tatizo kuu si ni nani alikosea bali ni “mkakati wa kijeshi na kanuni zilizoko ambazo zinaruhusu makosa kama hayo kutokea tena na tena.”

“Kusaka suluhu ya makosa hayo kunahitaji uchunguzi huru na mabadiliko ya dhati na yanayopimika kwenye eneo hilo,” amesema Guterres.

Amesema Umoja wa Mataifa umejulishwa na serikali ya Israel kuwa hivi sasa inajipanga kuruhusu “ongezeko la dhahiri” la misaada kuingia Gaza akisema kuwa ni matumaini yangu ongezeko hilo litafanyika haraka.

Ametamatisha hotuba yake ya dakika 7 kwa kutaka pia uchunguzi huru wa kilichotokea Gaza, utekelezaji wa kikamilifu wa azimio la wiki iliyopita la Baraza la Usalama la kutaka sitisho la mapigano na misaada ifikie walengwa kwani baa la njaa linajongea Gaza.