Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mtu 1 huuawa kila saa kwa bomu au kilipuzi - UN

Mfanyakazi wa UNMAS akichunguza mabomu ya kutegwa ardhini, jimbo la Equatoria kati, Sudan Kusini.
© UN Photo/Isaac Billy
Mfanyakazi wa UNMAS akichunguza mabomu ya kutegwa ardhini, jimbo la Equatoria kati, Sudan Kusini.

Mtu 1 huuawa kila saa kwa bomu au kilipuzi - UN

Amani na Usalama

Mabomu, vilipuzi na vifaa vingine vya mlipuko vinaendelea kuua na kujeruhi watu katika maeneo mengi yenye changamoto kubwa za migogoro duniani na matokeo yake vifaa hivyo vya mlipuko, kwa wastani hukatili Maisha ya mtu mmoja kila saa, na waathirika wakubwa wakiwa ni watoto kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa.

Ikiwa leo ni siku ya kimataifa ya uelimishaji kuhusu mabomu na msaada wa kuchukua hatua mashirika ya kibinadamu, operesheni za kulinda amani za Umoja wa Mataifa na wafanyikazi wa Umoja wa Mataifawanasema nvifaa vya mlipuko vinaongezeka kila mara duniani kote  na mabobu yakiwemo ya kutegwa ardhini yanatishia raia.

Mwaka huu wa 2024, maadhimisho ya Siku hii ya Kimataifa ambauo kila mwaka huadhimishwa Aprili 4 yanaweka mkazo maalum katika kuongeza ufahamu wa mahitaji na haki za watu wenye ulemavu katika mazingira ya migogoro. 

Azimio nambari 2475 la Baraza la Usalama lililopitishwa miaka mitano iliyopita linatoa wito kwa nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa kuhakikisha usalama wa watu wenye ulemavu, kuwapatia fursa ya kuwarekebisha na kuwajumuisha katika shughuli za kuzuia migogoro na kujenga amani.

Kauli mbiu ya mwaka huu - Kulinda maisha, kujenga amani.

Kupitia ujumbe wake wa siku ya mwaka huu iliyobeba maudhui “Kulinda maisha , kujenga amani”  Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesisitiza kuwa “kuna tishio kubwa linaloletwa na mabomu ya ardhini na mabaki ya silaha za vita katika maeneo yenye migogoro duniani kote, kuanzia Afghanistan, Myanmar, Sudan hadi Ukraine, Colombia na Gaza.” 

Ameongeza kuwa hata baada ya mizozo kukoma, silaha hizi zinaendelea kuhatarisha maisha, kuzuia misaada ya kibinadamu, na kuzuia maendeleo. 

Ujumbe wake pia unasifu juhudi za wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa  wa ofisi ya uteguzi wa mabomu UNMAS na unahimiza kuungwa mkono kwa mipango inayolenga kuondoa silaha hizi, kuhakikisha njia salama kwa jamii, na kulinda makundi yaliyo hatarini, ikiwa ni pamoja na wale wenye ulemavu. 

Katibu Mkuu amesema Nchi Wanachama zinatakiwa kuidhinisha Mkakati wa Umoja wa Mataifa wa Utekelezaji wa hatua dhidi ya mabomu na kutekeleza kikamilifu mikataba ya kimataifa kama vile Mkataba wa Kupiga Marufuku ya matumizi ya mabomu, Mkataba wa Mashambulizi ya mabomu mtawanyiko, na Mkataba wa matumizi ya baadhi ya silaha za kawaida. 

Amesema “Lengo kuu ni kuondoa silaha hizi hatari duniani kote, akisisitiza juhudi za pamoja katika misingi ya nchi kwa nchi na jamii kwa jamii.”

Nusu ya waathirika wa vifaa vya milipuko ni watoto

Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa katika miongo ya hivi karibuni, operesheni za kijeshi zimezidi kufanyika katika maeneo yenye watu wengi, ikiwemo miji mikubwa, na kutokana na matumizi ya silaha za milipuko, raia ambao wengi wao ni watoto wanauawa na kujeruhiwa.

Majeraha yanaypjitokeza katika kesi kama hizo kawaida ni mabaya sana kuanzia kuungua vibaya hadi kupoteza viungo kama miguu na mikono, na kupoteza uwezo wa kusikia au kuona. 

Kwa kuongezea, watoto ambao ni waathirika wakubwa wa silaha za vilipuzi wanaweza kuteseka kutokana na changamoto ya shinikizo baada ya kiwewe na  wasiwasi na kuhitaji msaada wa kisaikolojia.

Matumizi ya silaha za vilipuzi yanaweza pia kuathiri kwa njia isiyo ya moja kwa moja maisha ya watoto wanaoishi katika maeneo ya vita. 

Mashambulizi kwenye maeneo ya makazi ya watu huharibu miundombinu ya raia kama nyumba, shule, hospitali, vifaa vya usambazaji wa maji, na mitambo ya umeme.

Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa hata baada ya mwisho wa mizozo hiyo, mabomu na mabaki ya silaha za vita ambazo hazijalipuka zinaendelea kuwa tishio kwa maisha na afya ya binadamu. 

Watoto wana hatari zaidi kwa sababu mara nyingi wanacheza nje, wanapendezwa na vitu visivyojulikana na vya ajabu, na hawajui kwamba vinaweza kuwa hatari sana kwao.

Taarifa huokoa maisha

Jumatano wiki hii, Shirika la Mpango wa Maendeleo la Umoja wa Mataifa UNDP na kitengo cha shirika la habari la Uingereza BBC Media Action, kwa msaada wa serikali ya Japan, zilitangaza kuanzishwa kwa kampeni ya kuwafahamisha wakazi wa Ukraine kuhusu hatari inayoletwa na mabomu na vifaa vya milipuko.

Kampeni, hiyo iliyoandaliwa kwa ushirikiano na Huduma ya Serikali ya Ukraine kwa Hali za Dharura na mashirika muhimu yasiyo ya kiserikali katika eneo hilo, imeandaliwa ili kufikia wakazi wote wa nchi hiyo. 

Uangalifu hasa utatolewa kwa makundi ya watu yaliyo hatarini zaidi na mikoa yenye ongezeko la idadi ya ajali zinazohusiana na vifaa vya milipuko.

Hatua ya awali ya kampeni hiyo ilianza Desemba 2023, kwa usambazaji wa vifaa vya elimu kupitia televisheni, redio, mitandao ya kijamii na matangazo ya nje utaanza kufanywa mwezi Juni mwaka huu.