Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wakimbizi wa ndani Sudan wataka vita ikome warejee nyumbani

Kamishna Mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR Filippo Grandi (kati), akiwa ziarani nchini Sudan.
UNHCR Video
Kamishna Mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR Filippo Grandi (kati), akiwa ziarani nchini Sudan.

Wakimbizi wa ndani Sudan wataka vita ikome warejee nyumbani

Wahamiaji na Wakimbizi

Namkumbuka mama yangu na ndugu zangu na ninataka kurejea nyumbani, amesema Rabia Mohammed Ahmed mkimbizi wa ndani nchini Sudan akizungumza akiwa kwenye kituo cha wakimbizi cha Beet AlShabab mjini Port Sudan.

Bi. Ahmed alikuwa anaelezea masaibu yake wakati wa ziara ya Kamishna Mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR Filippo Grandi, ziara iliyokuwa na lengo la kuangalia masaibu yanayokumba wakimbizi  hao wa ndani.

Rabia Mohammed Ahmed mkimbizi wa ndani nchini Sudan akizungumza akiwa kwenye kituo cha wakimbizi cha Beet AlShabab mjini Port Sudan.
UNHCR Video
Rabia Mohammed Ahmed mkimbizi wa ndani nchini Sudan akizungumza akiwa kwenye kituo cha wakimbizi cha Beet AlShabab mjini Port Sudan.

Mapigano yalianza lini?

Mwezi Aprili mwaka jana wa 2023 wananchi waliamshwa na mapigano kwenye mji mkuu Khartoum kati ya majenerali wawili: mmoja kutoka jeshi la serikali na mwingine akiongoza wanamgambo wa Rapid Support Forces. Miezi kumi tangu mzozo huo kuzuka, takribani watu milioni 8 kati ya raia wote milioni 45.7 wa Sudan ni wakimbizi ambapo milioni 1.5 kati yao wamekimbilia nje ya nchi hadi Jamhuri ya Afrika ya Kati, Chad, Misri na Ethiopia huku wengine wamesalia ndani.

Bi. Ahmed akiendelea anasema kuwa “kwa kuwa hakuna dalili za haya mapigano kukoma wakati wowote mjini Khartoum, bora niondoke nchini mwangu kabisa. Hakuna utulivu au amani; kuna jambo gani muhimu zaidi kuliko amani? Haijalishi uko katika hali gani, unahitaij amani na utulivu, ndio hicho.”

Soundcloud

Grandi uso kwa uso na wakimbizi wa ndani

Grandi akiwa hapa anamtembelea Bi. Ahmed na katika mazungumzo kati yao kupitia mkalimani akamweleza kuwa tunataka kusaidi kidogo hivyo tungependa kusikia kutoka kwako.

Na hivyo akizungumza kupitia mkalimani, Rabia akasema kuwa wao ni familia ya watu watatu na mume wake hayuko.

Na Grandi akizungumza kupitia mkalimani akasema tunajaribu kutafuta fedha na natumai mume wako atajiunga nawe karibuni.”

Mkuu huyo wa UNHCR akasema  "unachoona hapa nyuma yangu ni eneo dogo tu linalohifadhi makumi ya watu. Lakini kuna maeneo mamia ya mamia ya aina hii takribani nchini kote. Wakimbizi wengi wanaishi na jamaa zao, na marafiki kwenye makazi yaliyojaa kupita kiasi.”

Kutoka hapa Kamishna Mkuu huyu wa UNHCR akaelekea kituo kingine cha kupokea wakimbizi cha Al Salam kilichoko eneo la Kassala hapa Sudan. Ni kwenye jengo lenye ghorora 4 n wakimbizi hapa, wanaume, wanawake, na watoto,  nyuso zao hazina matumaini.

Hatuna taarifa za hali za ndugu zetu Khartoum

Grandi anafika na kulakiwa na wanawake waliokuweko nje ya jengo hili.. wanazungumza kwa sauti ya chini. Kando familia nyingine inatazama kwa matumaini kuwa bila shaka ujio huu utawaletea mambo mazuri.

Mkuu huyu wa UNHCR akaingia katika moja ya vyumba vya jengo hili na kuwa na mazungumzo na wanawake na wanaume. Akasikika akiwauliza, je mna ndugu wowote waliobakia Khartoum? Na je mna taarifa zozote kuhusu nyumba na mali zenu? Mali ziko vizuri au hapa? Na jibu likawa  hapana!

Kamishna Mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR Filippo Grandi(wa pili kutoka kulia), akiwa ziarani nchini Sudan.
UNHCR Video
Kamishna Mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR Filippo Grandi(wa pili kutoka kulia), akiwa ziarani nchini Sudan.

Tumepoteza taifa letu, vita ikome turejee makwetu

Mmoja wa wanawake waliokuwa wanazungumza na Grandi ni Amani Omer Hussein ambaye amesema, “tumepoteza taifa letu. Maisha yetu yalikuwa yamebarikiwa, lakini angalau bado tuko hai, tunashukuru Mungu. Mapigano Khartoum yalishtua nchi nzima. Khartoum ni kitovu cha kila kitu. Mapigano yamesababisha bei za bidhaa kuongezeka, na kufanya kila kitu kisiweze kuendelea. Tunaomba Mungu akomeshe vita ili kila mtu aweze kurejea nyumbani. Nchi yetu inaumia hakuna amani.”

Kituo cha tatu cha Grandi kikawa kambi ya wakimbizi ya Wad Sharifey huko Kassala nchini Sudan. Wengi hapa ni vijana na Jengo ambamo wanaishi wakimbizi lina kuta lakini bila madirisha.

Vitanda ni vya “teremka tukaze,” au vile vinavyotengenezwa kwa kupitanisha kamba.  Grandi anapata fursa ya mazungumzo na wao kupitia mkalimani. Kisha akatoka na kusema, "ni muhimu kurudia tena wito wetu, hasa kwa viongozi wa kijeshi nchini Sudan, ni lazima warejee kwenye meza ya mazungumzo, warejee kwenye mwelekeo wa mazungumzo ya dhati na yenye maana. Angalau kwa kuanzia na makubaliano ya kusitisha mapigano ili watu waweze kurejea majumbani mwao. Kuna mamilioni ya waliofurushwa makwao.”

Mkuu huyo wa UNHCR akasema na wakati huo huo kazi hiyo ikiendelea, ni vema kupatia msaada muhimu kwa wale walioathiriwa na mzozo, kuanzia wakimbizi hadi wakimbizi wa ndani na wenyeji wanaowapatia hifadhi ambao mara nyingi huwa na rasilimali kidogo. Kisha tufanye kazi na mamlaka za maeneo na serikali kuu kusaidia watu hawa.

Kwa watoto, licha ya kuwa ukimbizini, mmoja wao anachora gari.. penginepo ndoto ya kulimiliki siku za usoni.