Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Haki za watoto zizingatiwe na zilindwe bila kujali waliko - UN

Watoto wakimbizi wa Sudan Kusini wakitembea pamoja baada ya kutoka shuleni kwenye makambi ya wakimbizi ya Nyumanzi Uganda (Maktaba)
© UNICEF/Jiro Ose
Watoto wakimbizi wa Sudan Kusini wakitembea pamoja baada ya kutoka shuleni kwenye makambi ya wakimbizi ya Nyumanzi Uganda (Maktaba)

Haki za watoto zizingatiwe na zilindwe bila kujali waliko - UN

Haki za binadamu

Visa vya kutisha vya ukatili dhidi ya watoto hususan waliofurushwa makwao maeneo mbalimbali duniani vimesababisha viongozi waandamizi wa Umoja wa Mataifa kurejelea wito wao wa ulinzi wa watoto na kuhakikisha wakati wowote ule haki zao zinalindwa kwa mujib uwa sheria ya kimataifa, na wakati huo huo watendao uhalifu huo wasikwepe sheria.

Mwaka 2022, Umoja wa Mataifa ulithibitisha matukio 27,180 ya ukiukwaji mkubwa wa haki za watoto, wakitumika kwenye mizozo, wakiuawa, wakikatwa viungo na kuachwa na ulemavu, ubakaji, ukatili wa kingono, kutekwa nyara, shule zao kushambuliwa n ahata kunyimwa misaada ya kibinadamu.

Virginia Gamba, ambaye ni Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu Watoto walio kwenye mizozo ya kivita ametoa taarifa hizo wakati akihutubia Kamati ya Tatu ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, kamati ambayo imenza kikao baada ya kumalizika kwa Mjadala Mkuu wa mkutano wa 78 wa Baraza Kuu, UNGA78.

Cha kusikitisha ni kwamba miongoni mwa matukio hayo, zaidi ya watoto 2,300 walikumbwa na matukio kadhaa ya unyanyasaji, na miongoni mwa matukio hayo pia, 2880 yalitokea mwaka 2021 lakini yalithibitishwa mwaka jana.

Watoto wakimbizi hatarini zaidi

Bi. Gamba amesema watoto wakimbizi wako hatarini zaidi kwani ukimbizi mara nyingi huchochea ukiukwaji wa haki na unyanyasaji dhidi ya watoto, kama vile kutumikishwa vitani, kutekwa nyara, ukatili wa kingono na kusafirishwa kiharamu.

Halikadhalika, watoto wanapofurushwa makwao, huduma za msingi kama vile elimu na afya huvurugika na wakati huo huo wananyimwa misaada ya kibinadamu.

Sababu zitokanazo na tabianchi kama vile majanga ya kimazingira na uwepo wa mabomu ya kutegwa ardhini, bila kusahau vilipuzi ambavyo bado havijalipuka, huchochea zaidi hatarini hizo.

Tweet URL

Wote wana umri wa chini ya miaka 18

Bi. Gamba ametoa wito kwa nchi kutambua kuwa watu wote wenye umri wa chini ya miaka 18 ni watoto na wapatiwe ulinzi maalum kwa mujibu wa Mktaba wa Kimataifa wa Haki za Mtoto, CRC.

Watoto wenye umri wa kati ya miaka 13 hadi 18 mara nyingi huchukuliwa kuwa ni watu wazima au wanakabiliwa nah atua za kukabilia ugaidi huku haki zao za kuwa watoto zikipuuzwa.

Ushauri mwingine ni jitihada zaidi za kukusanya data na taarifa za karibu ili kufunga pengo lililoko la taarifa na kuhakikisha ulinzi na usaidizi kwa watoto wote wakiwemo wale wenye ulemavu.

Muda unayoyoma

Najat Maalla M'Jid, huyu ni Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu Ukatili dhidi ya Watoto, naye pia alihutubia Kamati hiyo ya Tatu ya UNGA akisisitiza kuwa watoto wanalipa gharama kubwa sio tu wakati wa vita bali pia wakati wa ukosefu wa utulivu wa kisiasa na uchumi unapoporomoka.

Ameelezea wasiwasi wake kuwa maendeleo ya kutokomeza ukatili dhidi ya watoto ifikapo mwaka 2030 yanaponyoka, na ametoa wito kwa hatua za dharura kubadili mwelekeo.

Mwakilishi huyu amekuwa akijikita zaidi kwenye kusongesha ulinzi wa watoto dhidi ya ghasia kwa kutumia uchechemuzi, ushauri, kujenga ushirikiano wa utekelezaji wa majukumu katiya nchi na jamii.

“Ushirikiano wangu na nchi wanachama umeangazia athari chanya na faida za kuwekeza kwenye sekta mtambuka za ulinzi wa watoto na huduma za kuzuia ghasia kwa watoto bila kujali hadhi yao,” amesema Bi. M’Jid.

Tufikirie upya safari na utalii

Ripoti yake kwa Baraza Kuu imejikita katika kulinda watoto kwenye muktadha wa safari na utalii.

Ingawa safari na utalii ni muhimu kwa maendeleo ya jamii na dunia, sekta hiyo ina changamoto kubwa katika ulinzi wa watoto.

Bi. M'Jid ametaka jamii kuridhia msimamo usiovumilika dhidi ya utumikishaji watoto kupitia dhima mbalimbali katika sekta za safari na utalii.

“Watoto wanaweza kuwa eneo la wazi, wakiuza vitu vya kumbukizi la eneo mitaani, ufukweni, wakibeba mabegi na meza. Wanaweza kuwa ‘nyuma ya pazia’ wanafanyika kazi za kusafisha vyombo, au vyumba vya wageni. Au pengine wanaweza kuwa wanatumikishwa kwenye maduka ya kuchua misuli, madanguro au hata ndani ya nyumba zao ambako wanatumikishwa kingono.”

Amesisitiza kuwa sekta hiyo ina fursa ya kudhibiti ukatili wa watoto kupitia mnyororo wake wa thamani ambao ulijijengea baada ya janga la coronavirus">COVID-19, hivyo fursa hiyo isipotee.